TANGAZO


Thursday, April 18, 2013

Rais wa Zanzibar, Dk. Shein azitaka Wizara kutimiza majukumu yake

Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein
Said Ameir, Ikulu Zanzibar 
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesisitiza wito wake wa kuzitaka Wizara kuimarisha idara za Mipango, Sera na Utafiti ili ziweze kutimiza majukumu yake ipasavyo.

Amesema idara hizo kadri inavyowezekana zijengewe uwezo wa kibajeti na kitaaluma kwa kuwa majukumu yake ndio mhimili wa kila Wizara.

Rais amesema hayo jana kwa nyakati tofauti wakati alipokuwa akihitimisha vikao vya tathmini vya Mipango Kazi ya Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais kwa kipindi cha Julai 2012 na Machi 2013.

Katika majumuisho ya vikao hivyo Rais awapongeza Makamu wa Kwanza wa Rais Mheshimiwa Seif Shariff Hamad na Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi kwa kuziongoza vyema Ofisi zao na hatimae kupata mafanikio makubwa katika utekelezaji wa majukumu ya Ofisi hizo katika kipindi hicho.

Awali akiwasilisha taarifa ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Waziri wa Nchi wa Ofisi hiyo Mohamed Aboud   Mohamed alieleza kuwa mitambo mipya ya kisasa ya kiwanda cha upigaji chapa cha Serikali inatarajiwa kuwasili nchini mwishoni mwa mwezi Aprili mwaka huu.

Alieleza kuwa kuwasili kwa mitambo hiyo ambayo itafungwa katika eneo la Maruhubi nje kidogo ya mji wa Zanzibar kutaimarisha shughuli za upigaji chapa ambapo mbali ya kutumia tekinolojia ya kisasa ya dijitali lakini uendeshaji wa kiwanda hicho utakuwa wa kibiashara ili kiweze kujiendesha chenyewe.

Waziri Aboud aliongeza kuwa katika kukabiliana na maafa nchini pamoja na kuendelea kutoa elimu ya kukabiliana na maafa kwa jamii Ofisi yake imeandaa Mpango wa kukabiliana na Maafa pamoja na Mkakati wa Mawasiliano wa Maafa ambao umesambazwa kwa wadau.

Wakati huo huo imeelezwa kuwa utatuzi wa masuala ya kijamii yakiwemo masuala ya uchafuzi wa mazingira, ugonjwa wa UKIMWI, matumizi ya madawa ya kulevya na watu wenye ulemavu ni miongoni mwa mambo yanayopewa kipaumbele na Serikali ya Awamu ya Saba.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Fatma Abdulwahid Fereji amesema hayo wakati alipokuwa akiwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa MpangoKazi wa Wizara yake wakati wa kikao cha tathmini kilichofanyika jana.

Kutokana na jitihada zinazofanywa na Serikali katika kushughulikia masuala hayo ya kijamii wananchi wamekuwa na mwitikio mzuri kwa Serikali yao.

Waziri alikieleza kikao hicho kuwa uvunaji bila utaratibu wa maliasili zisizorejesheka, uingizaji wa bidhaa chakavu uliokithiri na  miradi kuanzishwa bila ya kufanyiwa tathmini ya athari za kimazingira na athari za mabadiliko ya tabianchi ni miongoni mwa changamoto zinazoikabili Wizara yake katika kushughulikia masuala ya mazingira nchini.

Waziri Fereji aliezieleza changamoto nyingine kuwa ni uingizaji na matumizi ya madawa ya kulevya, udhalilishaji wa watu wenye ulemavu na kupungua kwa fedha za wahisani katika kuendesha miradi ya kupambana na ugonjwa wa UKIMWI.

Alieleza matumaini yake kuwa kutokana na jitihada za Serikali na kwa ushirikiano na wadau wengine Zanzibar itaweza kupambana na  changamoto hizo na hatimae kushinda.
     

No comments:

Post a Comment