Bingwa wa michezo ya olimpiki kutoka nchini Morocco, anayedai kuwa wanawe, waliibwa na mawakala wa Norway , amekamatwa nchini Ufaransa.
Khalid Skah, aliyeshinda mbio za mita 10,000, michezo ya Olimpik ya Barcelona 1992, alizuiliwa katika uwanja wa ndege wa Orly mjini Paris, baada ya kusakwa na maafisa wa Norway kwa kosa la kuwaiba wanawe.
Kwa miaka mingi, amekuwa akilumbana na mkewe raia wa Norway mahakamani kuhusu nani anayepaswa kuwalea wanao.
Kesi hii imesababisha mzozo wa kidiplomasia baada ya Norway kukubali kuwa ilihusika na mpango wa kuwahamisha watoto hao kutoka Morocco.
Bwana Skah alithibitisha kukamatwa kwake kupitia mtandao wa kijamii.
Wakili wake wa Norway, Brynjar Meling, anasema kuwa bwana Skah ameomba atibiwe lakini yuko tayari kusafiri kwenda Norway kuweza kujieleza kwa maafisa wa nchi hiyo.
Bwana Skah, amekuwa akiwashtumu maafisa katika ubalozi wa Norway nchini Morocco, kwa 'kuwateka nyara' wanawe na kumsaidia mkewe Anne Cecilie Hopstock, kuwachukua kinyume na sheria.
Aidha Hopstock alikwenda Morocco na familia yake mwaka 2006, lakini akarejea mnamo mwaka 2007 baada ya uhusiano wake na mumewe Skah kuvunjika.
Watoto hao, Tarik na Selma, walisalia Morocco, lakini wakatoweka nyumbani kwao mwaka 2009 na mnamo mwaka 2010 walioenekana kwa mara nyingine katika televisheni ya Norway.
Vijana hao walisimulia walivyotoroka nyumbani kwao baada ya babao kuwa mkali kiasi cha kuwafungia ndani ya vyumba vyao.
Waliwasiliana na mama yao ambaye naye aliwasiliana na ubalozi wa Norway mjini Rabat kutaka usaidizi.
Maafisa katika ubalozi huo walifanya mipango ya kuwachukua watoto hao kutoka barabarani na kuwapa hifadhi katika makao ya ubalozi ambako walisalia hadi waliposafirishwa kwenda uhispania kwa ndege.
"Sisi wenyewe ndio tulitaka kutoroka," alisema Tarik.
Selma aliongeza kusema: "hatukuruhisiwa kuishi maisha ya kawaida wala hatukuruhusiwa kwenda shuleni."
Norway ilikubali kuwa mmoja wa maafisa wake aliwasaidia watoto wake akishirikiana na afisaa mmoja wa kikosi maalum aliyewasafirisha watoto hao kutoka Morocco.
Serikali ya Morocco imewatuhumu maafisa wa Norway kwa kukiuka mkataba wa Vienna kuhusu maswala ya kidiplmoasia na kutaka washtakiwe.
Bwana Skah na Bi Hopstock wote wameruhusiwa kuwalea wanao kila mmoja nchini Kwake ingawa sasa wanasemekana kuwa watu wazima wanaoweza kufanyia maamuzi
No comments:
Post a Comment