Maelfu ya watu wamekimbia makaazi yao nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo, baada ya waasi kutoka Uganda kushambulia mji mmoja wa Mpakani.
Kwa mujibu wa mashirika ya kutoa misaada wapiganaji wa Allied Democratic Forces ADF, walivamia mji wa Kamango siku ya Alhamisi na kuanza kupora mali.
Msemaji wa jeshi la Uganda, Luteni Kanali Paddy Ankunda amethibitisha tukio hilo.
Shirika la Msalaba Mwekundu limesema kuwa takriban watu elfu kumi na nane wamevuka mpaka na kuingia nchini Uganda.
Kundi hilo la waasi wa ADF, lina makao yake katika eneo lenye utajiri mkubwa wa madini Mashariki wa Congo, eneo ambalo makundi mengine ya waasi yamesababisha maafa makubwa katika kipindi cha miongo miwili iliyopita.
Msemaji huyo wa Jeshi Uganda Luteni Kanali Paddy Ankunda, ameliambia shirika la habari la AFP kuwa watu kadhaa waliuawa kwenye shambulio hilo.
Ripoti zinasema waasi hao waliwateka nyara watu kadhaa akiwemo chifu mmoja wakati walipokuwa wakaitoroka kutoka mji huo
Kundi la ADF liliundwa miaka ya tisini, katika eneo la Magharibi mwa Uganda, lililazimika kuvuka mpaka na kuingia nchi jirani baada ya kushambuliwa na jeshi la Serikali ya Uganda.
No comments:
Post a Comment