Wanasheria wanaomwakilisha Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta, wametaka mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC kumruhusu mteja wao kutohudhuria baadhi ya vikao vya kesi dhidi yake itakayoanza katika mahakama hiyo mwezi ujao.
Bwana Kenyatta anakabiliwa na kesi ya uhalifu dhidi ya binadamu kufuatia machafuko ya baada ya uchaguzi yaliyoikumba Kenya mwaka 2007.
Stakabadhi rasmi iliyowasilishwa mbele ya majaji wa mahakama ya ICC jana Jumatatu inatoa ombi kwamba Uhuru Kenyatta, aruhusiwe japo kwa masharti kutohudhuria kesi yake mfululizo, ila awe tu mahakamani wakati wa kuanza kwa vikao vya kesi hiyo na hatimaye wakati wa kutolewa hukumu.
Mawakili wa bwana Kenyatta wanadai kuwa anastahili kuruhusiwa kufuatilia vikao vingine muhimu vya kusilizwa kwa kesi hiyo kupitia picha za video.
Huenda ikadhaniwa kwamba hatua ya bwana Kenyatta kutoa ombi hili wakati kumetokea shambulio la kigaidi katika jengo la kibiashara la Westgate jijini Nairobi kuwa sadfa lakini wengi wanadhani kuwa ni mojawepo wa mbinu za kulemaza kesi dhidi yake.
Mawakili wa bwana Kenyata wametaja kwamba Naibu rais William Ruto ambaye pia anakabiliwa na mashtaka kama yake mbele ya Mahakama hiyo ya ICC ameruhusiwa hivi punde kurejea nyumbani kukabiliana na hali baada ya shambulizi hilo la Westgate mwishoni mwa juma.
No comments:
Post a Comment