Baadhi ya Maafisa Mawasilino Serikalini waliohudhuria mkutano huo wa tathmini uliofanyika jana katika Ukumbi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Jijini Dar es Salaam.
MKURUGENZI Msaidizi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Bi. Zamaradi Kawawa Akiwasilisha ripoti ya utekelezaji Mikutano ya awamu ya kwanza ya utaratibu wa maafisa mawasiliano kuzungumza na waandishi wa habari kuhusu Sera na Mipango pamoja na ujibuji wa hoja mbalimbali zinazohusu Ofisi zao, kwenye katika mkutano uliofanyika jana Ukumbi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Jijini Dar es Salaam.
Meneja Mawasiliano wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Innocent Mungy Akiwasilisha kwa Maafisa Mawasilino Serikalini juu ya namna bora ya kuandaa na kuboresha taarifa kwa vyombo vya habari, katika mkutano uliofanyika jana Ukumbi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Jijini Dar es Salaam.
MKURUGENZI wa Idara ya Habari na Msemaji
wa Serikali Assah Mwambene akiongea na Maafisa Mawasilino Serikalini (hawamo
pichani) jana wakati mkutano wa tathmini wa awamu ya kwanza ya utaratibu wa
maafisa mawasiliano kuzungumza na waandishi wa habari, ambapo alisisitiza
utoaji wa taarifa za utekelezaji wa Sera na Mipango pamoja na kujibu hoja mbalimbali
zinazohusu Ofisi zao. Kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari,Vijana,Utamaduni
na Michezo Bi. Sihaba Nkinga na katikati ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya
Habari Bi. Zamaradi Kawawa. (Picha zote na Hassan Silayo, Maelezo)
NDUGU Mkurugenzi wa Idara ya Habari, Maelezo
Wakurugenzi, Wakurugenzi Wasaidizi na Mameneja mliopo hapa,
Maafisa Mawasiliano,
Waandishi wa Habari,
Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana Habari za Asubuhi!!!
Awali ya yote napenda kuchukua fursa hii kumshukuru mungu kuweza
kunikutanisha nanyi siku hii ya leo tukiwa na afya njema. napenda kutoa
shukrani zangu za dhati kwenu kwa kuhudhuria mkutano huu muhimu kwa ajili ya
kufanya tathmini ya utekelezaji wa ratiba ya mzunguko wa kwanza wa mikutano ya
Waandishi wa Habari na Wasemaji Serikalini.
Ndugu Washiriki,
Kama mnavyofahamu Wizara
ambayo ina jukumu la kusimamia masuala ya Habari na Uratibu wa Mawasiliano ya
Serikali, iliandaa ratiba kwa ajili ya Ofisi za Serikali kujitangaza kwa umma kupitia
vyombo mbalimbali vya mawasiliano nchini.
Ratiba
hiyo ilianza rasmi Tarehe 4, Julai,2013 na kumalizika Septemba 3,2013 ambapo
Wasemaji wa Taasisi/Wakuu wa Idara/Vitengo vya Mawasiliano Serikalini
walitakiwa kuzungumza na vyombo vya Habari katika siku na muda uliopangwa .
Mikutano 75 ilifanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Idara ya Habari-MAELEZO na
mkutano mmoja wa Hospitali ya Taifa Muhimbili ulifanyika katika ukumbi wa
mikutano wa Kitengo kipya cha magonjwa ya moyo cha Hospitali hiyo iliyopo
Upanga, Dar es Salaam.
Nimeambiwa kuwa Jumla ya Taasisi za Serikali
88 zilitakiwa kushiriki katika mikutano hiyo, kati ya Taasisi hizo, Taasisi 75
sawa na asilimia 85 zilishiriki katika mikutano hiyo na Taasisi 14 sawa na
asilimia 15 hazikushiriki.
Kwa
mara nyingine tena natoa pongezi kwa Taasisi zote zilizoshiriki katika mikutano
hiyo. Mikutano hii ni muhimu na imeleta tija kwa kuwa wananchi kupitia Vyombo
vya Habari nchini walipata fursa ya kuelewa masuala mengi ya msingi
yanayotekelezwa na Serikali kwa lengo la kupunguza umaskini na kukuza uchumi wa
wananchi. Ni ukweli usiopingika kuwa maswali yaliyoulizwa na wananchi kupitia
Waandishi wa Habari wakati wa mikutano hiyo kunaonesha shauku kubwa iliyokuwepo
ya kutaka kujua Serikali inafanya nini kwa ajili ya wananchi wake.
Aidha,
napenda kutoa wito kwa Taasisi ambazo
hazikuhudhuria mzunguko wa kwanza wa mikutano hii wajiandae kwa ajili ya
kushiriki mzunguko wa Pili.
Ndugu Washiriki,
Kama
mnavyofahamu, jukumu kubwa mlilopewa ni
kuwezesha Serikali kupitia Ofisi zenu kufanya
mawasiliano na umma kupitia Vyombo vya Habari kuhusu masuala mbali mbali
yanayohusu Sera na Miradi inayotekelezwa na Serikali yenye lengo la kustawisha maendeleo
ya watanzania. Kwa kufanya hivyo,
Serikali inatimiza wajibu wake wa kutoa haki ya msingi ya wananchi ya kupata
habari hususan zinazohusu utekelezaji wa shughuli mbali mbali za Serikali.
Kumekuwa na malalamiko
ya kutokuridhika na namna ambavyo Serikali haitoi taarifa kwa umma ili kuweza
kutosheleza kiu ya wananchi ya kupata habari zinazohusu utekelezaji wa shughuli
za maendeleo ambazo kwa kiasi fulani huchangiwa na fedha za walipa kodi.
Ndugu Washiriki,
Nitumie nafasi hii
kuwaasa kuwa tumieni fursa za ratiba za mikutano zinazoandaliwa na Idara ya
Habari-MAELEZO ili kukidhi kiu ya jamii ya kuhabarishwa na kuelimishwa shughuli
za Serikali.
Pamoja na mikutano
hiyo inayoratibiwa na Wizara, napenda pia kuwakumbusha kuwa Taasisi kupitia Ofisi zenu kuandaa Mkakati wa
Mawasiliano Serikalini kwa wale ambao hawana na wale ambao tayari wameshaandaa
Mkakati huo utekelezeni kwa dhati ili kufanikisha malengo yaliyokusudiwa.
Aidha, natoa wito kwenu
kama daraja la mawasiliano ya Serikali kwa umma kuelewa Sera na shughuli zote
zinazotekelezwa na Taasisi zenu ili muweze siyo tu kuwa wasemaji wazuri wa Serikali lakini pia
kuwa washauri wazuri wa viongozi katika
ngazi mbali mbali kuhusiana na masuala ya mawasiliano ya Serikali kwa umma.
Nasisitiza kuwa toeni
ushauri ulio sahihi, kwa haraka na wakati ili kutoa majibu mwafaka kwa umma pale ambapo
Vyombo vya Habari vinakuwa vimetoa taarifa zisizo sahihi. Hili lifanyike kwa
vyombo vyote vya Habari vikiwemo Radio, Televisheni, Magazeti na Mitandao ya
Kijamii pale inapolazimu ili kuondoa upotoshaji wa taarifa za Serikali
unaosababishwa na ukuaji wa teknolojia ya Habari na Mawasiliano ambapo kila mtu
anaandika kile anachokijua bila kufuata weledi wa taaluma ya uandishi wa habari.
na utangazaji. Taarifa zisizosahihi
zikiachwa bila kujibiwa zinaweza kuleta uchonganishi kati ya Serikali na
umma na hivyo kusababisha sintofahamu isiyokuwa na ulazima.
Aidha, napenda
kuchukua fursa hii kuwashukuru Waandishi
wa Habari walioshiriki katika zoezi hili kwa mchango mkubwa wa kutoa taarifa
kwa umma kuhusu utekelezaji wa shughuli mbali mbali za Serikali hususan kwa
kazi kubwa mliyoifanya wakati wa mikutano ya Waandishi wa Habari na Wasemaji wa
Taasisi za Serikali iliyoanza Julai 4,2013 na kumalizika Septemba 3, 2013.
Ndugu Washiriki ,
Wizara sasa imeandaa
ratiba ya awamu ya Pili ya Mikutano ya Waandishi wa Habari na Wasemaji wa
Taasisi ambayo inaanza Septemba 16, 2013. Naomba mshiriki kwa kikamilifu na
mjiandae vizuri zaidi kama mlivyofanya awali. Aidha, mkitumie vizuri kikao cha tathmini
kwa kufahamu mafanikio na upungufu uliokuwepo wakati wa utekelezaji wa awamu ya
Kwanza ya Mikutano hiyo ili muweze kujirekebisha na kuboresha zaidi mikutano hii
ya Awamu ya Pili.
Ni matumaini yangu
kuwa wenzetu Waandishi wa Habari wataendelea kutoa Ushirikiano kwa Serikali
katika kutoa taarifa wakati wa mikutano hii.
Ndugu Washiriki ,
Mwisho niwatakie
maandalizi mema, mfanye kazi vizuri kwa kuhabarisha jamii yale yote
yanayofanywa na Serikali yetu. Wizara
itaendelea kushirikiana nanyi ili kufanikisha majukumu yetu sote.
Naomba sasa nitamke
kuwa mkutano wenu umefunguliwa rasmi. Nawatakia kila la heri na mafanikio
katika tathmini ya kazi kubwa mliyoifanya katika Awamu ya Kwanza ya kukutana na
waandishi wa Habari pamoja na kujibu maswali yote kwa usahihi na kwa kutumia
takwimu sahihi.
Ahsanteni.
No comments:
Post a Comment