Mamia ya wahamiaji haramu wamevunja sehemu ya uzio wa nyaya wenye urefu wa futi 19 ambao unazingira eneo linalomilikiwa na Uhispania la Melilla, Kaskazini mwa Afrika.
Takriban watu 100 walivunja uzio huo kutoka upande wa Morocco na kuingia Ulaya.
Walinzi sita wa kiraia wa Uhispania walijeruhiwa kwenye sokomoko hilo na polisi.
Mhamiaji mmoja alivunjika mguu alipoanguka kutoka juu ya uwa huo kwa mujibu wa maafisa wa Uhispania.
Maelfu ya raia huingia nchini Morocco na kujaribu kuvuka mpaka kuingia Ulaya.
Eneo la Melilla, makao kwa takriban watu 80,000 lina moja ya mipaka miwili ya Ulaya inayopakana na Afrika.
Mpaka mwingine ni wa Ceuta, eneo lengine la Uhispania Kaskazini mwa Morocco.
Serikali ya Uhispania inasema kuwa migogoro inayoshuhudiwa Kaskazini mwa Afrika, imesababisha ongezeko la watu wanaojaribi kuingia Ulaya kwa kuvuka mpaka huo.
Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, Wahamiaji hao walioingia katika eneo la Melilla mapema Jumanne watahifadhiwa katika kituo cha kuwapokea wahamiaji.
Gavana wa Melilla, Abdelmalik el-Barkani, alisema kuwa mnamo mwezi Mei, walikuwa na wakati mgumu kukabiliana na ongezeko la wahamiaji.
No comments:
Post a Comment