TANGAZO


Thursday, April 24, 2014

Kupotoshwa kwa kile walichodai michango yao Bunge Maalum la Katiba, UKAWA watoa tamko

                       
Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba kutoka Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Moses Machari akizungumza na waandishi wa habari, mjini Dodoma leo, kuhusu alichodai kupotoshwa kwa masula kaadhaa juu yao na wale aliowataja wajumbe wa kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), ikiwemo kuzuliwa kuwatukana waasisi wa Muungano, Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amani Karume. (Picha zote na Kassim Mbarouk- www.bayana.blogspot.com)

Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba kutoka Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Moses Machari akizungumza na waandishi wa habari, mjini Dodoma leo, kuhusu alichodai kupotoshwa kwa masula kaadhaa juu yao na wale aliowataja wajumbe wa kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), ikiwemo kuzuliwa kuwatukana waasisi wa Muungano, Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amani Karume.


Ndugu waandishi wa habari,
Leo tarehe 24/04/2014 nalazimika kukutana nanyi kwa lengo la kutoa ufafanuzi juu mambo mbalimbali ya kizushi yanayotolewa ndani na nje ya ukumbi wa Bunge Maalum. Kwa ujumla nitazungumzia mambo yafuatayo:
1.  Tuhuma ya kuchukua Posho na kuondoka
2.  Tuhuma ya Matusi na Ukosoaji wa Viongozi mbalimbali.
3.  UKAWA kutumika na Mataifa ya Nje
4.  Kauli za Vitisho na Uchochezi unaofanywa na wajumbe wa CCM (Kauli za Ndg. Damian Komba na  William Lukuvi).  
Ndugu Wanahabari,
Ni ukweli usiopingika kwamba kumekuwepo na upotoshaji mkubwa sana ndani na nje ya bunge juu ya wajumbe tulioamua kuahirisha kuendelea na vikao vya Bunge maalumu la katiba (Wana UKAWA) baada ya kutoridhishwa na mwnenendo mzima wa vikao vya Bunge hilo. Kwa kuwa sisi wajumbe tuliopewa jukumu la kuhakikisha tunaipatia nchi yetu katiba mpya inayozingatia maslahi mapana ya nchi yetu; na kwa kuwa pamekuwepo na mionendo ya kizushi iliyosheheni propaganda tele miongoni mwa Wajumbe wanaotokana na CCM pamoja na wajumbe wengine ambao kimsingi ni  mawakala  CCM; katika hali hiyo kwa mtu yeyote mwenye akili nzuri na timamu asingeweza kuendelea kujenga hoja yoyote katika mazingira ya fujo kama yale.
Ndugu Wanahabari,
Baadhi ya mambo mabaya ambayo yametendeka katika Bunge Maalum kabla na hata baada ya wajumbe wa UKAWA kuondoka ni pamoja na haya yafuatayo:
Kwanza, ni  upotoshaji wa makusudi unaofanywa na CCM dhidi UKAWA kwamba wajumbe wa UKAWA tumerudi bungeni kuchukua posho.
Ndugu wanahabari,
Jambo hilo si kweli na ninapenda kuwahakikishia Watanzania kwamba hakuna mwana UKAWA hai aliyerejea katika ofisi za bunge kudai posho wala kuchukua posho. Kauli ya upotoshaji kama hiyo ni dalili za CCM na vibaraka wao kukosa hoja za kujibu hoja nzito  za UKAWA  zilizowasilishwa ndani ya Bunge maalumu zilizohusu Muungano wetu.  Itakumbukwa kwamba mara tu baada ya UKAWA kutoka baadhi ya Ma-CCM walisema kwamba UKAWA wamechukua posho za hadi tarehe 30 Aprili na kukimbia, lakini pia ikasemwa tena ndani ya bunge kuwa UKAWA warudishe fedha za Wananchi walizochukua kwa siku ambazo hawako bungeni, sasa unajiuliza nani hapa mkweli mara wamechukua, mara wanakuja kuchukua, hii ni dalili ya kushindwa kuwa na hoja na kuamua kuchafua wajumbe wa UKAWA, ilihali tulichokikataa ni kuwa na mjadala usioendana na rasimu ya katiba iliyotokana na maoni ya wananchi. Maajabu ya maajabu ma-CCM wamekalia mipasho na kutaka UKAWA tukae na watu waliopoteza mwelekeo katika mchakato huu wa kuapata katiba mpya. Jambo hilo haliwezekani hadi watakapojisahihisha na kuheshimu maoni ya wananchi yaliyowasilishwa na Tume ya mabadiliko ya katiba. UKAWA ni watu makini na tusiokurupuka.

Lakini pili ndugu waandishi wa habari, zimekuwepo tuhuma juu ya UKAWA kutumika na mataifa ya nje.
 Ndugu zangu Wanahabri, kusimamia maoni ya wananchi ni jukumu la kila kiongozi wa taifa lolote. Hivyo UKAWA hatutaweza kushawishiwa kamwe na taifa lolote na  hatutaweza kukoma kutetea maoni ya watanzania kwani ndio msingi wa utawala wa kidemokrasia na maoni yaliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya katiba kupitia mwenyekiti wake Jaji Joseph Sinde Warioba. Inaeleweka bayana kuwa ma-CCM na wale  vibaraka wao wanataka kuwafanya UKAWA washindwe kusimamia maoni ya wananchi na badala yake UKAWA tuendelee kujadili mambo mengine. Katika lugha nyingine, wajumbe wa CCM wamedhamiria  kuhamisha ajenda iliyowafanya kuonekana hawana hoja za kupangua hoja za walio wachache ambao wengi wao ni wafuasi wa UKAWA. Aidha tuhuma hizi nzito zilizotolewa na Ndg. PAUL MAKONDA, tunazipuuza kwa kuwa tunaelewa wazi anatafuta umaarufu kwa kupitia kuikashifu UKAWA. Hata hivyo Ndg. PAUL MAKONDA a.k.a mtafuta umaarufu tunampuuza kwa kuwa tunamchukulia kama KIFARANGA cha kuku labda siku moja akijitokeza mama au baba wa kifaranga tutamjibu na kumtaka athibitishe pasipo kuacha shaka kwa kueleza ni nchi gani na namna gani UKAWA inatumika na mataifa ya nje kutaka kuvuruga amani ya nchi yetu. Ninachoweza kusema katika hatua hii, kama kuna Mwana CCM yeyote anayeweza kuthibitisha madai yaliyotolewa na Paul Makonda ajitokeze na kuthibitisha tuhuma hizo pasipo kuacha shaka. UKAWA tuko imara na hatuwezi kuyumbishwa na tuhuma za kipuuzi zisizokuwa na ukweli, tuna akili nzuri na tunajua umuhimu wa nchi kuwa na amani na kamwe hatuwezi kukubali vitendo vya uvunjifu wa amani hapa nchini. Lakini pia sidhani na sitegemei kuona wajumbe wenzangu wa UKAWA wakikaa kimya kwa kuvumila upotoshaji wa aina hii ukifanywa, bali ninashawishika kusema kwamba UKAWA itatumia umakini wake kuhakikisha hatua sahihi zinachukuliwa dhidi ya mtu au kikundi chochote kitakachofanya mambo yasiyokuwa na tija kwa maslahi mapana ya nchi yetu.

Ndugu wanahabari, kumekuwepo na Tuhuma ya kwamba wana Ukawa wanatukana au wanatumia Matusi dhidi ya waasisi wa muungano wetu. Napenda kueleza kwamba, UKAWA ni watu makini na kamwe hatuwezi kuwatukana waasisi wa Muungano wetu lakini mimi kama mwana UKAWA naweza kumkosoa mtu yeyote Yule wakiwemo waasisi wa muungano wetu kwa yale waliyoyafanya na sitakiwi kutafsiriwa kuwa nimetukana kwa kuwa ipo tofauti kubwa sana ya kukosoa na kutukana viongozi au mtu mwingine yeyote Yule. Kwa kuwa ma-CCM ni wapenzi wa propaganda yaani upotoshaji; kamwe sitegemei kuona hata siku moja katika uhai wangu wakikubali Ukweli wa mtu yeyote asiyekuwa mwana CCM kirahisi kabla ya kutokea madhara makubwa. Ninyi na mimi ni mashahidi na tuna recods mbalimbali kuhusu Wabunge na viongozi wa CCM kuukataa ukweli hadi madhara makubwa yajitokeze juu ya jambo Fulani, kwa mfano masula ya OPERESHENI TOKOMEZA nk, walielezwa mapema lakini hawakusikia hadi madhara makubwa yalipoonekana na kupigiwa kelele kwa kiasi kikubwa ndipo wakachukua hatua kwa shinikizo kubwa ilihali watu walishapoteza maisha. Kwa hiyo, kumkosoa mtu yeyote siyo matusi bali ni utamaduni wa kawaida kwa jamii yoyote iliyostaarabika duniani. Hii ni kwa sababu haiwezekani binadamu akaishi na kufanya maamuzi pasipo kukosea na kwa mantiki hiyo ni sharti akosolewe kwa lengo la kujenga na siyo kubomoa.
Hivyo basi kumkosoa hayati Mwl. NYERERE na Rais KARUME haikuwa kosa na wala hawa wazee wetu hawakuwa malaika wala Miungu (Mungu) kiasi kwamba hakuna mahala walipotenda makosa; hilo haliwezekani. Hivyo basi ni vema, CCM waache uvivu wa kufikiri na hivyo kushindwa kutofautisha Matusi na kuwakosoa Waasisi wa Muungano wetu au viongozi wengine walio hai hivi sasa. Mimi binafsi sijasikia na wala sijaona ni wapi Wajumbe wa UKAWA waliwatukana wazee hawa bali walichokifanya baadhi ya wajumbe wa UKAWA ni kukosoa makosa au dosari za muungano zilizosababishwa na hayati Rais Nyerere na Karume ili katika mchakato huu wa Katiba Mpya tuweze kuziepuka kasoro hizo na kuwa na MUUNGANO IMARA ZAIDI.
Hao wanaoendelea kusema kwamba Mhe. TUNDU LISSU na wengine waliwatukana wazee hao ni mwendelezo wa upotoshaji wanaoufanya kwa makusudi baada ya kuishiwa hoja za kutetea msimamo wao wa serikali mbili. TUNDU LISSU na baadhi ya  wana UKAWA  hawakutukana bali walikosoa dosari au mapungufu ya muungano wetu katika kuanzishwa kwake. CCM na washirika wao wa Propaganda wamwogope Mungu na watubu dhambi ya kusema uwongo ili wasihukumiwe. Mbaya zaidi hata viongozi wa dini Mathalani Askofu Mkuu Mstaafu wa Kanisa la Anglican Tanzania DONALD MTETEMELA na Shehe JONGO nao wameingia katika orodha ya watu wanaosema uwongo hadharani pasipo kumwogopa Mungu. Ninasema kwamba Tundu Lissu hajawatukana waasisi wetu bali aliwakosoa na akashauri tuangalie dosari za muungano wetu ziko wapi na tuujenge upya ili kuondoa kero za Muungano kwa pande zote mbili.
KAULI ZA UCHOCHEZI MIONGONI MWA WANA CCM:
Ndugu wanahabari, ninyi na mimi ni mashahidi kwamba pamekuwepo na Kauli za Vitisho na Uchochezi unaofanywa na wajumbe wa CCM.Kwa mfano vitendo vilivyofanywa na Waheshimiwa Wabunge/ Wajumbe WILLIUM V. LUKUVI na Kept. DAMIANO KOMBA vya kutoa kauli za kutufarakanisha wananchi tulio na mapenzi mema na nchi yetu inadhihirisha ni wazi watu hawa na chama chao CCM hawataki amani na utulivu kidogo tulio nao vikaendelea kuwepo. Hii ni kwa sababu kauli zao zinachochea hasira miongoni mwa watu na hatima yake ni kwamba watu wanaweza kuamua kufanya lolote kutokana na uchochezi huo. Na Binafsi ninashangaa sana kwa nini Serikali haijawachukulia hatua hadi sasa. Uongozi wa nchi yetu umekaa kimya kana kwamba kauli walizozitoa ni nzuri kwa nchi yetu, wakati ni kauli mbaya kwa mustakabali wa maisha ya sasa na ya baadaye. Kwa Mfano Mhe. LUKUVI katika hotuba yake wakati wa kumsimika Askofu wa kanisa la Methodist Dodoma alisema maneno yafuatyo:
“…tuwaache Wanzanzibari wajitawale wenyewe na Tanganyika; Wanzanzibari kule walipo 95% ni Waislamu. Tunataka wajitangazie serikali ya kiislamu kule, Mnajua madhara yake? Wale waarabu watarudi; Watazalisha siasa kali kule watakuja kutusumbua. Mimi najua, kabisa. Kwa hiyo ndugu zanguni mnaposikia mjadala kule kuna watu wanajifanya kuwasemea kumbe wana nia nyingine. Zanzibar ni kisiwa na visiwa vinasumbua…”.
Katika DVD yenye kauli hiyo, Mhe. LUKUVI anadhihirisha wazi kana kwamba  Waarabu  si watu au binadamu wema pamoja na Dini ya kiislamu hapa nchini jambo ambalo siyo jema katika kujenga taifa linaloheshimu misingi ya umoja miongoni mwa watu wenye imani tofauti za kidini. Nimejiuliza na bado ninajiuliza maswali mengi: Je, kauli ya Lukuvi ni serikali nzima au ni yake binafsi? Nauliz hivi  kwa kuwa siku hiyo alienda katika kanisa hilo  kama mwakilishi wa Mhe. Waziri Mkuu ambaye ndiye Kiongozi Mkuu wa Shughuli za Serikali. Swali la pili la kujiuliza, kwa kuwa kauli ya Mhe. Lukuvi inaonesha kuwa na chembechembe za kuichukia dini ya kiislamu na waarabu hapa nchini, Je, ni lini Tanzania ikawa nchi ya dini nyingine zilizosalia kama Ukristo; Ubudha; Uhindu nk hadi aoneshe chuki ya wazi dhidi ya Uislamu halafu serikali chini ya Mhe. Rais bado wanamuacha Mhe. Lukuvi? Binafsi ninavyoelewa, ni kwamba nchi yetu na serikali yetu huendeshwa kwa misingi ya kutofungamana na dini yoyote ile bali inatambua na kuheshimu uwepo wa dini mbalimbali na imani za watu wa dini hizo. Mbali na hali hiyo, Tanzania imekuwa ikishirikiana na mataifa mbalimbali duniani ikiwemo mataifa ya waarabu na ya Kiislamu kwa Mfano ABUDHABI; OMANI; ILANI;KUWAIT; LIBYA nk.  Nchi hizo zimekuwa na mchango mkubwa kwa nchi yetu kwani zimekuwa zikitupatia misaada ya kifedha pasipo kujali Tanzania inayo madhehebu mengine ya kidini kama vile Ukristo nk ambapo watu wa madhehebu yote wamenufaika na misaada hiyo ya waarabu na waislamu wa nchi zimezowahi kutusaidia. Ni Vema tukajiuliza Mhe. LULUVI anapata wapi uhalali na jeuri ya kutoa kauli inayoonekana kuwa na mlengo wa kutoipenda dini ya kiIslamu na watu wa jamii ya kiarabu wakati yeye ni kiongozi na maadili ya uongozi yanakataza ubaguzi wa aina yoyote ile katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku?
Mwisho kabisa, mimi na wana UKAWA tumesikitishwa na kauli ya Kepteni Damiano Komba(Mb) ya kwamba ataingia Msituni iwapo serikali mbili hazitaendelea kuwepo hapa nchini. Kauli hiyo ni mwendelezo ule ule wa wa vitisho na kuwafanya Watanzania waishi kwa hofu lakini pia kuwatia hasira wananchi Wenye mawazo tofauti na ule wa CCM wa kuendelea kuwa na mfumo wa Muungano wa serikali mbili. Ni imani yangu kwamba kutishia kwenda Msituni ni kauli mbaya na ya kichochezi kwa kuwa Matendo ya watu walioamua kwenda msituni siyo mazuri hata kidogo. Tujifunze kwa wenzetu wa nchi za DRC; BURUNDI; RWANDA;UGANDA; SUDANI KUSINI nk. Maisha yao yamekuwa ya hofu mno katika nchi hizo.
Ndugu Wanahabri,
Kepteni Komba anataka kutuingiza katika machafuko kwa sababu ya madai ya serikali tatu zilizopendekezwa na wananchi kupitia Tume ya mabadiliko la katiba? Katika, hili ninatamka bayana kwamba Mhe. Komba anapaswa kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwanza na chama chake lakini pia na serikali inayotuongoza ili kuepusha nchi isiingie kwenye machafuko. Kauli za namna hiyo zinachochea hasira miongoni mwa watu. Uzalendo siyo kutoa kauli za namna hiyo bali kutoa kauli zenye kuleta matumaini. Kwa kuwa chama chake CCM kimefumba macho kwa kutokemea kauli hizo ni wazi siyo makosa kwa mtu kutafsiri kwamba kauli za Akina Lukuvi na Kept. Komba ndiyo msimamo wa CCM na kwa mantiki hiyo, inatubidi watanzania tusiyo wana CCM tutafakari hatua sahihi za kuchkua dhidi ya mtu yeyote yule mwenye kutetea  maslahi mapana ya nchi yetu. Ni wazi CCM wanataka kuiingiza nchi yetu kwenye machafuko kupitia kauli zinazotolewa na viongozi hao. Je, na sisi UKAWA tuseme kwamba tutaingia msituni? P
Ndugu waandishi wa Watanzania wote, sisi UKAWA ni watu tunaoheshimu utaratibu uliowekwa na katiba, sheria na kanuni mbalimbali za nchi yetu. Tunawataka CCM kueleza ni kwa nini watu wake wanatoa kauli za uchochezi hadharani? Ninawaeleza kwamba wasidhani kwamba UKAWA tunatishika na kauli za namna hiyo, tuko imara na tutaendelea kudai katiba mpya kwa hoja na ikitokea vinginevyo tutakabiliana na chama au mtu yeyote Yule kwa namna yoyote na kwa gharama yoyote ili kuhakikisha hakuna dhulma na unyanyasaji wowote. Tunawataka CCM na watu wake  kuheshimu utaratibu unaotumika katika kuendesha nchi yetu, na daima waelewe kwamba UKAWA siyo wajinga.
 Ndugu, wanahabari, kupitia kwenu nina amini kwamba ujumbe huu utawafikia wana CCM na hivyo kuwa chachu ya kuwafanya watafakari upya kauli zao. Niwatoe hofu wananchi wote kwa kusema kwamba UKAWA hatutarajii kuona uvunjaji wa taratibu za nchi yetu bali tunatarjia kuona kila mtu au kikundi chochote kile kikiheshimu sheria zilizopo ili kuiepusha nchi yetu kuingia kwenye matatizo. Ni aibu watu wazima wamekalia propaganda badala ya kujadili rasimu kama dhamira yao ni njema. UKAWA hatukutoka nje kwa kupenda, na wala baada ya kutoka hatukwenda “picnic” bali tulitoka kwa sababu ya tabia chafu ya Wajumbe wa CCM na mawakala wao ya kutoa  kauli za mipasho na kejeli badala ya kujadili Rasimu ya Katiba iliyokuwa mezani. Waingereza wanasema “ Don’t argue with a fool because others may not see the difference” Katika mazingira kama yale UKAWA tungeendelea kubishana na watu wenye shingo ngumu kama wale wote tungeonekana kuwa na matatizo ya kufikiri jambo ambalo sisi UKAWA hatukubali kubeba ujinga wa wengine.
Hata baada ya sisi wana UKAWA kuondoka kinachoendelea Bungeni hivi sasa, ni upotezaji wa muda na fedha za walipa kodi masikini wa Tanzania.  Sisi wana UKAWA kwa kutambua umuhimu wa Katiba laikini pia kwa kutambua kuwa wananchi wetu bado ni masikini hatukupenda kutumia fedha ya umma bure. Hivyo tuliacha posho na tukaamua kwenda kwenda kwa wananchi kuwaeleza uozo unaoendelea bungeni ili hatimaye tuweze kupata ushauri wa wananchi  juu ya nini kifanyike. CCM wanatubeza, lakini niseme tu katiba yoyote ile inatakiwa kupatikana kwa maridhiano.
Nawashkuru sana na asanteni kwa kunisikiliza
……………………….
Moses Joseph Machali (mb)
MBUNGE WA KASULU MJINI NA MJUMBE WA BUNGE MAALUM

24/04/2014

No comments:

Post a Comment