TANGAZO


Saturday, December 28, 2013

Dk. Shein awa mgeni rasmi mahafali ya 9 ya SUZA

.Asema Mafunzo Vyuo Vikuu lazima yalenge kutoa mchango katika utekelezaji wa mpango wa Taifa

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa SUZA, akisalimiana na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Ali Juma Shamuhuna, wakati alipowasili Chuo Kikuu cha Taifa, Kampasi ya Tunguu, katika sherehe za mahfali ya 9 ya chuo hicho, ambayo wahitimu wa fani mbalimbali wamepatiwa Shahada, Stashahada na Vyeti. (Picha zote na Ramadhan Othman,Ikulu)
 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti waa Baraza la Mapinduzi,
Dk. Ali Mohamed Shein, ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa SUZA, akisalimiana na walimu wa Chuo Kikuu cha SUZA, alipowasili katika mahfali ya 9 ya chuo hicho, yaliyofanyika katika Kampasi ya chuo, Tunguu, Wilaya ya Kati Unguja leo.

Baadhi ya wahitimu wa fani mbalimbali  wa Chuo Kikuu cha Taifa SUZA, wakiwa katikaa maandamano wakati wa sherehe za mahafali ya 9 chuo hicho, yaliyofanyika katika Kampasi ya Tunguu, Wilaya ya Kati Unguja leo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa SUZA (wa pili kulia), akiongoza maandamano wakati wa sherehe za mahafali ya 9 ya chuo hicho, yaliyofanyika katika Kampasi ya Tunguu,Wilaya ya Kati Unguja leo, yakiwashirikisha baadhi ya wahitimu na walimu.
Wahitimu wa Stashahada ya Teknolojia ya Habari, waliotunukiwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti waa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa SUZA (hayupo pichani), katika mahafali ya 9, yaliyofanyika Kamapasi ya Tunguu leo. Kutoka kushoto ni Stewat Njelekela, Seif Mohamed Nassor na Husna Shaabani Bwamadi.
Baadhi ya wahitimu wa Shahada ya Sayansi na Elimu ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), wakiwa katika mahafali yao hayo, baada ya kutunukiwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa (SUZA), katika mahafali ya 9 iliyofanyika katika Kampasi ya Tunguu leo. 
Baadhi ya wahitimu wa Shahada ya Sayansi ya Kompyuta ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), wakisimama kwa ajili ya kutunukiwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa (SUZA), katika mahafali ya 9 yaliyofanyika katika Kamapasi ya Tunguu leo.

 
Na Said Ameir
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameutaka uongozi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar –SUZA kuhakikisha kuwa upanuzi wa mitaala, ufundishaji na tafiti zinazofanywa na chuo hicho zinaelekezwa katika kutoa michango na rai zitakazochangia na kurahisisha utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya nchi.
Akizungumza wakati wa mahafali ya Tisa ya Chuo Kikuu hicho yaliyofanyika leo huko Tunguu, mara baada ya kuwatunuku vyeti, stashahada na shahada wahitimu 763 Dk. Shein amesema ni jukumu la vyuo vikuu hasa vya Serikali kutoa taaluma inayolenga kurahisisha utekelezaji wa mipango ya maendeleo Taifa na jamii kwa ujumla.
Kwa hiyo amebainisha kuwa zitihada zinazofanywa na chuo za kukuza elimu zitakuwa na manufaa zaidi endapo elimu itakayotolewa italiongoza Taifa na itatumika kurahisisha maisha na kuimarisha maendeleo kwa kusaidia utekelezaji wa Dira ya Maendeleo 2020, MKUZA II, Malengo ya Milenia na Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
Dk. Shein aliwaeleza wahitimu, jumuiya ya wanachuo na wageni waliohudhuria mahafali hayo kuwa Serikali inaziunga mkono jitihada zinazofanywa na chuo hicho za kuongeza mafunzo ya nyanja mbalimbali kwa kuwa inaamini kuwa maendeleo ya nchi yanategemea nguvukazi yenye elimu ya kutosha.
Kwa hiyo alisisitiza kuwa Serikali ina kila sababu ya kuimarisha maslahi ya watumishi wa SUZA kila hali ya uchumi itakaporuhusu na kuongeza kuwa azma ni kuhakikisha kuwa maslahi yanakuwa mazuri hadi kuwavutia wale walioko nje kurudi chuoni hapo.
Hata hivyo Mheshimiwa Rais alihimiza watumishi wa chuo kufanyakazi kwa bidii na kujituma bila kusubiri kuhimizwa kwani kuendelea na mtindo wa kufanya kazi kwa mazoea hakulisaidii Taifa wala watumishi wenyewe kwa kuwa nchi inazidi kubaki nyuma hivyo kushindwa kuboresha hata maslahi yao mwenyewe.
Dk. Shein alieleza kuwa ameridhika na jitihada za chuo hicho za kuzidi kuongeza nyanja za masomo ambapo katika kipindi kifupi chuo hicho kimeweza kuongeza programu mpya tisa zikiwemo mbili za shahada za uzamili, fani tano za kiwango cha shahada na mbili za kiwango cha stashahada.
Alikipongeza chuo kwa kuanzisha mafunzo ya shughuli za ujasiriamali na ubunifu hatua ambayo aliieleza kuwa itasaidia sana jitihada za Serikali za kuwawezesha wananchi kiuchumi.
Kwa hiyo amewataka wahitimu wa vyuo vikuu nchini kubeba dhana ya ujasiriamali kama wanavyofanya vijana wenzao wasomi wa nchi nyingine ulimwenguni zikiwemo China na Marekani na kuachana na dhana ya kuona shughuili za ujasiriamali ni kazi za mikono tu na ni kwa ajili ya watu waliokosa elimu ya juu.  
Akizungumza katika mahafali hayo Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Mheshimiwa Said Bakari Jecha aliishukuru Serikali kwa kukiunga mkono chuo hicho kwa hali na mali katika jitihada zake za kukikiimarisha ikiwemo kuanzisha skuli mbalimbali chuoni hapo.
Mwenyekiti huyo hata hivyo aliiomba Serikali kuangalia upya maslahi ya watumishi wa chuo hicho ambayo aliyaeleza kuwa ni madogo yakilinganishwa na maslahi katika vyuo vikuu vingine hali ambayo inakifanya chuo hicho kisiweze kushindana katika soko la ajira.
Wakati huo huo Makamu Mkuu wa SUZA Profesa Idris Ahmada Rai amesema kuwa katika kuimarisha uwezo, chuo kimeweza kufanikiwa kupata rasilimali mbalimbali kupitia utaratibu wa ushindani kwa wanataaluma wa chuo hicho kupeleka miradi na tafiti zao.
Akizungumza katika mahafali hayo Profesa Rai alibainisha kuwa chuo kimeweza kushinda miradi miwili inafadhiliwa na Seriklai ya Norway yenye thamani shilingi bilioni 3.3, Denmark inafadhili mradi mmoja wenye thamani ya shilingi bilioni 2.2, COSTECH mradi mmoja wenye ya shilingi milioni 90, Shirika la Umoja Maendeleo la Umoja wa Mataifa- UNDP mradi mmoja wenye thamani ya shilingi milioni 44.3 na Uturuki inafadhili mradi wa shilingi milioni 80.  
Profesa Rais alieleza pia kuwa chuo hicho kimefanya mabadiliko ya Muundo wake, Dira na Dhamira pamoja na mambo mengine.
Kwa hiyo alibainisha mabadiliko hayo kuwa ni kuweka maadlili makuu ya chuo ambayo yataongoza utendaji wa chuo kwa lengo la kufikia Dira na Dhamira za Chuo.
Aliyataja maadili makuu hayo kuwa ni pamoja na Kukubali mabadiliko na kuyapeleka mbele, Kufanyakazi kwa vitendo, Kufanyakazi kwa pamoja, Uwazi na ukweli, Uhuru wa fikra/mawazo na kujieleza, Kuzingatia wakati na ubora, Nia njema na Uzalendo.
Mahafali hayo yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali walikwemo mawaziri na makatibu wa Wakuu. Miongoni mwa mawaziri wakuohudhuria ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mheshimiwa Ali Juma Shamuhuna.

No comments:

Post a Comment