TANGAZO


Wednesday, April 10, 2013

Waajiriwa wapya Nishati na Madini waaswa kutetea maslahi ya jamii


Katibu Mkuu wa Nishati na Madini, Eliakimu Maswi akizungumza na waajiriwa wapya katika darasa watakaloendeshea mafunzo yaliyoandaliwa, ili kuwapa uelewa juu ya utendaji kazi katika utumishi wa umma juzi.



Katibu Mkuu wa Nishati na Madini, Eliakim Maswi (wa pili toka kushoto), akiwa katika picha ya pamoja na waajiriwa wapya baada ya ufungunzi wa mafunzo yao, yatakayochukua siku kumi katika Chuo cha Utumishi wa Umma. Kushoto kwake ni Mkurugenzi wa Utawala na Utumishi, Mrimia Mchomvu. (Picha zote na Habari na Nuru Mwasampeta, Wizara ya Nishati na Madini)

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Bwana Eliakim Maswi amewaasa waajiriwa wapya wa wizara yake kuutumikia umma wa watanzania kwa bidii na bila ubaguzi.

Aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, wakati akifungua mafunzo kwa waajiriwa hao yaliyoandaliwa kwa ajili yao ikiwa ni utaratibu wa kawaida wa Wizara ili kuwapa uelewa wa uendeshwaji wa shughuli za serikali.

Akifafanua zaidi, Katibu Mkuu Maswi aliwashauri waajiriwa wapya kutoa huduma bora kwa watanzania, na kuongeza kwamba anahitaji watu wanaotetea maslahi ya umma na kutumikia serikali na wananchi kwa juhudi.

Aidha, alieleza kuwa sifa kuu ya watumishi wa umma ni kutoa huduma bila upendeleo, kufanya kazi kwa uadilifu, kuheshimu matumizi sahihi ya taarifa na kuwajibika kwa umma wa Watanzania.

“Popote mtakapokuwa, mkifanya kazi kwa bidii mtaipa sifa Wizara yetu lakini pia serikali iliyoko madarakani.  Ni kwa sababu hiyo, mnatakiwa mpende kazi zenu na mzitekeleze kwa bidii’’, alisisitiza.

Alibainisha kuwa Serikali zote duniani zinaendeshwa kwa juhudi katika kazi na kusema Tanzania siyo nchi maskini bali inasumbuliwa na tabia ya uvivu wa kazi kwa baadhi ya Watanzania wakiwemo baadhi ya watumishi wa umma.

Katika mafunzo hayo ya wiki moja, washiriki watapata fursa ya kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu utumishi wa umma ikiwa ni pamoja na muundo wa serikali, uendeshaji wa serikali, maadili ya utendaji kazi, maboresho katika utumishi wa umma, mifumo ya uongozi, na uendeshaji wa ofisi.


Pia, watajifunza kuhusu virusi na ugojwa wa ukimwi, jambo ambalo Katibu Mkuu Maswi aliwasisitiza kuzingatia na kutochezea maisha yao kwa kujiingiza kwenye mahusiano na watu wasiowafamu.  


No comments:

Post a Comment