TANZANIA imenyakua Tuzo tatu za Ubunifu katika Utumishi wa Umma Barani Afrika. Tuzo hizo zimetolewa wakati wa Maadhimisho ya Nne ya Siku ya Utumishi wa Umma Barani Afrika jijini Accra leo.
Hafla ya utoaji wa Tuzo hizo imefanyika katika ukumbi wa Ikulu ya Ghana, jijini Accra ambapo Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, George Yambesi, akimwakilisha Waziri wa Nchi-Utumishi, Celina Kombani (MB), ambaye pia ni Mwenyekiti wa mpito wa Mkutano wa Mawaziri wa Utumishi Barani Afrika, alisema kuwa ni muhimu kwa watumishi wa Umma Barani Afrika kujikita katika ubunifu ili kuleta tija kwa tasisi na wateja wanaowahudumia.
Sherehe hizo, zimehudhuriwa na viongozi pamoja watumishi wa umma kutoka sekta mbalimbali barani Afrika.
Awali, Mkuu wa Watumishi wa Umma nchini Ghana, Prosper Douglas Kweku Bani, alisema mchango wa watumishi wa Umma Barani Afrika unatambuliwa lakini mwisho wa siku atakayetia jitihada zaidi katika kazi yake lazima atunzwe ingawa "wote ni bora na lengo ni moja", alisema.
Katika tuzo hizo, Tanzania imenga'arishwa na Taasisi za Wakala wa Vipimo (WMA), Nida na NAO.
Hapa chini ni baadhi ya matukio yaliyojiri katika Ikulu ya Ghana, wakati wa hafla hiyo ya utoaji Tuzo za Ubunifu katika picha.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma George Yambesi, akisoma hotuba yake katika Ikulu ya Ghana wakati wa utoaji Tuzo za Ubunifu kwa taasisi za Umma mbalimbali Barani Afrika.
Baadhi ya watumishi wa Umma kutoka Mataifa mbalimbali Barani Afrika, waliohudhuria hafla ya Utoaji Tuzo, wakiwa Ikulu ya Ghana-Accra, wakati wa utoaji wa tuzo hizo leo.
Kikundi cha akinamama kutoka Kusini mwa Ghana kikionesha umahiri wake katika kucheza ngoma za utamaduni kwa kutumia vibuyu vikubwa viliyokatwa katikati.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma George Yambesi (katikati ya waliobeba Tuzo) katika picha ya pamoja na wawakilishi wa Tanzania baada ya kujinyakulia Tuzo tatu za Ubunifu, siku ya Utoaji Tuzo katika Ikulu ya Ghana-Accra. (Picha zote na Florence Lawrence-PO PSM)

No comments:
Post a Comment