Mtendaji Mkuu Bodi ya
Filamu Bi. Joyce Fisoo akiwasilisha Rasimu ya awali ya Sera ya Filamu wakati wa
moja ya kikao cha wadau cha kujadili rasimu ya awali ya Sera ya Filamu
kilichofanyika hivi karibuni, jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi msaidizi kutoka Idara ya Sera
na Mipango Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bi. Verediana Mushi na Kushoto ni mdau wa filamu Bw. John Kitime.
Wadau mbalimbali wa
tasnia ya filamu wakijadiliana wakati wa kikao cha wadau cha kujadili rasimu ya
awali ya Sera ya Filamu kilichofanyika hivi karibuni. (Picha
na Genofeva Matemu)
Na Genofeva
Matemu – Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WHVUM SERIKALI
ya Tanzania imejipanga kuendeleza kwa dhati TASNIA ya Filamu ili kuwa chanzo
kikubwa cha ajira kwa wasanii na pia kuongeza uchumi wa nchi.
Ni
dhahiri kuwa sekta ya filamu ni njia madhubuti ya kutambulisha jamii kiutamaduni,
kisiasa na kijamii na pia katika kukuza
na kuongeza fursa za nchi katika uwekezaji na utalii.
Filamu
na Makala za Filamu zikitumika vizuri zitaweza kuhamisha na kuondoa
tofauti mbalimbali zilizopo ndani ya
jamii na hivyo kuongeza umoja na mshikamano baina ya watu wa makabila na watu
wenye asili mbalimbali, hivyo kuutambulisha utamaduni wa Mtanzania.
Kazi na shughuli za Filamu nchini zimekuwa zikisimamiwa
na Sera ya Utamaduni ambayo ilitayarishwa na kupitishwa mwaka 1997 pamoja na Sheria ya Filamu na Michezo ya Kuigiza na 4 ya
mwaka 1976.
Katika kipindi cha kuanzia mwaka 1997 hadi mwaka 2013
kumekuwepo na maendeleo makubwa katika
Tasnia ya Filamu nchini hivyo kuisababishia Sera ya Utamaduni ya Mwaka 1997 kutokidhi
baadhi ya mahitaji ya tasnia ya filamu na
kupelekea mahitaji ya kurekebisha Sera ya Utamaduni kama Sera mama na kutungwa
kwa Sera ya Filamu.
Mnamo
Desemba 12 mwaka 2013, wadau mbalimbali kutoka Wizara ya Habari,Vijana
Utamaduni na Michezo, Bodi ya Filamu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Wizara ya Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi walishiriki katika kikao cha wadau cha kujadili rasimu ya awali
ya Sera ya Filamu.
Wadau wengine ni Wizara ya Afya na Ustawi wa
Jamii, Wizara ya Kazi na Ajira, BASATA, Idara ya Sanaa na Sanaa za Maonyesho,
Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam, Mamlaka ya Mapato Tanzania, Mtandao wa Muziki,
Swahili Films, ROSAF, TAPAF, Umoja wa
Mashirikiano wa Filamu, Filamu Cental,
Chama cha Hakimiliki Tanzania, Shirikisho la Sanaa za Maonyesho pamoja na
G&S Associates and Advocates.
Hata hivyo wadau ambao hawakushiriki walipewa
nafasi na Serikali kuwasilisha maoni yao ambapo mwitiko umekuwa mzuri na maoni
yanaendelea kupokelewa ili hatimaye kuwa na Sera bora na shirikishi.
Katika kikao hicho Rasimu ya awali ya Sera ya Filamu
iliwasilishwa kwa kuelezea historia fupi ya filamu nchini, vikao vya wadau vilivyofanyika
vya mapendekezo ya kuwa na Sera ya Filamu kati ya mwaka 2004 na 2013, nyaraka
kama Mpango Mkakati wa Bodi ya Filamu unaoonyesha haja ya kuwa na Sera ya
filamu pamoja na kuelezea malengo mahususi na matamko ya Sera mpya inayopendekezwa
kutungwa.
Aidha, wadau walijadili uzoefu wa nchi nyingine kama
Kenya, Nigeria, China, Afrika Kusini, Marekani, Canada, India na Uingereza na
matokeo ya tafiti mbalimbali zilizofanyika pamoja na Changamoto zinazoikabili
Tasnia ya Filamu nchini.
Miongoni mwa mapendekezo yaliyotolewa
na wadau ni pamoja na kuwa Sera itamke uanzishwaji wa Chuo cha Taifa cha Filamu, Sera itamke kuwepo
kwa Mfuko ambao utasaidia katika kuimarisha Sekta ya Filamu na Sanaa za
maonyesho kwa ujumla, Sera itoe tamko kuhusu kusimamia maadili katika tasnia ya Filamu na kudhibiti ukatili wa kijinsia
katika tasnia ya Filamu.
Pia walipendekeza kuwa hoja na matamko
yawe na takwimu zaidi, Sera itamke namna ya kumlinda msanii wa Tanzania,
mzalishaji wa ndani na wawekezaji, pamoja na kupiga vita udhalilishaji wa watoto
wa kike.
Kwa upande mwingine, wadau hao walitoa
pongezi kwa Wizara kwa kuandaa Rasimu ya awali ya Sera ya Filamu iliyotokana na
maoni mbalimbali ya wadau, Sera ambayo itaiwezesha Tasnia ya Filamu kupata
mwelekeo bayana na kukidhi matakwa ya kila mdau katika tasnia ya filamu.
Wizara
inapenda kuujulisha umma kuwa imekua na inaendelea kushirikiana na wadau wa
Filamu kwa kila hatua ili hatimaye ifanikishe azma ya kuwa na nyaraka zote
muhimu katika kuendeleza, kusimamia, kuratibu na kukuza tasnia ya filamu nchini.
No comments:
Post a Comment