Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mh. Janet Mbene (katikati) akiwa ameongozana na Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam Prof. Emanuel Mjema (kulia) mara baada ya kukitembelea chuo hicho jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mh. Janet Mbene akiongea na viongozi wa Chuo cha elimu ya Biashara mara baada ya kutembelea maeneo mbalimbali ya chuo hicho jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mh. Janet Mbene akiwa ameambatana na viongozi wa Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam (CBE) akiangalia vifaa vya kisasa vya kujifunzia wanafunzi katika chuo wakati wa ziara yake jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam Profesa Emanuel Mjema (mwenye suti nyeusi), akimwonesha Naibu Waziri
wa Viwanda na Biashara Janet Mbene maeneo ya chuo hicho,
yaliyovamiwa ambayo sasa yamejengwa majengo ya biashara.
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mh. Janet Mbene akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Chuo cha elimu ya Biashara mara baada ya kuhitimisha ziara yake katika chuo hicho,
jijini Dar es Salaam.
Na Aron Msigwa –
MAELEZO.
14/2/2014.Dar es
salaam.
SERIKALI imesema kuwa Chuo
cha Elimu ya Biashara (CBE) kampasi ya
Dar es salaam licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali kimeendelea kufanya
vizuri katika nyanja ya elimu kwa kuboresha mafunzo yanayotolewa chuoni hapo, kupanua
miundombinu na kuweka mifumo ya kisasa ya kufuatilia vitendo vya ukiukaji wa
maadili na udanganyifu unaofanywa na wanafunzi wakati wa mitihani.
Kauli hiyo imetolewa leo na Naibu Waziri wa
Viwanda na Biashara Mh.Janet Mbene wakati akizungumza na uongozi wa chuo hicho mara
baada ya kutembelea maeneo mbalimbali ya chuo hicho leo jijini Dar es salaam.
Amesema chuo hicho kwa
muda mrefu kimekuwa mstari wa mbele katika kutoa vijana wenye ujuzi ambao
wamekuwa msaada kwa jamii na taifa zima na kuongeza kuwa serikali itaendelea
kuunga mkono juhudi zinazofanyika chuoni hapo kwa kukijengea uwezo kifedha
kadri bajeti ya serikali itakavyoruhusu.
“Chuo hiki tunakiamini,
kikubwa muendelee kuhakikisha mnapokea wanafunzi wenye vigezo ili wanapohitimu
waweze kufanya vizuri na wawe mfano, serikali inaendelea kufanya kila
linalowezekana kuhakikisha chuo hiki kinafanikiwa” amesisitiza.
Mh. Mbene amepongeza
hatua mbalimbali zilizochukuliwa na uongozi wa chuo hicho katika kuhakikisha
suala na nidhamu na maadili kwa wanafunzi linadumishwa na kuongeza kuwa huo ni
mfano wa kuigwa kwa vyuo vingine hapa nchini katika kujenga taifa lenye vijana
wenye maadili.
Ametoa wito kwa wakufunzi wa chuo hicho kutimiza wajibu wao
kwa kusimamia elimu na haki na kuwataka kuepuka vitendo vinavyoweza
kuwadhalilisha wanafunzi na kuharibu taswira ya chuo hicho.
“Ninapenda kuona mnasimamia
viwango vya elimu na maadili na kukomesha tabia na vitendo vyote vinavyoweza
kuharibu taswira nzuri ya chuo” amesema.
Akizungumzia changamoto
mbalimbali zinazokikabili chuo hicho ikiwemo uhaba wa fedha za maendeleo,
ufinyu wa eneo kutokana na kuwepo kwa baadhi ya watu waliovamia na kujenga
katika eneo la chuo na ukosefu wa wakufunzi wa kutosha Mh. Mbene ameeleza kuwa
serikali imezipokea changamoto hizo na itazifanyia kazi ili chuo hicho
kiendelee kutoa elimu bora.
Kwa upande wake Mkuu wa
Chuo hicho Prof.Emanuel Mjema amesema kuwa uongozi wake unaendelea kuchukua
hatua mbalimbali za kuboresha hali ya elimu ya chuo na kuweka msisitizo katika
kulinda na kudumisha maadili kwa wanafunzi wote wanaoingia na kutoka chuoni
hapo.
Amesema suala la elimu
sasa limepewa kipaumbele ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wanaohitimu wanakuwa
bora na wanakidhi viwango kitaifa na kimataifa na kuongeza kuwa chuo kwa sasa
kimefanikiwa kudhibiti kabisa vitendo vya udanganyifu vilivyokuwa vikifanywa na
wanafunzi wakati wa mitihani.
“Tangu nimeingia
madarakani mwezi Januari 2013 nimefanikiwa kubadilisha utaratibu wa mfumo wa
utungaji wa mitihani, mfumo huu haumpi mwanafunzi fursa ya aina yoyote ya
kuweza kuibia wakati wa mitihani wala kushirikiana na mwanafunzi, sasa
mwanafunzi analazimika kusoma kwa bidii na kila mtu anatimiza majukumu yake ”
amesisitiza.
Ameongeza kuwa katika
kuhakikisha chuo hicho kinaimarisha maadili kwa wanafunzi na wakufunzi hasa
madarasani na wakati wa mitihani tayari kamera 20 za kisasa zimekwifungwa
kwenye vyumba vya madarasa 20 na matukio yote hurekodiwa na kuwa ushahidi pale
yanapotokea madai ya udanganyifu au kuonewa wakati wa mitihani.
“ Kwa sasa hatuna utani
na suala la elimu maana wapo waliokumbwa na adhabu mbalimbali kufuatia kuwepo
kwa vifaa hivi ambavyo vimetoa ushahidi mzuri na tayari mwalimu mmoja
amekwishafukuzwa kazi kwa kukosa nidhamu na toka 2013 hadi sasa hali iko shwari
kabisa” amebainisha Prof. Mjema.
Naye Rais wa serikali
ya wanafunzi wa chuo hicho (COBESO) Bw. Benedict Masasi akizungumza wakati wa
ziara hiyo amesema kuwa kwa sasa hali ya chuo na masomo inakwenda vizuri, wao
kama serikali ya wanafunzi hawana malalamiko kutoka kwa wanafunzi kutokana na
uelewa uliojengeka miongoni mwa wanafunzi na kuongeza kuwa wao kama serikali ya
wanafunzi wanafanya kazi bega kwa began a uongozi wa chuo. (Picha zote na Aron Msigwa - MAELEZO)






No comments:
Post a Comment