TANGAZO


Friday, August 23, 2013

CUF chatoa Maazimio ya Kikao cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa kilichofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 22 Agosti, 2013

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), akisoma maazimio ya Kikao cha Baraza Kuu la Uongozi kilichofanyika Agost 22, 2013, jijini Dar es Salaam, Makao Makuu ya chama hicho, Buguruni leo. Kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa CUF Taifa, Machano Khamis Ali. (Picha zote na Kassim Mbarouk-www.bayana.blogspot.com)
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), akisoma maazimio ya Kikao cha Baraza Kuu la Uongozi kilichofanyika Agost 22, 2013, jijini Dar es Salaam, Makao Makuu ya chama hicho, Buguruni leo. Katikati ni Makamu Mwenyekiti wa CUF Taifa, Machano Khamis Ali na kushoto ni Mwenyekiti wa Wilaya ya Ilala, Said Ricco.
Mwandishi wa ITV, Henry Mabumo, akiuliza swali kwa Mwenyeiti wa CUF Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba wakati alipokuwa akizungumza nao leo, wakati wa kusoma maazimio ya kikao cha Baraza Kuu la Uongozi Taifa.
Baadhi ya waandishi wakimsikiliza Mwenyekiti wa CUF Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba, wakati alipokuwa akisoma maazimisho ya Baraza Kuu jijini Dar es Salaam leo.
Baadhi ya wananchama wa Chama cha Wananchi (CUF), wakimsikiliza Mwenyekiti wao, Profesa Ibrahim Lipumba, wakati alipokuwa akisoma maazimio ya kikao cha Baraza Kuu la Uongozi jijini leo.
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, akisoma maazimio ya Kikao cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa, kilichofanyika Agost 22, 2013, jijini Dar es Salaam, Makao Makuu ya chama hicho, Buguruni leo. Kulia ni Naibu Mkurugenzi wa CUF Taifa, Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa chama hicho, Abdul Kambaya.
 
 
BARAZA Kuu la Uongozi Taifa la The Civic United Front (CUF- Chama Cha Wananchi) limekutana na kufanya kikao chake cha kawaida kwa mujibu wa katiba ya chama katika ukumbi wa Shaaban Mloo, Dar es salaam, tarehe 21-22 Agosti, 2013. Kikao kimeongozwa na Mwenyekiti wa Chama Taifa, Mhe. Prof Ibrahim Lipumba. Baraza Kuu la Uongozi la Taifa lilipokea, kuzijadili na kuzifanyia maamuzi ajenda mbalimbali zilizowasilishwa na Kamati ya Utendaji ya Taifa ikiwa ni pamoja na;
1.   Taarifa ya utekelezaji wa kazi za chama Mei-Julai, 2013.
2.   Taarifa ya utekelezaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.
3.   Taarifa ya utekelezaji wa kazi za wabunge na wajumbe wa baraza la wawakilishi kuanzia Januari-Julai,2013
4.   Taarifa ya kutekwa na kuteswa kwa viongozi wa CUF kulikofanywa JWTZ mkoani Mtwara.
5.   Program ya kuimarisha Chama Sept-Julai, 2013 na Uchaguzi wa ndani ya Chama.
6.   Hali ya kisiasa, kiuchumi na kijamii nchini, pamoja na masuala mengineyo yaliyojadiliwa na kufanyiwa maamuzi.

Baada ya mjadala wa kina kuhusiana na ajenda hizo, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa limefikia maazimio yafuatayo;

1.  Kuhusu Taarifa ya Kazi za Chama kwa Kipindi cha Mei-Julai, 2013;
 
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa limepokea taarifa ya kazi za Chama kwa kipindi cha mwezi Mei-Julai, 2013 na kuipongeza Kamati ya Utendaji Taifa kwa kazi iliyofanywa katika kipindi hicho. Kamati ya Utendaji Taifa imepongezwa kwa kufanikisha ushindi na kurejesha Jimbo la Chambani, mkoa wa kusini Pemba na Wadi ya Ng’omeni katika Jimbo la Mkoani, Wilaya ya Mkoani kwa kukipatia chama chetu ushindi wa kutosha. CUF inawashukuru wananchi wote wa Chambani na Wadi ya Ng’omeni na kuwaahidi utumishi wa dhati kwa maendeleo yao na Taifa kwa ujumla kupitia kwa wagombea wa chama waliochaguliwa.

Baraza Kuu la Uongozi la Taifa limeiagiza kamati ya utendaji ya Taifa kufanya utafiti wa kina juu ya matokeo yasiyoridhisha ya uchaguzi mdogo wa marudio wa Udiwani katika kata 26 uliofanyika nchini na kuleta mapendekezo ya utekelezaji katika kikao kijacho cha baraza kwa ajili ya kufanyiwa kazi.

2.  Taarifa ya Utekelezaji Kazi za Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.


Baraza kuu la uongozi la Taifa linawapongeza mawaziri na manaibu kwa kusimamia majukumu yao vizuri na kuweza kudhihirisha wazi kuwa CUF na viongozi wake wana uwezo mkubwa wa kuleta mabadiliko chanya ya maisha ya Wazanzibar. Baraza kuu la uongozi la Taifa linawaomba wanzanzibar wote kuiunga mkono CUF katika jitihada hizi za kuleta mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi kwa wananchi wote.

3.  Taarifa ya Utekelezaji wa kazi za Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuanzia Januari-Julai,2013

Baraza kuu limepokea taarifa ya utekelezaji wa kazi za wabunge na wajumbe wa baraza la wawakilishi kwa kipindi cha Januari-Julai, 2013. 
Linawapongeza kwa kazi nzuri ya kuzisimamia serikali zote mbili kikamilifu na kuweza kufichua ubadhilifu na ufisadi wa kutisha katika wizara mbalimbali.

Baraza kuu la uongozi la Taifa linawataka wabunge wa CUF, wazihoji Kamati za Bunge na Mkaguzi na Mdhibiti wa hesabu za Serikali ili zifanye upembuzi yakinifu na kutoa maelezo kwa Watanzania na hususani Wananchi wa Mtwara, kwamba fedha iliyotengwa kwenye bajeti ya mwaka 2010/2011, Shilingi 540 milioni ambazo zilikuwa ziende kwenye mradi wa “Mnazi Bay Gas and Electricity Development Project”, fedha hizo zimetumikaje wakati mradi wenyewe haupo, na hali mradi huo ulikuwa umeingizwa katika vitabu vya utekelezaji vya Serikali, wawaeleze Watanzania ni kwa sababu gani mradi huo wameufuta na fedha hizi zimekwenda wapi?
Aidha, limewataka wabunge kufuatilia taarifa ya ufisadi zilizofichuliwa na kamati ya hesabu za serikali kuu kiasi cha shilingi bilioni 247 za “commodity import support” ambazo hazijalipwa na kuhakikisha wahusika wanawajibishwa. Vilevile Bunge lichukue hatua za kuwawajibisha mawaziri waliolidanganya Bunge kuhusu miradi hewa ya barabara iliyotengewa shilingi bilioni 252.

4.  Hali ya amani, usalama wa Taifa na Haki za Binadamu Nchini;
 
a)  Kuhusu kuteswa na kudhalilishwa kwa Naibu Mkurugenzi wa Oganaizesheni, Uchaguzi na Bunge wa CUF (Mhe. Shaweji Mketo na wenzake)
Baraza kuu la uongozi la Taifa linalaani vitendo vya kikatili  ambavyo Jeshi la Ulinzi la Tanzania (JWTZ) limewafanyia viongozi wa CUF kwa kuwatesa na kuwadhalilisha huku jeshi la Polisi likiwabambikizia kesi zisizokuwepo ili kulinda ukatili wa JWTZ. Baraza Kuu linaamini kuwa, mateso haya ya wanajeshi na polisi kwa raia yanatokana na kauli ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliyoitamka Bungeni na kuvipa vyombo vya dola mamlaka ya “kupiga tu” kwani wakati Mhe. Mketo na wenzake wanateswa, askari hao wa JWTZ walieleza dhahiri  kuwa wamepewa ruhusa ya kupiga na kuua wakorofi wote watakoisumbua serikali, na kwamba hata wakiua hawatachukuliwa hatua zozote. Hatima ya utekelezaji wa Kauli ya waziri Mkuu unaendelea katika maeneo mbali mbali ya Nchi kama vile mkoa wa Mtwara, Kata ya Misima iliyoko wilaya ya Handeni(ambako wananchi wanateswa na kupigwa na wanajeshi wakilazimishwa kujiunga na Mafunzo ya Mgambo).

b) Madawa ya kulevya na Utoroshaji wa Nyara za Serikali.
Baraza kuu la uongozi la Taifa linasikitishwa na kukithiri kwa biashara ya madawa ya kulevya na biashara ya kutorosha nyara za serikali huku vyombo vya dola vikichukua hatua dhaifu kupambana na biashara hizo haramu.  Baraza Kuu linahoji ni kwa nini vyombo vya dola vinawekeza nguvu kubwa kuzima harakati na uhuru wa vyama vya siasa, waandishi wa habari, wanaharakati, viongozi wa dini na wananchi wasio na hatia? Baraza Kuu linao kwamba, nguvu hizo zingetumika kudhibiti ujambazi, biashara ya madawa ya kulevya, wizi wa rasilimali za nchi yetu, ubadhirifu serikalini na madhambi mengine, wananchi wa Tanzania wangekuwa na uchumi imara na wangejenga taifa lenyenguvu kubwa ya kidemokrasia na kiuchumia siku za mbeleni.

Baraza kuu la uongozi la Taifa linasikitishwa na udhaifu mkubwa kwa Jeshi la Polisi Kitengo cha Kuzuia Madawa ya Kulevya kilichopo uwanja wa ndege wa Dar es Salaam. Baraza Kuu linaona kuwa Waziri wa Uchukuzi Dr. Harison Mwakyembe (kwa nia nzuri) amejibebesha majukumu ya waziri wa mambo ya ndani(ambaye anaonekana kukwepa majukumu yake). Waziri wa uchukuzi ana majukumu mazito ya kusimamia reli, bandari, viwanja vya ndege, usafirishaji na uchukuzi kwa ujumla. Polisi na wizara ya mambo ya ndani viko wapi mpaka waziri wa uchukuzi ndiye aende kusimamia kukamatwa kwa wanaosafisrisha maawa ya kulevya na nyara za seikali? Na bila aibu, serikali inachukua hatua za kumsimamisha au kumfukuza kazi askari polisi mwenye cheo cha Koplo ati kwa kusaidia kupitisha madawa, bila kuzingatia ukweli kuwa Koplo huyo lazima alitumwa na msimamizi wake au vigogo wengine katika mamlaka za serikali.

Baraza kuu la uongozi la Taifa linamtaka waziri wa Mambo ya ndani asimamie majukumu yake, kama anawaogopa matajiri wanaofadhili mitandao ya dawa za kulevya na usafirishaji wa nyara za serikali ni bora ajiuzulu. Baraza Kuu linawataka mawaziri hawa na mamlaka zingine za serikali kushirikiana kuwachunguza na kuwachukulia hatua kali za kinidhamu viongozi wa vitengo vyote vya ulinzi na ukaguzi katika uwanja wa ndege wa JKIA na maeneo mengine ya usafiri ambako madawa ya kulevya hupitishwa na nyara za serikali hutoroshwa.

Baraza Kuu linaitaka serikali ya CCM ipambane na “mapapa wa utoroshaji wa nyara za serikali na madawa ya kulevya” badala ya kufanya “geresha” ya kupambana na “vidagaa” vya biashara hizi ambavyo hata vikichukuliwa hatua kali, wakubwa wa biashara wanaendelea kuliumiza taifa. Waziri anayejali maisha yake kuliko maisha ya vijana wanaoteketea kwa madawa aachie ngazi mara moja.

b)Kupigwa Risasi kwa Sheikh Ponda.
Baraza kuu la uongozi la Taifa linalaani kitendo cha kikatili cha kupigwa risasi Sheikh wa Kiislamu Issa Ponda. Sheikh huyu alipigwa risasi bila sababu, hakuwa anapambana na polisi wala hakuwa na silaha. Huu ni ukatili mkubwa na usiokubalika. Baraza Kuu linaitaka Serikali kuunda Tume Huru itakayochunguza suala hili kama zilivyoundwa tume huru nyingine kwenye matukio kadhaa ya uvunjwaji wa Haki za Binadamu.
Baraza Kuu linamtaka kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro Christopher Shilogile ajiuzulu kupisha uchunguzi wa tukio hili na kama hafanyi hivyo serikali imuwajibishe.

Baraza kuu la uongozi la Taifa limemtaka mwenyekiti wa chama taifa, Kamati ya Utendaji ya Taifa na viongozi wote wa chama nchi nzima, kusimama kidete kumtetea raia yeyote wa nchi hii haki zake zinapovunjwa bila kufungwa na itikadi za dini, siasa, kabila, rangi, uraia n.k. Baraza Kuu linataka haki za wananchi wote wa Tanzania ziheshimiwe bila kujali cheo wala kipato na vyombo vya dola vifanye kazi kwa kuhakikisha haki hizo za msingi hazidharauliwi wala kuvunjwa.

c)  Mahusiano ya Rwanda na Uganda Kiuchumi na Kiusalama

Baraza Kuu la Uongozi la Taifa limesikitishwa na kufedheheshwa na Mgogoro wa kiuchumi uliotangazwa na nchi majirani za Rwanda na Uganda, kuhusu kutotumia Bandari ya Dar es Salaam kwa sababu ya urasimu wa Mamlaka ya Bandari,ubabaishaji wa vyombo vya dola kama Jeshi la Polisi(maarufu kama “askari wa pikipiki” au “tigo”), askari wa usalama barabarani na miundombinu mibovu ya barabara zetu na miundombinu duni ya bandari zetu. Baraza Kuu linaitaka Serikali kulitazama jambo hili katika sura ya kiuchumi na si vyema kulitazama jambo hili katika mtazamo wa Kisiasa ili kuweza kuwa na mkakati wa kunusuru hali hii.

Baraza Kuu la Uongozi la Taifa pamoja na kuwa na Uzalendo mkubwa kwa Taifa letu, linatoa wito kwa Rais Kikwete kutafuta njia za Kidiplomasia ili kuweza kutatua Mgogoro wa Kisiasa baina ya Tanzania na Rwanda ili kuleta maelewano ambayo yatadumisha usalama baina ya nchi zetu. Hatuna njia ya kuchagua zaidi ya kumaliza kila mtafaruku kwa amani na kujenga maelewano.


d) Kuhusu Matukio Kadhaa ya Mauaji na Tume za Uchunguzi zilizoundwa kuchunguza Matukio hayo.
Baraza Kuu linaitaka serikali kutoa taarifa juu ya Ripoti za Uchunguzi zilizowasilishwa na Tume hizo ili Wananchi wapate kujua ukweli wa Matukio hayo na hatua zitazochukuliwa baada ya upatikanaji wa Taarifa hizo. Baadhi ya tume za uchunguzi ni pamoja na ile ya mauaji ya Padre Mushi, mwandishi Daudi Mwangosi, Kutekwa na kuteswa kwa kiongozi wa madaktari Daktari Mwangosi, kutekwa na kuteswa kwa mhariri mtendaji wa Habari Cooperation ndugu Absalom Kibanda na matukio mengine mengi ya kikatili yaliyoweka doa katika ulinzi wa haki za binadamu za raia wa Tanzania.

5.  Kuhusu Rasimu ya Katiba Mpya ya Jamuhuri wa Tanzania;

Baraza Kuu linaipongeza Tume ya Kuratibu na Kukusanya Maoni ya Katiba inayoongozwa na Jaji Warioba kwa kupokea Mapendekezo ya CUF-Chama cha Wananchi kwenye Mapendekezo ya Katiba Mpya. Mambo yaliyopendekezwa na CUF na ambayo tume ya mabadiliko ya katiba mpya imeyaweka kwenye rasimu ya katiba ni pamoja na suala la Serikali Tatu, mgombea binafsi, Rais kutangazwa akipata zaidi ya asilimia 50 ya kura zote zilizopigwa la sivyo uchaguzi urudiwe kwa wale wawili walioongoza kwa kura, tume huru ya uchaguzi, mawaziri kutokuwa wabunge, spika kutokuwa mbunge, haki za watu wenye ulemavu, kupanuliwa na kuimarishwa kwa haki za binadamu n.k.
Baraza Kuu linaitaka Tume ya Jaji Warioba kuhakikisha inakamilisha suala la andiko la Katiba Mpya na uundwaji wa Tume Huru ya Uchaguzi kama ilivyowaahidi watanzania.


6.  PROGRAM YA CHAMA SEPT-JULY,2013 NA UCHAGUZI WA NDANI YA CHAMA.

Baraza kuu limeiagiza kamati ya utendaji Taifa kuendelea na maandalizi ya uchaguzi wa ndani ya chama kwa kuhakikisha kuwa uchaguzi huo unaratibiwa vizuri ili kupata viongozi makini kwa ngazi zote watakaoweza kukipatia ushindi mkubwa chama chetu katika chaguzi zijazo.


MWISHO;
The Civic United Front (CUF-Chama Cha Wananchi) na viongozi wake inawahakikishia watanzania wote juu ya uwezo wake kwa kushirikiana na wananchi wote katika kuandaa sera mbadala za nchi yetu ya kutekeleza mabadiliko wanayoyataka watanzania kwa kuwa na AGENDA YA MAENDELEO KWA WOTE (AGENDA FOR INCLUSIVE DEVELOPMENT). Baraza Kuu la Uongozi la Taifa linatoa wito na kuwakaribisha watanzania wote katika Chama Cha Wananchi CUF, ili kwa pamoja tuweze kushirikiana kudai haki sawa kwa wote katika uchumi, mgawanyo wa rasilimali za nchi, huduma za kijamii, haki za msingi za binadamu na maendelea ya jumla na kuwaondolea watanzania umasikini, ujinga, maradhi na mgawanyo wa kinyonyaji katika rasimali na mali asili za Watanzania.

HAKI SAWA KWA WOTE.

 Imetolewa na;
Baraza Kuu La Uongozi Taifa,                                                                                               Ijumaa, 23 Agosti 2013,
Dar Es Salaam.

Mhe. PROF IBRAHIM H. LIPUMBA                                            MWENYEKITI WA CUF TAIFA.

No comments:

Post a Comment