Ofisa Habari, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Asiatu Msuya, akieleza kwa waandishi wa habari (hawapo pichani), kuhusu ufunguaji wa Ofisi 23 katika Mikoa mbalimbali nchini, ili kutekeleza Mpango wa kutenganisha Upelelezi na uendeshaji wa Mashtaka, wakati wa mkutano na waandishi, uliofanyika ukumbi wa Idara ya Habari (Maelezo) leo, jijini Dar es Salaam. Kulia ni Wakili wa Serikali Mkuu wa Ofisi hiyo, Frederick Manyanda. (Picha zote na Hassan Silayo-Maelezo)
Wakili wa Serikali Mkuu, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Manyanda (kulia), akieleza kwa waandishi wa (hawapo pichani), mkakati wa kuhakikisha kuwa huduma ya usimamizi na utoaji wa haki inawafikia wananchi wote kwa karibu kwa kufungua Ofisi zaidi mikoani, wakati wa mkutano na waandishi, uliofanyika ukumbi wa Idara ya Habari (Maelezo) leo, jijini Dar es Salaam. Katikati ni Ofisa Habari toka ofisi hiyo, Asiatu Msuya na kushoto ni Ofisa Habari wa Idara ya Habari, Maelezo, Georgina Misama.
OFISI ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
imefanikiwa kufungua Ofisi 23 katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga,
Kilimanjaro (Moshi), Arusha, Mwanza, Kagera (Bukoba) Mara (Musoma), Shinyanga,
Tabora, Singida, Iringa, Mbeya, Mtwara, Lindi, Dodoma, Rukwa
(Sumbawanga),Ruvuma (Songea), Njombe, Manyara, Morogoro, Kigoma, Geita na Pwani. Aidha jumla ya Ofisi mbili
(2) za zimefunguliwa katika Wilaya za Temeke na Monduli. Kwa mwaka wa fedha
2012/2013 pekee jumla ya Ofisi tano (5) zimefunguliwa katika mikoa ya Pwani,
Kigoma, Morogoro, Manyara, Njombe na Geita ikiwemo pia Ofisi mbili za Wilaya.
Lengo
Lengo kuanzishwa na kuimarishwa kwa Ofisi
hizi za Mikoa na Wilaya ni kuhakikisha kuwa huduma ya usimamizi na utoaji wa
haki inawafikia wananchi wote kwa karibu zaidi. Baadhi ya huduma zinazotolewa
ni pamoja na kuendesha Mashtaka mahakamani, kushughulikia malalamiko na kero za
wananchi kuhusiana na kesi za jinai na madai zinazowakabili, kutembelea mahabusu
na kuratibu upelelezi wa kazi za upelelezi wa makosa ya jinai zinazofanywa na
vyombo pelelezi/chunguzi ikiwemo Polisi, Magereza, Uhamiaji,TAKUKURU.
Utekelezaji wa Mpango wa kutenganisha
Upelelezi na Mashtaka nchini
Serikali kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu
wa Serikali imeendelea kutekeleza mpango huu wa Utenganishwaji wa Upelelezi na
Mashtaka kwa mujibu wa Sheria ambapo mfumo wa Sheria ambao uliwezesha kutungwa
kwa Sheria ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, 2005 na Sheria ya Usimamizi wa
Uendeshaji Mashtaka nchini, 2008 umeboreshwa; pamoja na kuanzishwa kwa Jukwaa
la Ki-taifa la Haki-Jinai (National Criminal Justice Forum) Desemba 2009 linaloviunganisha
pamoja vyombo vyote vinavyosimamia utolewaji wa Haki-Jinai nchini;
Serikali pia imeboresha Muundo wa Divisheni ya Mashtaka kwa
kuweka Sehemu (Section) mahsusi inayosimamia utekelezaji wa mchakato wa
utenganishaji wa kazi za upelelezi na Mashtaka na uratibu wa kazi za
ki-pelelezi; pamoja na kuanzishwa kwa huduma ya Mashtaka ya moja kwa moja
ambako Mawakili wa Serikali wanaendesha kesi; Hii imepelekea idadi ya kesi zinazofunguliwa Mahakamani
ambako Mawakili wa Serikali wanaendesha Mashtaka kupungua ikilinganishwa na
kipindi cha nyuma; Kuongezeka kwa ubora wa huduma zitolewazo na kupungua kwa
kesi za kubambikizwa.
Utekelezaji wa Programu ya Utenganishwaji wa
Mashtaka na Upelelezi (Civilianization) imetoa msukumo mkubwa kwa Ofisi kuingia
uanachama na makubaliano ya mashirikiano na vyama vinavyohusiana na kazi za
Uendeshaji Mashtaka duniani, kama vile-IAP, HOPAC, APA, EAAP, na ARINSA; Serikali
itaendelea kupanua wigo wa uendeshaji wa Mashtaka kwa kuanzisha na kuimarisha
Ofisi katika Wilaya zote nchini pamoja na Mikoa miwili iliyobaki ya Katavi na
Simiyu.
Tunapenda kuwakumbusha Wadau wetu wote na
Wananchi kwa ujumla kuwa mstari wa mbele katika kutoa taarifa za uhalifu au
jinai yoyote katika jamii kwa vyombo husika kupitia utaratibu unaofaa; na kutoa
ushahidi Mahakamani pale unapohitajika kwa kuwa hizi ni nguzo muhimu katika uendeshaji wa kesi mbalimbali. Aidha tunatoa
wito kwa umma, wadau wetu na wananchi wote kwa ujumla pamoja na vyombo vya
habari nchini kufuatilia mtiririko, hoja zinazowalishwa Mahakamani na uamuzi
uliotolewa na Mahakama katika kesi mbalimbali zinazoendelea kuwa na taarifa
sahihi ya kuhusu kesi hizo.
Imetolewa Na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali
Ijumaa, Septemba 27, 2013
No comments:
Post a Comment