Mkurugenzi Msaidizi Uzuiaji Ujangili kutoka Mfuko wa
Kuhifadhi Wanyamapori Tanzania, Paul Sarakikya akieleza kwa waandishi wa habari
kuhusu mipango ya Serikali katika kupambana na ujangili na mikakati ya kulinda
hifadhi za wanyama pori nchini, Katika mkutano uliofanyika leo, ukumbi wa Idara
ya Habari, jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya
Habari Bi. Zamaradi Kawawa. (Picha na Frank
Mvungi-MAELEZO)
1.0
UTANGULIZI
Mfuko wa Kuhifadhi Wanyamapori
Tanzania (Tanzania Wildlife Protection Fund, TWPF) ulianzishwa kwa Sheria ya
Bunge Na. 21 ya mwaka 1978 baada ya kukifanyia marekebisho kifungu cha 69 cha
Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori (Wildlife Conservation Act) Na. 12 ya mwaka
1974. Marekebisho hayo yalitangazwa kwenye Gazeti la Serikali Na. 21 la tarehe
22 Mei, 1981.
Baada ya kufanyika mapitio ya Sheria
ya Wanyamapori Na. 12 ya mwaka 1974, sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori ya sasa
Na. 5 ya mwaka 2009 (Sura ya 283) inabainisha uwepo wa Mfuko kisheria katika
kifungu cha 91(1). Lengo la kuwa na Mfuko ni kuiongezea Idara ya Wanyamapori
uwezo wa kifedha za kutekeleza majukumu yake ya ulinzi wa wanyamapori. Serikali
inatambua kuwa ulinzi wa wanyamapori unahitaji fedha nyingi na fedha kutoka
Hazina hazikidhi mahitaji yaliyopo.
2.0
MAJUKUMU YA MFUKO
Kwa mujibu wa Kifungu cha 91(2) cha
Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori Na. 5 ya Mwaka 2009, malengo ya Mfuko (TWPF) ni
kuwezesha na kusaidia shughuli wanyamapori ndani na nje ya maeneo
yaliyohifadhiwa hususani katika maeneo yafuatayo:-
(i)
Uzuiaji
ujangili na usimamizi wa sheria;
(ii)
Uendeshaji
wa Kikosi cha Ulinzi wa Wanyamapori;
(iii)
Uhifadhi
wa wanyamapori;
(iv)
Kusaidia
maendeleo ya jamii zinazozunguka maeneo yaliyohifadhiwa;
(v)
Utoaji
wa elimu, mafunzo na uhamasishaji kuhusu masuala ya wanyamapori;
3.0
USIMAMIZI WA MFUKO
3.1
Bodi ya Wadhamini ya Mfuko
Mfuko unasimamiwa na Bodi ya Wadhamini
(Board of Trustees) kwa mujibu wa kifungu cha 92 cha Sheria tajwa. Mwenyekiti
wa Bodi ya Wadhamini ya Mfuko anateuliwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano ya
Tanzania. Wajumbe wengine wa Bodi ambao huingia kutokana na nyadhifa zao ni
Mkurugenzi Mkuu wa Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka
za Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Uhifadhi wa
Wanyamapori Tanzania (TAWIRI), Mwakilishi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mwakilishi
wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori ambaye
ni Katibu wa Bodi. Aidha, Wajumbe wengine wawili wa Bodi huteuliwa na Mhe.
Waziri wa Maliasili na Utalii. Bodi husimamia Mfuko katika vipindi vya miaka
mitatu. Bodi iliyoko sasa ilianza kufanya kazi Juni 2011 na inatazamiwa
kumaliza kipindi chake ifikapo Juni 2014.
4.0
PROGRAMU ZILIZO CHINI YA MFUKO
Mfuko unagharamia uendeshaji wa
program mbili zinazohusika na utoaji wa elimu ya uhifadhi wa wanyamapori kwa
jamii ndani na nje ya nchi. Programu hizo ni “Malihai Clubs of Tanzania” na
Majarida ya Kakakuona na “Tanzania Wildlife”
4.1
Malihai Clubs of Tanzania (MCT)
“Malihai Clubs of Tanzania” ni
Programu ya Serikali chini ya Idara ya Wanyamapori inayoshughulika na utoaji wa
elimu ya Uhifadhi wa Maliasili na Mazingira katika Taasisi za Elimu (Shule za
Msingi, Kondari, Vyuo). Pia kwa mwanachama mmoja mmoja na makundi ya jamii hasa
wanavijiji wanaoishi pembezoni mwa mapori yaliyohifadhiwa. Kwa kupitia program
hii elimu ya uhifadhi kwa umma kwa vitendo katika Shule za Msingi, Sekondari,
Vyuo na Vijiji hususan vile vinavyopakana na maeneo yenye wanyamapori huenezwa.
Kwa sasa, MCT inaendesha shughuli zake
katika Kanda tatu ambazo ni:
a.
Kanda
ya Kaskazini – yenye makao yake makuu katika Jiji la Arusha
b.
Kanda
ya Ziwa – yenye makao yake makuu katika Jiji la Mwanza
c.
Kanda
ya Nyanda za Juu Kusini – yenye makao yake makuu Mbarali Mkoani Mbeya.
4.2
Majarida ya kutoa elimu ya uhifadhi na
kukuza Utalii
Mfuko unachapisha majarida mawili: Kakakuona ambalo ni la Kiswahili na Tanzania Wildlife (la Kiingereza).
Majarida haya ni nyenzo muhimu kwa kueneza elimu ya uhifadhi kwa umma wa
Tanzania na kutangaza utalii ndani na nje ya nchi. Pia, ni jukwaa la wataalam
mbalimbali wa uhifadhi wa Maliasili, mazingira, utalii wa ndani na nje ya nchi.
Pia, ni jukwaa la wataalam mbalimbali wa uhifadhi wa Maliasili, mazingira,
Utalii na utamaduni kubadilishana mawazo, kuelezea uzoefu na utalaam wao.
Majarida yote mawili huchapishwa mara nne kwa mwaka. Nakala 6,000 (nakala 3,000
za jarida la Kiswahili la Kakakuona na nakala 3,000 za jarida la Kiingereza la
Tanzania Wildlife) huchapishwa kila robo ya mwaka. Katika mwaka wa fedha
2012-2013, jumla ya nakala 24,000 za majarida zilizochapishwa na kusambazwa
katika vituo vya uuzaji ambavyo viko sehemu mbalimbali nchini katika ofisi za
Wizara ya Maliasili na Utalii, mahotelini, kwenye baadhi ya vituo vya Shirika
la Hifadhi za Taifa (TANAPA) na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.
5.0
VYANZO VYA MAPATO YA MFUKO
Kifungu Na. 91(3) cha Sheria ya
Kuhifadhi Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009, kimeainisha vyanzo vya mapato ya
Mfuko kama ifuatavyo:-
a.
Mapato
mbalimbali kama yatakavyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mnamo mwaka 1983, Serikali kupitia Hazina ilitoa ruzuku ya Shilingi 2,500,000/=
kama kianzio (seed money) cha Mfuko;
b.
Asilimia
25 ya mapato yatokanayo na mauzo ya wanyamapori na nyara au silaha, magari,
vyombo, ndege, mahema au kitu chochote kilichohusika katika kutenda kosa la
ujangili kama ilivyoainishwa katika kifungu cha 111 cha Sheria ya Kuhifadhi
Wanyamapori Na. 5 ya Mwaka 2009. Hiki ndicho chanzo kikuu cha mapato ya Mfuko;
c.
Zawadi
na michango mbalimbali ndani na nje ya nchi itakayotolewa na wahisani, taasisi,
Serikali, au mashirika ya kimataifa; na
d.
Kiasi
chochote au mali yoyote itakayotolewa kwa Mfuko kutokana na vyanzo vingine
ambavyo vitabuniwa na Mfuko.
6.0
MIRADI/VITEGA UCHUMI VYA KUIMARISHA
MFUKO
Ili kukidhi mahitaji ya kifedha ya
uhifadhi endapo vyanzo vya sasa vya mapato vitayumba, Mfuko umebuni miradi
mbalimbali kama vyanzo vya kuongeza na/au mbadala vya mapato (complimentary
and/or alternative sources of income). Miradi hiyo ni Jengo la Kakakuona
(Kakakuona House), Pori la Akiba Pande, Bustani ya Wanyamapori Tabora, Bustani
ya Wanyamapori ya Ruhila (Songea) na Kambi ya kitalii katika Pori la Akiba
Selous.
7.0
CHANGAMOTO ZA MFUKO
Katika kutekeleza majukumu yake, Mfuko
unakabiliwa na changamoto mbalimbali. Changamoto kubwa ni mbili kama ifuatavyo:
7.1 Kutokana na mabadiliko ya hali ya kijamii
na kiuchumi pamoja na kuwepo kwa teknolojia ya mawasiliano ya simu za mkononi
mahitaji ya fedha kwa ajili ya kukabiliana na wimbi la ujangili nchini na
makubwa ukilinganisha na miaka ya 80 na 90. Kutokana na hali hiyo Mfuko hauna
uwezo wa kukidhi mahitaji ya fedha kwa ajili ya kuzuia ujangili hususan fedha
za kununua vifaa vya doria (magari, radiocalls, mahema, sare), mafuta ya magari
na ndege pamoja na malipo ya posho ya kujikimu ya wahifadhi wanyamapori.
7.2
Chanzo
kikuu cha mapato cha Mfuko ni 25% ya mapato yatokanayo na biashara ya uwindaji
wa kitalii. Biashara ya uwindaji wa kitalii hutegemea wateja ambao ni matajiri
kutoka nchi za Ulaya na Marekani. Mtikisiko wowote wa kisiasa, kiamani au
kiuchumi unapotokea katika nchi ambazo watalii hao wanatoka huathiri hali ya
uwindaji nchini na hivyo mapato ya Mfuko huporomoka.
8.0
MIPANGO YA KUKABILIANA NA CHANGAMOTO
Hatua mbalimbali zinachukuliwa ili
kukabiliana na changamoto hizo ikiwa ni pamoja na;
8.1
Kutafuta
vyanzo vingine vya mapato zaidi ya biashara ya uwindaji wa kitalii. Miradi ya
maendeleo ya Mfuko imebuniwa ili kuiendeleza na kuwa vyanzo vya mapato ya
Mfuko. Miradi hiyo ni Ujenzi wa Jengo la Kakakuona, Pori la Akiba Pande,
Bustani ya Wanyamapori ya Tabora, Bustani ya Wanyamapori ya Ruhila (Songea) na
Kambi ya Utalii katika Pori la Akiba Selous Miradi hiyo iko katika hatua
mbalimbali za kuiendeleza.
8.2
Kuandaa
maandiko ya miradi kwa wahisani ili kupata fedha za kuimarisha uhifadhi wa
wanyamapori nchini.
No comments:
Post a Comment