Takriban watu 26 waliuawa Jumanne katika mapigano kati ya
wanajeshi wa serikali na waasi katika mji wa Lubumbashi nchini DRC.
Wanajeshi walipambana na waasi hao Jumanne asubuhi baada ya makabiliano
makali yaliyoendelea usiku kucha.Mashambulizi yalianzishwa na kundi la waasi wa Mai Mai Kata Katanga, kundi linalotaka Lubumbashi kujitawala.
Waasi hao wanasema kuwa wanapigania uhuru wa mkoa huo ulio na utajiri mkubwa zaidi nchini Congo.
Aidha kundi lenyewe linaongozwa na Gedeon Kyungu Mutanga, aliyeachiliwa wakati waasi hao walipovamia gereza la Lubumbashi na kuwaachilia huru wafungwa.
Mkoa wa Lubumbashi una kiwango kikubwa zaidi cha madini ya Cobalt duniani na pia huzalisha madini ya Copper kwa wingi.
Mkuu wa polisi wa Lubumbashi aliambia BBC kuwa watu 26 walifariki wakiwemo wanajeshi na waasi.
Wafanyabiashara walifunga biashara zao huku maelfu wakisalia majumbani kwao siku ya Jumanne.
Wanajeshi wa serikali hata hivyo walishika doria baada ya kuwashinda waasi nguvu na kuwasukuma nje zaidi ya mji huo.
Mwezi Machi mwaka jana watu 5 waliuawa wakati washukiwa wa kundi la Mai Mai walipouvamia mji wa Lubumbashi.
No comments:
Post a Comment