Ofisa Lishe Mwandamizi wa Taasisi ya Chakula na Lishe, Maria Msangi, akieleza kwa waandishi wa habari (hawapo pichani), kuhusu
utekelezaji wa mpango wa uongezaji wa virutubisho kwenye vyakula ili kusaidia
kuondoa magonjwa yanayosababishwa na upungufu wa lishe, wakati wa mkutano
uliofanyika, ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Dar es Salaam leo. Kushoto ni Kaimu
Mkurugenzi Idara ya Sayansi wa Taasisi hiyo, Dk. Elifatio Towo. (Picha na Hassan
Silayo-MAELEZO)
Na Georgina
Misama-MAELEZO
Taasisi ya Chaula na Lishe yaiasa jamii kuzingatia lishe bora
kuanzia kipindi cha ujauzito hadi mtoto
anapofikisha miaka miwili.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi Idara ya Sayansi ya
Chakula na Lishe (TFNC) Dkt Elifatio Towo wakati wa mkutano na waandishi wa
habari leo jijini Dar es Salaam.
Dkt Towo alisema kuwa
uzingatiaji wa lishe bora utachangia katika kutokomeza utapiamlo na kuimarisha
afya ya mtoto tangu akiwa tumboni kwa mama na kudumu kwa maisha yake yote.
“Watoto waliopata
lishe ya kutosha na hasa katika kipindicha siku 1000 za mwanzo tangu mama
anapokuwa mjamzito mpaka mtoto anapofikisha miaka 2 wanakuwa wamepata faida
zitakazodumu katika maisha yao yote” alisema Dkt Towo.
Aidha aliongeza kuwa uongezaji wa Vitamini na Madini kwenye vyakula ni muhimu katika utendaji kazi
wa mwili kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 5 na wanawake walio katika umri wa kubeba mimba.
Alifafanua kuwa tafiti
zinaonesha kuwa asilimia 59 ya watoto
chini ya umri wa miaka 5, na asilimia 41 ya kina mama wana upungufu wa madini
chuma yanayopelekea kushusha kiwango cha utengenezaji damu.
Akieleza namna ya
kukabiliana na tatizo hilo, Dkt Towo alisema kuwa, Taasisi imeanzisha teknolojia ya uongezaji wa vitamin na madini
katika vyakula vikuu kama vile unga wa ngano, sukarik mafuta ya kula, na unga
wa mahindi.
Akijibu swali la mwandishi alietaka ujua licha ya kuwepo kwa
vyakula mbalimbali kwanini baadhi ya watoto wanaandamwa na magojwa, Afisa
Mwandamizi wa Sayansi ya Lishe Maria Msangi alisema kwamba lishe duni
inasababisha kinga hafifu na kupelekea
jamii yenye kuandamwa na magonjwa hasa ya kuambukizwa.
Uzinduzi wa Mpango kuongeza virutubishi kwenye vyakula ulifanywa na Mheshimiwa Rais
wa Jamuhuri ya Tanzania Dkt Jakaya Mrisho Kikwete na tayari vyakula hivyo
vinapatikana kwenye maduka na sokoni vikiwa na nembo maalum inayoonyesha
vyakula hivyo vimeongezwa virutubisho.
No comments:
Post a Comment