TANGAZO


Friday, May 24, 2013

Rais wa Zanzibar, Dk. Shein amjulia hali Sheha aliyemwagiwa tindi kali

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, akimuangalia Sheha wa Shehia ya  Tomondo, Wilaya ya Magharibi Unguja, Mohamed Saidi Kidevu (kulia), jinsi alivyoathirika na Tindikali aliyomwagiwa na mtu asiyejuilikana, huko Tomondo jana, wakati alipokuwa akirudi kuchota maji na kuelekea nyumbani kwake. Sheha huyo, yupo katika Hospitali ya Mnazi mmoja kwa matibabu. Kushoto ni Dk. Slim Mohamed Mgeni. (Picha zote na Ramadhan Othman, Ikulu Zaanzibar)

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, akipata maelezo kutoka kwa Sheha wa Shehia  ya Tomondo, Wilaya ya Magharibi Unguja, Mohamed Saidi Kidevu, aliyemwagiwa Tindikali na mtu asiyejulikana,  huko Tomondo jana, wakati alipokuwa akirudi kuchota maji na kuelekea nyumbani kwake. Sheha huyo, yupo katika Hospitali ya Mnazi mmoja kwa matibabu. Wa pili kulia ni Kaka yake Sheha, Sudu Mgeni Saidi.
 

Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar 
  
RAIS wa  Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein leo alifika hospitali ya Mnazi Mmoja  mjini Zanzibar kwa ajili ya kumjuulia hali  Sheha wa Shehia ya Tomondo mjni Zanzibar, Bwana Mohammed Said Kidevu aliemwagiwa tindikali na watu wasiojulikana.

Bwana Mohammed Said Kidevu alimwagiwa tindikali na watu wasiojulikana  usiku wa kuamkia juzi huko karibu na nyumbani kwake, mtaa ya Tomondo mjini Unguja na kupata majeraha makali katika sehemu za kichwani, shingoni, kifuani na jicho moja la upande wa kulia.

Kwa maelezo ya Dk.Slim Mohammed Mgeni, alimueleza Dk. Shein kuwa Bwana Mohammed anaendelea vizuri na hali yake inaendelea kuwa nzuri kwa mashirikiano na madaktari wakiwemo madaktari wa macho.

Dk. Slim alisema kuwa kutokana na hali yake kuendelea kuwa nzuri na kuendelea kupata matibabu mazuri bado hawajaamua kumsafirisha kwenda Hospitali Kuu ya Muhimbili Dar-es-Salaam.

Kwa maelezo ya Dk. Slim alisema kuwa hali ya Sheha huyo inaridhisha na juhudi zinaendelea kuchukuliwa katika kuhakikisha anaendelea kupata huduma nzuri za tiba.

Nae Dk. Shein  kwa upande wake alimuombea kwa Mwenyezi Mungu Sheha huyo kupona kwa haraka huku akilaani kitendo hicho ambacho si cha kiungwana na kueleza kuwa vyombo vinavyohusika vitaendelea na kazi zake za kuhakikisha wale wote waliohusika na kadhia hiyo  wanapatikanwa na kufikishwa mbele ya sheria.

Akitoa maelezo yake  Sheha huyo ambae anaendelea na matibabu katika hospitali hiyo ya MnaziMmoja, alimueleza Dk. Shein kadhia hiyo iliyompata wakati wa usiku akiwa anarudi kuchota maji na ndipo akamuona mtua aliyekuwa akija mbele yake na kudhani kuwa ana jambo anataka kumueleza ama anataka kuomba msaada kwa Sheha huyo.

Alieleza kuwa kwa vile yeye ni kiongozi wa Shehia hiyo na pia, ndie kiongozi wa eneo hilo aliona haja ya kusimama na kumsikiliza mtu huyo ambaye kwa hafla alimwagia tindikali na kukimbia.

Tukio kama hilo liliwahi kutokea hivi karibuni kwa kumwagiwa tindikali Katibu wa Mufti wa Zanzibar Sheikh Fadhil Soraga ambapo pia, aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Mji wa Zanzibar Rashid Juma nae alikumbwa na kadhia hiyo.

No comments:

Post a Comment