Eddah Mwakale (kulia), Manase Mwakale (katikati) na Bahati Mahenge (kushoto), wakiwa mahakamani Kisutu leo, ilipotolewa huku yao.
Washtakiwa katika kesi ya Epa, Manase Mwakale (mbele) na Bahati Mahenge (kushoto), wakiongozwa na askari Polisi, kutoka kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kupelekwa kwenye gari baada ya kuhukumiwa kwenda jela miaka 13 baada ya kupatikana na hatia katika kesi hiyo, Dar es Salaam leo.
Na Grace Gurisha
VIGOGO watatu katika kesi ya wizi wa sh. bilioni 1.1 fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), wamehukumiwa kifungo cha miaka 13 jela.
Vigogo hao, ambao ni mfanyabiashara Bahati Mahenge, Manase Makalle na Edda Makalle, ambapo sanjari na kifungo hicho, Mahenge na Manase watatakiwa kurejesha sh. bilioni 1.1.
Hukumu hiyo, imetolewa leo, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na jopo la Mahakimu Wakazi watatu, Sekela Mosha (Mwenyekiti wa Jopo), Lameck Mlacha na Sam Rumanyika.
Mlacha alisema Mahenge atatumikia kifungo cha miaka saba jela, Manase atatumikia kifungo cha miaka mitano jela na mkewe ambaye ni mshtakiwa katika kesi hiyo, Edda atatumikia kifungo cha mwaka mmoja na nusu jela.
Katika shtaka la kwanza la kula njama Mahenge amehukimiwa kifungo cha miaka mitano, shtaka la pili la kughushi Mahenge na Manase wamehukumiwa kifungo cha miaka 5, shtaka la tatu Mahenge amehukumiwa kifungo cha miaka saba jela.
Pia katika shtaka la nne Mahenge na Manase walihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela, shtaka la tano Mahenge, Manase na Edda walihukumiwa kifungo cha miezi 18 jela.
Hata hivyo, katika shtaka la sita Mahenge na Manase wamehukumiwa miezi 18 jela na shtaka la saba Mahenge alihukumiwa kifungo cha miaka mitano.
Katika shtaka la nane la wizi na shtaka la tisa la kujipatia ingizo kwa njia ya udanganyifu yalifutwa, baadaya upande wa Jamhuri kutokufanya marekebisho katika vifungu vya sheria.
Hata hivyo, mahakama hiyo, imewaachia huru washtakiwa wawili kwenye kesi hiyo Davis Kamungu na Godfrey Mosha baada ya kuwaona hawana hatia.
Kamungu na Mosha waliachiwa huru, baada ya upande wa Jamhuri kushindwa kuthibitisha mashtaka yanayowakabili bila kuacha shaka lolote.
Kabla ya hukumu hiyo kutolewa, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Shedrack Kimaro alidai kuwa upande wa Jamhuri hauna rekodi kama washtakiwa walishawahi kufanya makosa.
Pia aliiomba mahakama itumie kifungu cha 348(1) na cha 358(1) cha mwenendo wa mashauri ya jinai sura ya 20 kuwaamuru washtakiwa waliotiwa hatiani kuresha fedha walichukua na kuisababishia Serikali hasara.
Mahenge aliiomba mahakama impunguzie adhabu kwa sababu ana watoto wanne, wazazi wake ni wazee wote wanamtegemea.
Manase alidai kuwa ni mgonjwa anafamilia kubwa inayomtegemea na mshtakiwa Edda ni mkewe hivyo kama wote watahukumiwa watoto wao watateseka.
Washtakiwa hao walikuwa wanadaiwa kuiba sh. bilioni 1.1 za EPA, kupitia kampuni yao ya Changanyikeni Residential Complex.
Washtakiwa hao wanadaiwa kuiba pesa hizo baada ya kughushi nyaraka zinazoonesha kuwa Kampuni ya Marubeni Corporation ya Japan, ambayo ilikuwa ikiidai BoT kiasi hicho cha fedha, iliipa kampuni ya Changanyikeni Residential Complex, idhini ya kukusanya deni lake.
No comments:
Post a Comment