Mke wa Rais Jakaya Kikwete, Mama Salma, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA), akizungumza wakati wa halfa ya kukabidhi gari la kubebea wagonjwa lililotolewa na taasisi hiyo kwa Hospitali ya Sokoine, mkoani Lindi leo. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa huo, Ludovick Mwananzila na kulia ni Kaimu Katibu wa hospitali hiyo, Tawani Selemani.
Mama Salma Kikwete akimuonesha gari la kubebea wagonjwa Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Ludovick Mwananzila lililotolewa na Taasisi hiyo kwa Hospitali ya Sokoine leo.
Mama Salma Kikwete akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa Hospitali ya Sokoine, mkoani Lindi baada ya kukabidhi gari hilo.
Mama Salma Kikwete akikabidhi funguo za gari la kubebea wagonjwa kwa Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Sokoine, mkoni Lindi, Dk. Abdallah Chome, wakati wa hafla hiyo leo. Kulia ni Mkuu wa mkoa huo. Ludovick Mwananzila. (Picha na Lorietha Laurence-Maelezo)
Na Anna Nkinda – Maelezo, Lindi
TAASISI ya Wanawake na Maendeleao (WAMA) imeipatia Hospitali ya mkoa wa Lindi (Sokoine ) gari la kubebea wagonjwa aina ya Hyundai lenye namba za usajili SM 1044 ambalo litasaidia kwa kiasi kikubwa kukabiliana na tatizo la upungufu wa vifaa tiba katika Hospitali hiyo.
Hafla hiyo fupi ya makabidhiano ya gari hilo yamefanyika leo katika hospitali hiyo na kuhudhuriwa na wafanyakazi wa Serikali ya mkoa na wahudumu wa sekta ya afya wa Hospitali hiyo.
Alikabidhi gari hilo Mke wa Rais ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi hiyo alisema kuwa lengo la kutolewa kwa gari hilo la wagonjwa ni kuhakikisha kuwa huduma ya afya inaimarika na inawasaidia wananchi wengi wa mkoa huo.
“Taasisi ya WAMA inafanya kazi na wadau mbalimbali wa maendeleo hivyo basi wenzetu wa Korea kupitia Shirika lao la maendeleo la JAICA walitoa gari hili kwa waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bernard Membe ambaye alilikabidhi kwa Taasisi yangu ambao nasi leo tumelileta katika Hospitali hii”, alisema Mama Kikwete.
Mwenyekiti huyo wa WAMA alisema gari hilo ni maalum kwa ajili ya wagonjwa hususani kina mama wajawazito watakaokuwa wanahitaji kupata huduma hiyo lengo kubwa likiwa ni kupunguza vifo vyao na vya watoto wachanga ili nchi iweze kutimiza malengo ya Maendeleo ya Milinia.
Mama Kikwete alisema, “Miaka mitano iliyopita niliwakabidhi gari lingine la kubebea wagonjwa , ni matarajio yangu kwamba magari haya yatatumika vizuri na kila mtu atambue kuwa hiyo ni mali yake na siyo ya WAMA kwani gari likiharibika tatizo ni la wote na ni imani yangu kwamba uongozi wa mkoa unasimamia ili kuhakikisha gari hili litafanya kazi iliyokusudiwa”.
Kwa upande wake mkuu wa Mkoa wa Lindi Ludovick Mwananzila alimshukuru Mama Kikwete kwa vifaa tiba anavyowapatia katika hospitali hiyo na kumuomba asichoke kuwasaidia kwani wananchi wanahitaji msaada na moyo wake wa huruma ili wapate huduma bora ya afya na kutokwenda kutibiwa maeneo ya mbali.
“Viongozi wa mkoa huu waliamua kuwa na hospitali ya Rufaa, hivi sasa kiwanja tunacho na michoro ya kujengea majengo iko tayari changamoto iliyopo ni hatuna fedha za kuanza ujenzi . Tunaomba utusaidie kututafutia wafadhili wa kutujengea hospitali jambo ambalo litapunguza idadi ya wagonjwa wanaotibiwa hapa”, alisema Mwananzila.
Wastani wa mahudhurio ya wagonjwa kwa siku katika hospitali hiyo ni kati ya 80 hadi 100 na wagonjwa wanaolala wodini kwa usiku mmoja ni kati ya 70 hadi 100 pia huduma zinazopatikana ni kutibu magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukia na utoaji wa chanjo na elimu ya afya kwa umma.
No comments:
Post a Comment