Jeshi la Sudan Kusini limesema waasi wa Sudan Kusini wameutwaa
mji muhimu, wa Bor uliopo kilomita 200 kaskazini mwa Juba, wakati mapigano
yakiendelea baada ya kuripotiwa kwa jaribio la kupindua serikali Jumapili.
"askari wetu wamepoteza udhibiti kwa wapiganaji wa Riek Machar," amesema
msemaji wa jeshi Philip Aguer.Hali hiyo ya mapigano yaliyoanza katika mji mkuu Juba, tayari yamesababisha watu 500 kuuawa na kuleta wasiwasi wa kutokea kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Umoja wa Mataifa umetaka mgogoro huo umalizwe kwa njia ya mazungumzo ya kisiasa, na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema watu wapatao 20,000 wamepata hifadhi katika viwanja vya Umoja wa Mataifa mjini Juba.
Uingereza na Marekani zimetuma ndege zao kuwaondoa raia wao kutoka Sudan Kusini, na afisa mmoja wa wizara ya ulinzi wa Marekani ameelezea hali hiyo ya mapigano kuwa inaelekea kuwa mbaya.
Tangu uhuru, makundi kadha yamekuwa yakipigana dhidi ya serikali ya Sudan Kusini. Haijabainika iwapo mojawapo ya makundi haya yamehusika katika kuuteka mji wa Bor.
Siku ya Jumatano, meya wa mji wa Bor, Nicholas Nhial Majak, aliiambia BBC kuwa ghasia hizo zimesambaa hadi mji wa Bor, kilomita mia mbili kutoka Juba.
No comments:
Post a Comment