* Takribani Sh. Tril. 19. 7 kutumika
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Anne Makinda akiwaasa
wabunge wote kushiriki kikamilifu katika kamati zao kizalendo kwa kujali nchi
yao ili ipatikane bajeti yenye tija kwa taifa jana, wakati wa kupokea taarifa
ya Wizara ya fedha jijini Dar es Salaam. (Picha zote na Eleuteri Mangi- MAELEZO)
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Anne Makinda akiwaasa
wabunge wote kushiriki kikamilifu katika kamati zao kizalendo kwa kujali nchi
yao ili ipatikane bajeti yenye tija kwa taifa jana, wakati wa kupokea taarifa
ya Wizara ya fedha jijini Dar es salaam.
Waziri wa Fedha Saada Mkuya Salum akiwasilisha taarifa ya sura ya Bajeti
kuu ya Serikali kwa wabunge jana, jijini Dar es salaam inayotarajia kuanza kutumika kwa mwaka wa fedha
unaoanza Julai 2014/2015.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mizengo Pinda akizungumza na wabunge wakati wa kupokea
taarifa ya Wizara ya fedha jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Fedha Saada Mkuya akiteta jambo na Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji) Dkt. Mary Nagu kabla ya kupokea taarifa ya bajeti ya Wizara ya
fedha jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya Wabunge na wadau wa bajeti wakiwa katika mkutano huo.Baadhi ya Wabunge wakijadili jambo wakati wa mkutano huo, uliofanyika jana katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam.
Na Eleuteri Mangi- MAELEZO
SERIKALI imepanga kutumia jumla ya sh.19, 653.31 ambayo
ndiyo sura ya bajeti katika mwaka wa fedha 2014/2015 kwa ajili ya matumizi ya
kawaida na ya maendeleo ya nchi na watu wake.
Kauli hiyo
imetolewa na Waziri wa Fedha Saada Mkuya Salum alipokuwa akiwasilisha taarifa
ya sura ya Bajeti kuu ya Serikali inayotarajia kuanza kutumika mwaka wa fedha unaoanza
Julai 2014/2015 leo (jana) jijini Dar es salaam.
Waziri Saada alisema kuwa mfumo wa bajeti kwa
mwaka wa fedha unaoanza unazingatia sera za bajeti kwa mwaka 2014/2015 ambazo zitazingatia
vipaumbele vya mpango wa Maendeleo wa Taifa
na malengo ya utekelezaji wa mkakati wa matokeo makubwa sasa (BRN).
Kwa upande
wa matumizi ya kawaida Serikali inatrajia kutumia jumla ya sh.trilioni 14, 208.
21 ambayo inajumuisha mfuko mkuu wa serikali, mishahara ya watumishi wa
Serikali, wizara, mikoa, halmashauri, taasisi na wakala za Serikali.
Aidha, kwa matumizi mengine yatakuwa ni kwa ajili
ya maendeleo kwa mwaka wa fedha unaotarrajiwa kuanza Julai mwaka huu ambapo
kiasi cha 5, 445.10 ambazo ni sawa na asilimia 27.7 zimepangwa kutumika kwa
kuhusisha fedha za ndani na za nje ya nchi.
Waziri Saada akiwasilisha taarifa yake kwa
Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wabunge hao waliipokea
Taarifa ya Serikali kuhusu Makadirio ya Bajeti katika Ukumbi wa Kimataifa wa
Mwalimu Nyerere jijini Dar es salaam ambayo inatarajiwa kuongeza wigo wa
wabunge kuijadili bajeti hiyo kabla ya kusomwa bungeni mjini Dodoma.
Shabaha ya bajeti ya mwaka ujao wa fedha ni
kuhakikisha pato la taifa litakuwa kwa asilimia 7.2 mwaka 2014, asilimia 7.4
mwaka 2015, asilimia 7.7 mwaka 2016 na kuendelea kuongezeka hadi kufikia asilimias
8.0 ifikapo mwaka 2017.
Misingi ya bajeti ya Serikali kwa kipindi cha
mwaka 2014/2015 ni pamoja na kuendelea kuwepo na kuimarishwa amani, usalama,
utulivu na utengamano misingi ambayo itasaidia kupatikana kwa katiba mpya kwa
wakati kama ilivyopangwa.
Kwa upande wake Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais,
Mahusiano na Uratibu Stephen Wasira akiwasilisha rasimu ya mpango wa maendeleo
wa taifa katika bunge likikaa kama kamati alisema kuwa maeneo ya vipaumbele yanalenga miradi ya kitaifa ya
kimkakati inayolenga kutanzua vikwazo vikuu vya kiuchumi inajumuisha
miundombinu ya uasfirishaji kama reli, barabara, bandari, na usafiri wa anga.
Vipaumbele vingine ni nishati, huduma ya maji
mijini na vijijini, kilimo, viwanda, maendeleo ya rasilimali watu na huduma za
kiuchumi kama fedha, biashsra na utalii.
Naye Spika wa Bunge la Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Anne Makinda amewaasa wabunge wote washiriki
kikamilifu katika kamati pamoja na serikali ili ipatikane bajeti yenye tija kwa
taifa na wabunge waikamilishe kizalendo kwa kujali nchi yao.
Kikao cha Bunge la bajeti kinatanguliwa na
kamati mbalimbali zitakutana ambapo vikao vilianza Aprili 27, 2014 kwa wajumbe
kuwasili jijini Dar es salaam na kuhitimishwa Mei 4, 2014 na wabunge kuanza
safari kwenda Dodoma tayari kwa kuanza kikao chake kama ilivyopangwa.
Kamati ya bunge ya Kilimo,
Mifugo na Maji, kamati
ya kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira wakati wa Bunge la bajeti,
kamati ya kudumu ya Bunge ya Miundombinu, kamati ya Nishati na Madini, kamati ya Bunge ya hesabu za Serikali (PAC) kujadili
hesabu zilizokaguliwa za Serikali kuu na mashirika ya umma, kamati ya kudumu
ya Bunge ya Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa.
Na nyingine ni kamati ya kudumu ya Bunge
ya Huduma za Jamii, kamati ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kamati ya kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, kamati ya kudumu ya Bunge ya Uchumi,
Viwanda na Biashara, kamati ya kudumu ya
Bunge ya masuala ya UKIMWI, kamati ya LAAC Dar es salaam na kamati ya kudumu ya
bunge ya maendeleo ya jamii.
No comments:
Post a Comment