TANGAZO


Wednesday, June 26, 2013

Mkurugenzi Halmashauri ya Chilolo afariki dunia ghafla

Mohamed Gwalima, enzi za uhai wake (kulia), akijiandaa kumzawadia  Kompyuta aliyekuwa Katibu Tawala  wa Mkoa  wa Iringa, Gertrude Mpaka, wakati wa hafla ya kumuaga iliyofanyika ukumbi wa St. Dominic, mjini Iringa. Wa pili kulia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kilolo, Joseph Muhumba na Mkuu  wa Wilaya ya Kilolo, Gerald Guninita. (Picha na Francis Godwin Blog)
Mfanyabiashara maarufu, mkoani Iringa na kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Salim Abri Asas (wa pili kulia), akikabidhi msaada wa mifuko 200 ya saruji yenye thamani ya zaidi ya sh. milioni 3.2 kwa Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Gerald Guninita, hivi karibuni, ofisini kwake. Wanaoshuhudia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kilolo, Joseph Mhumba (kushoto) na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kilolo, ambaye sasa ni marehemu, Mohamed Gwalima.
Waombolezaji wakiwa wamelibeba jeneza lenye mwili wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Wilaya ya Kilolo, marehemu Mohamed Gwalima leo kwa ajili ya kusafirishwa kuelekea nyumbani kwao, Rufiji kwa mazishi. (Picha zote na Francis Godwin)


Na  Francis Godwin, Iringa
ALIYEKUWA  Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, mkoani Iringa, Mohamed Gwalima amefariki dunia ghafla nyumbani kwake Kilolo.

Akithibitisha kutokea kwa kifo cha Mkurugenzi huyo, Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Gerald Guninita ambaye yupo kikazi mjini Dodoma, amesema kuwa Mkurugenzi huyo, amefariki ghafla nyumbani kwake baada ya kuwasili kutoka safari jijini Dar es Salaam, usiku wa kuamkia leo.

Mkuu huyo wa Wilaya alisema kuwa alipigiwa  simu kujulishwa juu ya kifo cha Mkurugenzi huyo usiku huo.

" Ni kweli ndugu mwandishi, habari hizo ni za kweli kabisa nimepigiwa simu na Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kilolo juu ya kifo hicho cha Gwalima", alisema.
 
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, Joseph Muhumba alisema  kuwa kifo cha Mkurugenzi huyo, kimeacha pigo kubwa katika Halmashauri ya Kilolo.

Kwani alisema kabla ya kifo cha ghafla cha Mkurugenzi huyo, alikuwa naye jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kutafuta wahisani wa kusaidia kufufua kiwanda cha Chai Kidabaga ili kuwakomboa wananchi wa Wilaya hiyo.

Alisema kuwa mbali ya kuwa kifo hicho, kimetokea ghafla ila Mkurugenzi huyo kabla ya kifo chake alikuwa akilalamika kusumbuliwa na tatizo la Kisukari.

Muhumba alisema kuwa kifo cha Mkurugenzi huyo, kilitokea ghafla usiku wa kuamkia leo baada ya kurejea kutoka jijini Dar es Salaam, pia amewapa pole nyingi wananchi wa Kilolo kwa msiba huo mzito.
 
Wakati  huo  huo, waombolezaji walifika kuaga mwili wa Mkurugenzi huyo, walieleza kusikitishwa kwao na hatua ya kamati ya mazishi kushindwa kutoa nafasi kwa watumishi wa Halmashauri ya Kilolo na Halmashauri nyingine mkoani Iringa pamoja na wananchi kuaga mwili huo.
 
Mbali ya waombolezaji hao zaidi ya 500, kufika mapema zaidi katika viwanja vya chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa kwa ajili ya kuaga mwili huo, ila hali imekuwa tofauti baada ya kuwepo kwa ratiba zinazochanganya zaidi ya mbili.

Taarifa za awali zilizotolewa zilionyesha kuwa mwili huo, ungeagwa majira ya saa 4 asubuhi, ila baadhi ya watu waliofika muda huo kuaga, waliambiwa kuwa mwili huo, ungeagwa muda wa saa 7 mchana na baada ya kufika majira ya saa 7 mchana lilitolewa tangazo jingine na Kaimu Mkurugenzi kuwa taratibu za kuuandaa mwili zinaendelea na mara baada ya kuaga basi mwili huo utapelekwa msikitini .
 
Hata hivyo, hali haikuwa hivyo wananchi waliokuwa wamejiandaa kwa ajili ya kuaga mwili huo, walijikuta wakiduwaa baada ya mwili huo kutolewa chumba cha maiti na kupakiwa katika gari kisha kupelekwa msikitini na baada ya msikitini mwili huo, uliingizwa katika gari jingine la wagonjwa na kuondoka kuelekea kijiji cha Ikwiriri, Rufiji kwa mazishi yatakayo fanyika kesho.

Baadhi ya watumishi waliofika kuaga mwili huo wameonyesha kusikitishwa na hatua ya kutouaga mwili wa Mkurugenzi wao.

Marehemu Gwalima, alizaliwa tarehe 16 februari 1957, Ikwiriri, Rufiji na kupata elimu ya Sekondari kutoka kidato cha kwanza mpaka cha nne katika Shule ya Sekondari Same, kuanzia mwaka 1978-1980 alipata elimu ya Kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari Shinyanga.

Mwaka 1980 mpaka 1981, alitumikia Taifa katika Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), kabla ya kujiunga na masomo ya shahada ya uchumi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), akichukua stashahada aliyotunukiwa mwaka 1986.
 
Mara baada ya kutunukiwa shahada ya uchumi, mwaka 1986, aliajiriwa kama mchumi katika Halimashauri ya Wilaya ya Mtwara.

Alitumikia Taifa katika maeneo mbalimbali kama mchumi mpaka mwaka 2007, alipoteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halimashauri ya Wilaya ya Mbulu.

Mwaka 2012, alihamishiwa katika Halimashauri ya Wilaya ya Mtwara na mwaka huu 2013, alihamishiwa katika Halimashauri ya Wilaya ya Kilolo, ambako amekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halimashauri hiyo, mpaka mauti yalipo mfika tarehe jana, 25/06/2013,  saa 1:15 jioni katika nyumba aliyokuwa anaishi na familia yake, ilyopo karibu na Ofisi za Halimashauri hiyo.

MWENYEZI MUNGU AILAZE ROHO YAKE MAHALI PEMA PEPONI, AMIN.

No comments:

Post a Comment