TANGAZO


Friday, November 8, 2013

Kimbunga Hayan chaipiga Ufilipino

 


Picha ya satalaiti ikionyesha kimbunga Haya
 
Kimbunga kikali kinachokadiriwa kuwa kibaya zaidi kuwahi kushuhudiwa kimeanza kuipiga Ufilipino. Kimbunga hicho kijulikanacho kama "Super typhoon Hayan"kimeandamana na upepo mkali unaovuma kwa kasi ya karibu kilomita 300 kwa saa na kusababisha mawimbi ya bahari kwenda juu urefu wa mita 15 katika maeneo ya pwani.
 
Wataalam wa masuala ya hali ya hewa wanasema iwapo makadirio ya mwanzo yaliyozingatia picha za satelaiti yatakuwa hivyo, basi kimbunga hicho kitakuwa kikubwa kuliko vyote kuwahi kutokea katika nchi.
 
Shule na maofisi vimefungwa kuepuka madhara ya kimbunga Hayan, na maelfu ya watu wamehamishwa kutoka maeneo yanayohofiwa kukumbwa na kimbunga hicho, ili kuepuka madhara makubwa.
Eneo lililokumbwa na kimbunga Hayan, lilikuwa linarejea katika hali yake ya kawaida baada ya kupigwa na tetemeko la ardhi mwezi uliopita.

Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa nchini Ufilipino imesema madhara makubwa ya kimbunga hicho yameshuhudiwa umbali wa kilomita 62 kusini mashariki mwa mji wa Guiuan, katika jimbo la Samar lililopo mashariki mwa Ufilipino.

Gavana wa jimbo la Leyte kusini mwa nchi hiyo, Roger Mercado, ametuma ujumbe wa mtandao wa tweeter Ijumaa asubuhi akisema miti iliyoangukia barabarani imezuia mawasiliano ya usafiri na hivyo kukwamisha shughuli za uokoaji.

Kimbunga hicho hakitarajiwi kuupiga moja kwa moja mji mkuu Manila ulioko kaskazini mwa nchi.
Watu wapatao 5,000 wangali wakiishi katika mahema katika kisiwa cha Bohol baada ya kupoteza nyumba zao kutokana na tetemeko la ardhi la ukubwa wa 7.3 na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 200 mwezi uliopita

No comments:

Post a Comment