Meneja wa Kituo cha Mabasi Ubungo, Juma Iddi (kushoto),
akifafanua jambo kwa waandishi wa habari juu ya ushiriki wao katika utoaji wa
huduma ya usafiri wa Mabasi yaendayo haraka(Dar Rapid Transit-DART) katika
mkutano na waandishi wa habari leo, Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Msemaji wa
Halmashauri hiyo, Gaston Makwembe. (Picha zote na Eliphace Marwa)
Msemaji wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Gaston
Makwembe (kushoto), akiwaeleza waandishi wa habari Mpango wa Halmashauri kujenga
vituo vya Mabasi yaendayo mikoani na nchi za jirani katika maeneo ya Mbezi Luis
na Boko Basihaya katika mkutano na waandishi wa habari leo, Jijini Dar es
Salaam. Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari, Zamaradi Kawawa.
HALMASHAURI ya Jiji la Dar es Salaam itajenga vituo vya mabasi
yaendayo mikoani na nchi za jirani katika maeneo ya Mbezi Luis na Boko Basihaya.
Ujenzi wa vituo hivyo ni utekelezaji wa mipango ya Jiji ya kuimarisha huduma za
usafiri Dar es Salaam. Kituo cha Mbezi Luis kitahudumia wasafiri wa Kanda ya Kati
na Nyanda za Juu wakati Kituo cha Boko Basihaya kitatoa huduma kwa wasafiri wa Kanda
ya Kaskazini. Kwa Kanda ya Kusini Halmashauri ya Jiji itajenga Kituo cha Mabasi
Kongowe.
Kituo kitakachoanza kujengwa ni Mbezi Luis ambacho
kitajengwa sambamba na Boko Basihaya. Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo kimepangwa
kutoa huduma ya usafiri wa mabasi yaendayo haraka kwa wasafiri wote watakaokuwa
wakitumia vituo hivyo vya mabasi yaendayo mikoani. Ujenzi wa vituo vya Mbezi
Luis na Boko Basihaya, kutokana na upembezi yakinifu wa awali, unakadiriwa kugharimu
kiasi cha shilingi bilioni 40 kwa kila kituo.
Ujenzi wa vituo hivyo unahitaji
upembuzi yakinifu wa kina kwa lengo la kupata gharama halisi za utekelezaji
wake, kubaini vyanzo vya fedha na kuangalia uwezekano wa kuzishirikisha taasisi
mbalimbali za fedha na wawekezaji wanaoonyesha nia ya kushirikiana na
Halmashauri ya Jiji katika ujenzi wa vituo hivyo ambavyo vitakapokamilika vitakuwa
pia ni chanzo cha ajira kwa wananchi.
Katika kipindi hiki cha
maandalizi ya ujenzi wa vituo hivyo, bado Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo (UBT) kitaendelea
kutoa huduma kwa wasafiri waendao mikoani na nchi za jirani. Halmashauri ya
Jiji inapenda wananchi wafahamu kwamba UBT, kama ilivyopangwa na Serikali,
itakuwa ni kituo kitakachotoa huduma ya usafiri wa Mabasi Yaendayo Haraka(Dar
Rapid Transit-DART) baada ya kukamilika kwa ujenzi wa miundombinu yake. Pamoja
na hilo Halmashauri ya Jiji pia itajenga “shopping malls” na hoteli katika
kituo hicho cha UBT
Kukamilika kwa ujenzi wa vituo
hivyo vya mabasi ni mafanikio makubwa katika jitihada za serikali za kuimarisha
huduma za usafiri katika Jiji la Dar es Salaam. Wadau wa maendeleo katika sekta
hii, wananchi na taasisi mbalimbali wanategemewa kuendelea kutoa mapendekezo
yao ya kuimarisha huduma za usafiri Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment