Serikali ya Uingereza inanuia kupunguza kwa asilimia hamsini idadi ya vifo vinavyotokana na Malaria katika nchi kumi ambazo inasaidia ifikapo mwaka 2015.
Mawaziri wa Uingereza wanaonya kuwa vyandarua vinavyokinga dhidi ya Mbu na ambavyo Uingereza imenunua kwa ajili ya nchi hizi havitoshi katika harakati za kuangamiza Malaria.
Uingereza imeweza kununua vyandarua milioni 25, tangu mwaka 2010, lakini wakaguzi wa fedha nchini humo wanasema kuwa matumizi yake hususan kwa watoto wadodgo yanasikitisha, kwani havitumiki sana.
Wakaguzi hao wanataka Uingereza kushirikiana na watu wanapokea msaada huo ili kubadili maoni yao kuhusu matumizi ya vyandarua na umuhimu wake na pia kuhakikisha kuwa manufaa yanapatikana kwani pesa zimetumika kuvinunua vyandarua hivyo.
Mawaziri wamesema kuwa hatua ya matumizi ya vyandarua kuongezeka ni sehemu ya mpango unaolenga malengo mengi katika kuokoa maisha ya watu.
Hadi sasa hakuna chanjo dhidi ya Malaria na ugonjwa huo umesababisha vifo vya watu 660,000, mwaka jana na kuwaacha watu milioni 250 wakiwa wagonjwa sana.
Shirika la afya duniani limetahadharisha kuwa huenda ufadhili wa mipango ya kuangamiza Malaria ukapungua licha ya kuwa ugonjwa huo ni janga kubwa duniani na husababisha changamoto za kiuchumi kwa nchi zenye idadi kubwa ya watu wanaougua ugonjwa wenyewe.
Uingereza ilitumia pauni milioni 252 kati ya mwaka 2011-2012, katika nchi 18, kati ya hizi 16 zikiwa barani Afrika katika mpango wa kuangamiza Malaria.
Bajeti inatarajiwa kupanda hadi pauni milioni 494 kati ya mwaka 2014-2015, na kuifanya Uingereza kuwa mfadhili wa tatu kwa mkubwa kote duniani.
No comments:
Post a Comment