TANGAZO


Friday, May 23, 2014

Kamishna wa Sensa ya Watu na Makazi, Hajjat Amina Mrisho, atoa taarifa kuhusu Chapisho la Tatu la Taarifa za Msingi za Kidemografia, Kijamii na kiuchumi linalotokana na sensa ya 2012

Kamishna  wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka, Hajjat Amina Mrisho, akizungumza katika moja ya mikutano yake na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam.
 
UZINDUZI wa chapisho la Tatu la Taarifa za Msingi za Kidemografia, Kijamii na kiuchumi linalotokana na Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 (Basic Demographic and Socio-Economic Profile) katika ngazi ya Taifa uliokuwa umepangwa kufanyika siku ya Ijumapili tarehe 25 Mei, 2014 umeahirishwa.
 
Uzinduzi huo sasa utafanyika rasmi tarehe 10 Juni, 2014 katika ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwl. Julius Nyerere uliopo mtaa wa Shaaban Robert jijini Dar es Salaam kuanzia saa 3:00 asubuhi.
 
Mgeni rasmi katika uzinduzi huo atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.
 
Aidha, uzinduzi huo unatarajiwa kuhudhuriwa na watu wapatao mia tano (500) ambao ni pamoja na Viongozi mbalimbali wa ngazi za juu Serikalini, Mabalozi, Wadau wa Maendeleo, Viongozi wa Dini, Viongozi wa Vyama vya Siasa, Wawakilishi wa Mashirika yasiyo ya Serikali na Wadau wa Takwimu nchini.
 
Kwa kifupi chapisho hili linatoa viashiria mbalimbali ambavyo ni pamoja na Kiwango cha uzazi, umri wa kuishi wa mtanzania, vifo vya watoto wachanga, kiwango cha vifo vya wakina mama vitokanavyo na uzazi na taarifa nyingine kwa ajili ya kupanga mipango ya maendeleo.
 
Chapisho hili ni mwendelezo wa machapisho mbalimbali yanayotolewa na Ofisi zetu mbili yaani Ofisi ya Taifa ya Takwimu na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Zanzibar kama ilivyoainishwa kwenye kalenda ya machapisho ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012.

Imetolewa na Hajjat Amina Mrisho Said
Kamishna wa Sensa ya Watu na Makazi, 2012
23 Mei, 2014

No comments:

Post a Comment