![]() |
Mhe. Tundu Lisu |
KUHUSU
MUSWADA WA SHERIA YA MAREKEBISHO YA
SHERIA
YA MABADILIKO YA KATIBA (NA. 2), YA MWAKA
2013
(Kanuni ya
86(6) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, 2013)
UTANGULIZI
Mheshimiwa
Spika,
Tumerudi
kwa mara nyingine tena kutafakari mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83
ya Sheria za Tanzania. Hii ni mara ya tatu kwa Bunge lako tukufu kufanya
hivyo kuhusiana na Sheria hii hii. Kama itakavyokumbukwa, marekebisho ya kwanza
yalifanyika mwezi Februari ya mwaka jana, wakati marekebisho ya pili
yalifanyika aghalabu mwezi mmoja na nusu uliopita.
Mara
hii, kama ililvyokuwa kwa Sheria mama wakati wa Mkutano wa Tatu wa Bunge hili
tukufu mwezi Aprili, 2011, Muswada wa Sheria ya Marekebisho umeletwa kwenye
Bunge lako tukufu kwa Hati ya Dharura ya Mheshimiwa Rais ya tarehe 28 Oktoba,
2013. Muswada huu ulichapishwa kwenye Gazeti
la Serikali la siku tatu kabla, yaani tarehe 25 Oktoba, 2013. Hii ina maana
kwamba, kwa mujibu wa kanuni ya 93(3) ya Kanuni za Kudumu na kwa mujibu wa ratiba
mpya ya Mkutano huu wa Bunge lako tukufu, Muswada huu unatakiwa ujadiliwe na
kupitishwa leo hii hii.
Mheshimiwa
Spika,
Kama
tulivyosema wakati wa kujadili Muswada wa Sheria ya Uendeshaji Mahakama wakati
wa Mkutano wa Tatu wa Bunge lako tukufu, matumizi ya Hati ya Dharura katika
utungaji wa sheria yana madhara makubwa na ya wazi kwa demokrasia yetu: “... [S]heria zinazotungwa haraka haraka
namna hiyo zinakosa uhalali wa kisiasa kwa sababu ya kukosa ushiriki wa Wabunge
na wadau wengine. Vile vile, sheria hizo zinakuwa na makosa mengi kwa sababu ya
kukosekana umakini katika kuzitunga na utekelezaji wake kisiasa na kisheria
unakuwa mgumu. Aidha, sheria za aina hiyo zinafisha demokrasia na uwajibikaji
wa Serikali kwa Bunge na kwa wananchi kwa sababu jukumu la kikatiba la Bunge
kama baraza la kutunga sheria na la kusimamia serikali linageuzwa kuwa ni la
kupiga muhuri maamuzi na mapendekezo yanayoletwa na Serikali. Mwishowe, Bunge
la aina hiyo linakosa hadhi na heshima kwa wananchi na hivyo kukaribisha aina
nyingine za siasa za nje ya Bunge.” Historia ya miaka miwili ya Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba inathibitisha ukweli wa kauli hii.
Mheshimiwa
Spika,
Kama
ilivyokuwa kwa marekebisho ya kwanza ya Sheria hii, Muswada huu umekuja
kufuatia Rais Jakaya Kikwete
kuingilia kati kufuatia mtafaruku uliotokea wakati wa, na baada ya, kupitishwa
kwa marekebisho ya pili ya Sheria hii wakati wa Mkutano uliopita wa Bunge lako
tukufu. Mara hii Mheshimiwa Rais aliwaita viongozi wakuu wa vyama vya siasa
vyenye uwakilishi Bungeni kwenye majadiliano yaliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam,
tarehe 15 Oktoba, 2013. Baadaye, kwa maelekezo ya Mheshimiwa Rais, viongozi
wakuu wa vyama hivyo walikutana chini ya uratibu wa Kituo cha Demokrasia
Tanzania (TCD) mnamo tarehe 17 na 20 Oktoba, 2013, ili kukubaliana juu ya
maeneo ya Sheria hii yanayohitaji kurekebishwa kwa ajili ya kuyawasilisha
serikalini. Muswada huu ni matokeo ya mchakato huo.
Mheshimiwa
Spika,
Muswada
huu unapendekeza marekebisho katika vifungu vitatu vya Sheria na Sehemu ya VI
ambayo vifungu vyake vikuu vitafutwa na kutungwa upya katika Sheria ya Kura ya
Maoni, ambayo Muswada wake unaanza kujadiliwa leo hii hii. Maeneo
yanayopendekezwa kurekebishwa yanahusu idadi ya wajumbe wa Bunge Maalum
wasiotokana na Wabunge, mamlaka na utaratibu wa uteuzi wao; mamlaka ya Makatibu
wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na Baraza la Wawakilishi kufanya maandalizi kwa
ajili ya utekelezaji bora wa shughuli za Bunge Maalum na utaratibu wa kufanya
maamuzi juu ya Rasimu ya Katiba katika Bunge hilo. Eneo la mwisho
linalopendekezwa kurekebishwa ni utaratibu wa uhalalishaji wa Katiba Mpya
katika Sehemu ya VI ya Sheria.
1.
IDADI YA WAJUMBE WA
BUNGE MAALUM
Mheshimiwa
Spika,
Muswada
unapendekeza kuongeza idadi ya wajumbe wa Bunge Maalum wasiotokana na Wabunge
na Wawakilishi kutoka mia moja sitini na sita walioko kwa mujibu wa kifungu cha
22(1)(c) cha Sheria ya sasa hadi kufikia wajumbe mia mbili na moja. Hili ni
ongezeko la wajumbe thelathini na tano na litafanya idadi ya wajumbe wote wa
Bunge Maalum kufikia mia sita thelathini na tisa. Kama ilivyokuwa tangu Sheria
hii ilipotungwa mwaka 2011, wajumbe hawa watateuliwa na Rais kwa makubaliano na
Rais wa Zanzibar.
Licha
ya mabadiliko ya idadi yao, kuna mapendekezo mengine ya marekebisho yanayohusu wajumbe
wa Bunge Maalum. Wakati Sheria ilitamka tu kwamba wajumbe hao watatokana na
makundi tisa yaliyoainishwa katika kifungu cha 22(1)(c) bila kufafanua taasisi
husika za kila kundi wala idadi ya wajumbe kwa kila kundi, aya ya 2(a) ya
Muswada inapendekeza idadi ya wajumbe kwa kila kundi lililotajwa katika kifungu
hicho. Hivyo, kwa mfano, kundi la taasisi zisizokuwa za kiraia litawakilishwa
na wajumbe ishirini; taasisi za kidini zitawakilishwa na wajumbe ishirini, na
vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu vitawakilishwa na wajumbe arobaini na
mbili.
Makundi
mengine ni taasisi za elimu ya juu ambazo zitawakilishwa na wajumbe ishirini;
makundi ya watu wenye mahitaji maalum wajumbe ishirini, na vyama vya
wafanyakazi ambavyo vitawakilishwa na wajumbe kumi na tisa. Mengine ni vyama
vinavyowakilisha wafugaji vitakavyowakilishwa na wajumbe kumi; wajumbe kumi
kutoka vyama vya wavuvi; wajumbe ishirini kutoka vyama vya wakulima, na wajumbe
ishirini kutoka makundi mengine yoyote ya watu wenye maslahi yanayofanana.
Aya
ya 2(b) ya Muswada inamtaka Rais kuyaalika makundi hayo kutoka pande zote mbili
za Jamhuri ya Muungano kumpelekea orodha ya majina ya watu wasiopungua sita na
wasiozidi tisa kwa ajili ya kufikiriwa kuteuliwa kuwa wajumbe wa Bunge Maalum.
Kwa kila jina litakalopendekezwa, kutaonyeshwa umri, jinsia, uzoefu, ujuzi na
mahali anapoishi mhusika. Na katika kufanya uteuzi kutokana na majina hayo,
Rais atatakiwa kutilia maanani uwiano wa kijinsia.
Mheshimiwa
Spika,
Mapendekezo
ya marekebisho haya ni mapya na kwa kiasi fulani ni hatua chanya ikilinganishwa
na Sheria kama ilivyo sasa. Kwanza, ongezeko lolote la wajumbe wasiokuwa Wabunge
na Wawakilishi linapunguza hodhi ya vyama vya siasa kwa mchakato wa Katiba
Mpya. Hii ni kwa sababu, sifa mojawapo kuu ya Wabunge au Wawakilishi wa aina
zote ni kwamba wote wametokana na ni wanachama wa vyama vya siasa.
Pili,
kwa kuweka idadi ya wajumbe watakaowakilisha kila kundi lililotajwa na kifungu
cha 22(1)(c) cha Sheria, kuna uwezekano mkubwa zaidi wa makundi hayo
kuwakilishwa katika Bunge Maalum kuliko ambavyo idadi ya kila kundi isingewekwa
wazi. Tatu, kwa sababu ya ongezeko la wajumbe wasiokuwa Wabunge na Wawakilishi,
kuna uwezekano mkubwa zaidi wa mjadala katika Bunge Maalum kuwa bora zaidi kwa
kuingiza sauti na mitazamo isiyotawaliwa na maslahi ya kivyama. Yote haya
yanaongeza uwezekano wa kupatikana Katiba Mpya yenye taswira ya Kitanzania
zaidi badala ya Katiba yenye taswira ya kivyama zaidi na hayana budi kuungwa
mkono.
Hata
hivyo, Mheshimiwa Spika, mapendekezo haya bado hayajatosheleza haja ya kuwa na
mchakato wa kidemokrasia zaidi na wenye kujenga maridhiano ya kitaifa katika
kutengeneza Katiba Mpya. Kwanza, kwa kuendelea kumng’ang’aniza Rais kuwateua
wajumbe hawa, Muswada huu unaendeleza dhana ya Urais wa Kifalme katika mchakato
wa Katiba Mpya. Tumeielezea dhana hii kwa kirefu kuhusiana na mchakato huu kiasi
kwamba hatuna haja ya kujirudia rudia hapa. Itoshe tu kukumbushia kwamba hata
Chama cha Mapinduzi (CCM) katika enzi za ujana wake kilikuwa kinatambua hatari
ya Urais wa Kifalme katika mfumo wa kikatiba na kisheria wa nchi yetu. Ndio
maana katika Mwongozo wake wa 1981, CCM ililalamika kwamba “madaraka mengi na makubwa yamelimbikizwa
katika Ofisi ya Rais.”
Ukweli ni kwamba hata Rais Kikwete mwenyewe
ameonyesha dhahiri kwamba hataki mamlaka haya ambayo Muswada huu
unamng’ang’aniza. Katika mkutano wake na viongozi wakuu wa vyama vya siasa,
Mheshimiwa Rais alisema kwamba alikuwa tayari kuyaachia makundi yaliyotajwa
katika kifungu cha 22(1)(c) kuteua wawakilishi wao wenyewe endapo vyama vya
siasa vingekubaliana juu ya formula ambayo
ingehakikisha uwiano mzuri wa jinsia unazingatiwa. Ndiyo maana vyama vya siasa
vyenye uwakilishi ndani ya Bunge hili vilikubaliana kwamba “kifungu cha 22(2A) cha Sheria kama ilivyo
sasa kifutwe kabisa ... (na) kwamba wajumbe waliotajwa katika kifungu cha
22(1)(c) watateuliwa na taasisi watakazoziwakilisha.”
Pili,
kwa kutaja makundi ya jumla badala ya kutaja taasisi zinazounda makundi hayo,
Muswada unatoa mwanya kwa Rais kuteua watu anaowataka yeye na kueleza kwamba
wametokana na kundi mojawapo ya yale yaliyotajwa katika kifungu cha 22(1)(c)
cha Sheria. Kwa kiasi fulani, hivyo ndivyo ilivyotokea wakati wa mchakato wa
kuteua wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, kwa kadri ya taarifa
zilizotolewa na wadau mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge lako tukufu ya Katiba,
Sheria na Utawala wakati wa kujadili marekebisho ya pili ya Sheria hii mwezi
Agosti mwaka huu.
Tatu,
hata kama majina atakayopelekewa Rais hayatachakachuliwa, mapendekezo ya aya ya
2(b) hayawezi kutekeleza matakwa ya kuwa na wajumbe mia mbili na moja
wanaopendekezwa kwenye aya ya 2(a) ya Muswada huu. Hii ni kwa sababu aya hiyo
inapendekeza Rais apelekewe majina yasiyopungua sita na yasiyozidi tisa kutoka
kila kundi lililotajwa katika kifungu cha 22(1)(c) kutoka sehemu mbili za
Jamhuri ya Muungano.
Assuming,
kama aya ya 2(b) inavyoashiria, kwamba kila sehemu ya Jamhuri ya Muungano ina
makundi yaliyotajwa katika kifungu hicho, kutakuwa na makundi ishirini yatakayotakiwa
kupeleka majina kati ya sita na tisa kwa Rais kwa ajili ya uteuzi. Sasa endapo
kila moja ya makundi hayo litapeleka idadi ya juu kabisa inayopendekezwa na
Muswada; na endapo wajumbe wote hao watateuliwa kuwa wajumbe wa Bunge Maalum,
idadi yao itakuwa mia moja themanini. Kutakuwa na baki ya wajumbe ishirini na
moja ambao haijulikani watatoka wapi.
Kwa
upande mwingine, endapo kila kundi lililotajwa litapeleka idadi ya chini kabisa
ya majina kama inavyopendekezwa; na idadi hiyo wakateuliwa wote bila kuacha
hata mmoja, basi idadi ya wajumbe wa Bunge Maalum wasiotokana na Bunge au
Baraza la Wawakilishi itakuwa mia moja na ishirini. Kutakuwa bado na akiba ya
wajumbe themanini na moja ambao haijulikani watapatikana wapi na kwa utaratibu
gani. Kwa vyovyote vile linavyoangaliwa, pendekezo la aya ya 2(b) haliwezi
kutekeleza matakwa ya pendekezo la aya ya 2(a) ya Muswada huu kuhusu idadi ya
wajumbe wa Bunge Maalum wasiokuwa Wabunge na Wawakilishi.
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza namna tatu za kutatua tatizo hili. Njia ya kwanza ni kufuta kabisa pendekezo la Rais kupelekewa kati ya majina sita hadi tisa kwa ajili ya uteuzi. Badala yake, aya ya 2(b) ipendekeze kwamba Rais apelekewe na makundi husika majina kulingana na idadi iliyopangwa kwa kila moja ya makundi yaliyotajwa na kifungu cha 22(1)(c) cha Sheria. Hii itahakikisha kwamba idadi ya wajumbe mia mbili na moja inayopendekezwa inafikiwa.
Kwa
wanaopendekeza kivuli kikubwa cha Rais katika mchakato wa Katiba Mpya
kiendelee, pendekezo hili litamwondolea Rais discretion aliyo nayo katika kuteua wajumbe hao wa Bunge Maalum.
Badala yake, kazi ya Rais itakuwa ni mere
formality kwa maana kwamba atateua wajumbe kutokana na idadi kamili
atakayopatiwa na kila kundi.
Namna
ya pili ya kutatua tatizo lililoletwa na pendekezo la aya ya 2(b) ya Muswada ni
kufanya idadi ya majina atakayopelekewa Rais kuwa kubwa zaidi ya idadi ya
wajumbe wa kila kundi. Hivyo, kwa mfano, kundi la taasisi zisizo za kiserikali,
au za kidini, au taasisi za elimu ya juu, litapeleka majina kati ya thelathini
hadi arobaini ili Rais ateue wajumbe ishirini wa kundi hilo kama
inavyopendekezwa na aya ya 2(a). Aidha, kwa makundi ya vyama vya wafanyakazi,
au wakulima, au wafugaji nayo yatapeleka majina mengi zaidi ya mgawo wao ili
Rais aweze kuteua idadi ya wajumbe inayotakiwa kwa kila kundi.
Pendekezo
hili litahifadhi mamlaka substantive ya
uteuzi aliyo nayo Rais, lakini litathibitisha dhana kwamba wajumbe hao ni watu
wa Rais badala ya kuwa wawakilishi wa makundi yaliyowapendekeza.
Njia
ya tatu ya kutatua tatizo la namna ya kuwapata wajumbe wa Bunge Maalum
waliotajwa katika aya ya 2(a) ya Muswada ni kuzitaja taasisi zinazounda makundi
hayo na kuzigawia idadi ya wajumbe watakaoteuliwa kutoka kila taasisi. Hapa
inawezekana kila taasisi iliyotajwa kupeleka majina kulingana na idadi ya
wajumbe iliyotengewa, kama ulivyo msimamo wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni;
au kupeleka idadi kubwa zaidi ya majina kuliko idadi ya wajumbe wa kutoka taasisi
hiyo, na hivyo kumpa Rais flexibility ya
kuteua anavyoona yeye inafaa, kama inavyopendelewa na Serikali. Sehemu ya
kwanza ya pendekezo hili ilikwishakubaliwa na wakuu wa vyama vinavyounda TCD
lakini ikakataliwa na Serikali. Huu ni wakati muafaka wa kulifikiria tena
pendekezo hili.
2.
HOJA YA GHARAMA ZA
BUNGE MAALUMMheshimiwa Spika,
Serikali hii ya CCM imetumia hoja mbili kukataa kuongeza idadi ya wajumbe wa Bunge Maalum. Kwanza, inadaiwa kwamba ongezeko la wajumbe, kama ilivyopendekezwa na wadau wengi, litaongeza gharama za Bunge Maalum katika nyakati hizi za ‘Sungura Mdogo’ na economic belt-tightening. Pili, inadaiwa kwamba Ukumbi huu wa Bunge lako tukufu – unaotazamiwa kuwa venue ya Bunge Maalum – hautatosha endapo idadi ya wajumbe itaongezeka kama inavyopendekezwa.
Mheshimiwa
Spika,
Mchakato
wowote wa maana wa kutengeneza Katiba Mpya huwa na gharama kubwa. Hii ni kweli
kwa nchi zote ambazo zimepitia mchakato huo, na itakuwa kweli kwa Tanzania pia.
Kama Waheshimiwa Wabunge watakavyokumbuka, tangu mchakato huu uanze kwa uteuzi
wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Mei Mosi 2012, Bunge lako tukufu
limekwishaidhinisha zaidi ya shilingi bilioni 74.463 kwa ajili ya shughuli za
Tume peke yake. Kwa vyovyote vile itakavyokuwa, shughuli za Bunge Maalum
zitakuwa na gharama kubwa pia, kama sio zaidi.
Pamoja
na ukweli huu, hoja zote mbili za Serikali hii ya CCM ni potofu. Kwanza, hadi
sasa, licha ya kutakiwa kufanya hivyo katika Mkutano wa Kumi na Moja wa Bunge
la Bajeti, Serikali haijatangaza – na wala Bunge lako tukufu halijaidhinisha –
bajeti yoyote ya Bunge Maalum. Kwa sababu hiyo, hakuna msingi wala ushahidi
wowote wa kupima ukweli na uhalali wa hoja ya ongezeko kubwa la gharama
linalodaiwa na Serikali hii ya CCM endapo wajumbe wa Bunge Maalum wataongezwa
kama ilivyopendekezwa na wadau mbali mbali, wakiwamo vyama vyetu vya siasa. Vinginevyo,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali hii ya CCM ilieleze Bunge
lako tukufu na Watanzania kwa ujumla makadirio ya gharama za shughuli za Bunge
Maalum. Aidha, Serikali ieleze gharama hizo zimeidhinishwa na kikao kipi cha
Bunge lako tukufu.
Pili,
licha ya ukweli wa gharama kubwa za kutengeneza Katiba Mpya, gharama za
mchakato mbovu ni kubwa zaidi. Gharama hizo hazijumuishi fedha, muda na
rasilmali nyingine peke yake, bali pia zinaweza kujumuisha uharibifu mkubwa wa
mali na uchumi, na hata upotevu wa maisha ya watu, endapo maridhiano na muafaka
wa kitaifa havitapatikana na nchi ikaingia katika mtafaruku na machafuko ya
kisiasa.
Kwenye
jambo hili hatuna budi kujifunza kutoka kwa majirani zetu wa Kenya ambapo Rais
wa nchi hiyo na Makamu wake wanakabiliwa na mashtaka ya makosa dhidi ya
ubinadamu katika Mahakama ya Jinai ya Kimataifa, The Hague, kufuatia vurugu za
kisiasa zilizosababishwa na machafuko ya Uchaguzi Mkuu wa Desemba, 2007.
Uchaguzi huo ulifanyika baada ya mchakato wa Katiba Mpya ya nchi hiyo kuvunjika
mwaka 2006 pale Rasimu ya Katiba Mpya ilipokataliwa na Wakenya kwenye kura ya
maoni. Matokeo yake, maelfu ya watu waliuawa au kujeruhiwa, mabilioni ya fedha
na mali kuteketea na jumuiya ya kimataifa kuingilia kati kabla Wakenya
hawajafunguka macho kwamba kujenga muafaka wa kitaifa juu ya Katiba Mpya ni
gharama nafuu zaidi kuliko kiasi chochote cha fedha!
Tatu,
hoja ya udogo wa Ukumbi kwa ajili ya Bunge Maalum ni ya kuchekesha. Kwanza, tangu
kuzaliwa kwake zaidi ya miaka thelathini na sita iliyopita, CCM imefanyia
Mikutano yake yote Mikuu hapa Dodoma. Hata vyama vya upinzani kama CHADEMA na
CUF navyo vimefanya Mikutano yao Mikuu au Mabaraza ya Taifa hapa hapa nchini.
Mikutano na Mabaraza hayo ina mamia na hata maelfu ya wajumbe na suala la udogo
wa kumbi za kuifanyia halijawahi kuizuia isifanyike.
Pili,
hoja hii inapingana moja kwa moja na kauli ya Katibu wa Bunge lako tukufu kwa
vyombo vya habari kwamba Ukumbi huu utawekewa viti vingine 750 “ambavyo
vitatosha ukumbini hapo bila kubanana.” Na hata kama bado hautatosha kwa ajili
ya idadi ya wajumbe wa Bunge Maalum wanaopendekezwa na wadau, basi ukumbi mwingine
mkubwa zaidi unaweza kutafutwa hapa hapa Dodoma na hata nje ya Dodoma kama ikihitajika.
Muafaka wa kitaifa juu ya Katiba Mpya ni muhimu zaidi kuliko gharama za ukumbi
wa mikutano.
3.
MAKATIBU WA BUNGE
MAALUMMheshimiwa Spika,
Aya ya 3(a) ya Muswada inapendekeza kumpa Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na Katibu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar mamlaka ya kufanya “... maandalizi muhimu kwa ajili ya utekelezaji bora wa shughuli za Bunge Maalu.” Katika haraka haraka ya kupitisha marekebisho ya pili ya Sheria hii, suala hili halikuwekwa kwenye Muswada na hivyo halikufikiriwa na Bunge lako tukufu. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaunga mkono pendekezo hili.
4. HATIMA YA TUME YA MABADILIKO YA KATIBA
Mheshimiwa Spika,
Kwa mujibu wa Sheria kama ilivyo sasa, Tume ya Mabadiliko ya Katiba itavunjwa na Rais “baada ya kuwasilishwa kwa Rasimu ya Katiba kwenye Bunge Maalum....” Hata hivyo, kwa mujibu wa kifungu kipya cha 20(4) cha Sheria, “... Katibu wa Bunge Maalum anaweza, kwa kushauriana na Mwenyekiti wa Bunge Maalum, kumwalika Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti au Mjumbe yeyote wa Tume iliyovunjwa ili kutoa ufafanuzi utakaohitajika wakati wa mjadala wa Bunge Maalum.”
Licha
ya matakwa haya ya Sheria kama ilivyo sasa, kifungu cha 33(2) cha Sheria hiyo
hiyo kinailazimisha Tume “... kutoa elimu
ya uraia na uhamasishaji juu ya Katiba inayopendekezwa kwa muda usiozidi siku
thelathini kuanzia siku ya kuchapishwa (kwa taarifa ya kura ya maoni) katika
Gazeti la Serikali.” Hii ni kwa “madhumuni
ya kuelimisha na kuhamasisha wananchi kuhusu kuipigia kura ya maoni Katiba
inayopendekezwa....” Aidha, sambamba na kifungu cha 33(2) cha Sheria, Bunge
lako tukufu limetenga mabilioni ya fedha kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu
haya ya Tume katika mwaka huu wa fedha wa 2013/2014.
Mheshimiwa
Spika,
Pendekezo
la kuivunja Tume mara tu baada ya kuwasilisha ripoti yake na Rasimu ya Katiba
kwa Rais halikuwa sehemu ya Muswada wa Sheria ya Marekebisho iliyopitishwa
katika Mkutano uliopita wa Bunge lako tukufu. Kwa mujibu wa Taarifa Rasmi ya
Majadiliano ya Bunge (Hansard) ya tarehe 6 Septemba, 2013, hoja hiyo ililetwa
Bungeni na Mheshimiwa Selemani Jafo. Katika hoja yake, Mheshimiwa Jafo alidai
kwamba pendekezo hilo “... ni kutokana na kilio cha Watanzania wengi waliokuwa
wanapiga kelele mpaka wengine kuwavunjia heshima wazee wetu ambao kwa kweli
wapo tu....”
Taarifa
hiyo ya Hansard inaonyesha kwamba hoja ya Mheshimiwa Jafo iliungwa mkono na
Waziri wa Katiba na Sheria, Mheshimiwa Mathias Chikawe kwa maneno yafuatayo: “Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hili Mheshimiwa
Jafo wala asipoteze nguvu nyingi sana kulisemea, kwa sababu na mimi naliona na
ninakubali kwa sababu ... inawezekana ilikuwa tu ni oversight kwa upande wetu
tulipokuwa tunatunga hii sheria. Haiwezekani Tume ikaendelea bila kuvunjwa.”
Taarifa hiyo inaonyesha vile vile kwamba hoja ya Mheshimiwa Jafo iliungwa mkono
pia na Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Mheshimiwa Spika,
Katika hotuba yake kwa wananchi ya tarehe 4 Oktoba, 2013, Rais Kikwete aliisifu kazi ambayo Tume imeifanya kwa maneno yafuatayo: “Bahati nzuri (kutengeneza Katiba ya watu wa vyama vyote na wasiokuwa na vyama ambao ndio wengi kuliko wote) ndio sifa kubwa iliyoonyeshwa na wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Wamewasimamia na kuwasemea watu wote bila ya kubagua. Natambua kuwepo kwa baadhi ya watu ambao hawafurahii msimamo huo na matokeo ya kazi yao. Watu hao kuwalaumu wajumbe wa Tume kwa ajili hiyo ni kutowatendea haki.”
Akizungumzia
uhai wa Tume, Mheshimiwa Rais alisema yafuatayo: “Katika orodha ya madai ya ndugu zetu wa upinzani lipo suala la uhai wa
Tume ya Katiba. Wanataka usiishe wanapokabidhi rasimu ya pili kwa Bunge Maalum
bali waendelee kuwepo mpaka mwisho wa mchakato. Nimeulizia ilikuwaje?
Nimeelezwa kuwa jambo hili halitokani na mapendekezo ya Serikali wala ya Kamati
ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala. Limetokana na pendekezo la Mbunge katika
Bunge wakati wa kupitia vifungu na kuungwa mkono na Wabunge wengi. Kwa hiyo
kuilaumu Serikali si haki. Serikali inaweza kuwa mshirika katika hoja hii. Name
naiona hoja ya Wajumbe wa Tume kuwa na wajibu wakati wa Bunge Maalum hasa wa
kusaidia kufafanua mapendekezo ya Tume.”
Kama
Mheshimiwa Rais mwenyewe anaiona ‘hoja ya wajumbe wa Tume kuwa na wajibu wakati
wa Bunge Maalum hasa wa kusaidia kufafanua mapendekezo ya Tume’, haitaeleweka
endapo Bunge lako tukufu litakataa kufanya marekebisho ya Sheria hii ili
kuiwezesha Tume kuendelea kuwepo kama ilivyokuwa kabla marekebisho ya pili
hayajapitishwa. Kwa sababu hizo, na kama walivyokubaliana viongozi wakuu wa
vyama vya kibunge, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza kama ifuatavyo
kuhusu hatima ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba:
a) Kifungu cha 20(4)
cha Sheria kifutwe kabisa;(b) Kifungu cha 22(1) kirekebishwe kwa kuongeza aya ya (d) mara baada ya aya (c) itakayosomeka kama ifuatavyo: “Wajumbe wa Tume ambao hawatakuwa na haki ya kupiga kura katika Bunge Maalum, yaani watakuwa wajumbe ex officio wa Bunge Maalum.”
(c) Kifungu cha zamani cha 37(1) kirejeshwe ili kuwezesha uwepo wa Tume hadi baada ya matokeo ya kura ya maoni kutangazwa kama ilivyokuwa kabla ya marekebisho ya pili ya Sheria hii.
5. UTARATIBU WA KUPITISHA VIFUNGU VYA KATIBA MPYA
Mheshimiwa Spika,
Aya
ya 4 ya Muswada huu inapendekeza kufutwa kwa vifungu vidogo vya (3), (4), (5),
(6) na (7) vya kifungu cha 26 ambavyo viliingizwa na marekebisho ya pili.
Vifungu hivyo vilikuwa na athari ya kuruhusu Katiba Mpya kupitishwa kwa wingi
wa kawaida wa wajumbe wa Bunge Maalum. Mapendekezo ya marekebisho ya kifungu
yana athari ya kurudisha status quo ante,
yaani hali kama ilivyokuwa kabla ya marekebisho ya pili ya Sheria hii. Kwa maana
hiyo, endapo mapendekezo haya yatakubaliwa na Bunge lako tukufu, Katiba Mpya itaamuliwa
kwa wingi maalum wa theluthi mbili ya wajumbe wote wa Bunge Maalum wanaotoka
Tanganyika na idadi hiyo hiyo ya wajumbe wanaotoka Zanzibar. Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni inayakubali mapendekezo haya na inawasihi Waheshimiwa Wabunge wote
wayaunge mkono.
6.
UHALALISHAJI WA
KATIBA MPYAMheshimiwa Spika,
Aya
ya 5 ya Muswada inapendekeza kufutwa kwa vifungu sita vya Sehemu ya Sita ya
Sheria inayohusu uhalalishaji wa Katiba Mpya. Kama tulivyosema awali, vifungu
vinavyofutwa vimehamishiwa katika Muswada wa Sheria ya Kura ya Maoni, 2013.
Vifungu viwili vinavyopendekezwa kubaki ni kifungu cha 37 kinachohusu kuvunjwa
kwa Tume na ambacho tumekwishakijadili kwa kirefu; na kifungu cha 38
kinachohusu kuanza kutumika kwa Katiba Mpya. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inakubaliana na mapendekezo ya marekebisho haya na inasihi Waheshimiwa Wabunge
wote wayaunge mkono.
Mheshimiwa
Spika, Baada ya kusema yote haya naomba kuwasilisha.
Tundu Antiphas Mughwai Lissu (MB)
MSEMAJI, KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI
&
WAZIRI KIVULI, KATIBA NA SHERIA
No comments:
Post a Comment