Mkurugenzi wa Hospitali ya IMTU, Dk. Ali Mzige, akizungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam leo, kuhusu kuwapima watoto afya zao, Jumapili ijayo.
Mkurugenzi wa Hospitali ya IMTU, Dk. Ali Mzige, akisisitiza jambo wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam leo, kuhusu kuwapima watoto afya zao, Jumapili ijayo.
Na Genofeva Matemu - MAELEZO
HOSPITALI ya Chuo Kikuu
cha Kimataifa cha Tiba na Teknolojia (IMTU Hospital) kwa kushirikiana na Umoja
wa Jamii ya watu kutoka India, Bengali waliopo nchini Tanzania, watatoa huduma ya
upimaji afya bure Jumapili, Mei 26 mwaka huu kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano wanaoishi maeneo
ya Mbezi Beach .
Hayo yamesemwa na
Mkurugenzi wa Hospitali ya IMTU, Dk. Ali Mzige alipokua akizungumza na
waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusiana na afya ya mtoto na umuhimu
wa maziwa ya mama hasa kwa watoto walio chini ya miezi 6 .
Dkt. Mzige amesema
wanakusudia kupima uzito, presha na kutazama afya ya kinywa kwa watoto wenye
umri chini ya miaka mitano ambapo watatumia vifaa maalumu vya upimaji presha
kwa watoto hao.
“Tutapima uzito ambao
takwimu zake ni Kg 10 kwa mtoto wa mwaka mmoja, Kg 11 kwa mtoto wa mwaka mmoja
na nusu, Kg 12 mtoto wa miaka 2, Kg 13 kwa mtoto wa miaka miwili na nusu, Kg 14
kwa mtoto wa miaka 3, Kg 15 kwa mtoto wa miaka mitatu na nusu, Kg 16 mtoto wa
miaka 4, Kg 17 mtoto wa miaka minne na nusu, na Kg 18 ni kwa mtoto wa miaka
mitano”, amesema Dkt. Mzige.
Akirejea matokeo ya
sensa ya mwaka 2012 Dkt. Mzige amesema matokeo hayo yalionesha kuwa asilimia 42
ya watoto chini ya miaka mitano hapa nchini wamedumaa, ambapo asilimia 16 wana
uzito pungufu (Underweight) na asilimia 5 wamekonda (Marasmic) wako kwenye
rangi nyekundu ya kadi za watoto za kliniki.
Aidha Dkt. Mzige
ameishauri jamii kula lishe bora na kamili sababu lishe bora huanzia nyumbani
hivyo ni jukumu la jamii kupata elimu ya chakula bora na mlo kamili wenye kujenga afya bora kwa
watoto.
Zoezi la upimaji wa afya
kwa watoto limeanza rasmi mwaka huu na linatarajiwa kufanyika kila mwaka au
mara mbili kwa mwaka kwa kushirikiana na uhisani wa Bango Sangho jamii ya
wahindi wanaoishi hapa nchini ambao wamekua wakitoa vifaa vya kupimia afya za watoto.



No comments:
Post a Comment