TANGAZO


Saturday, April 20, 2013

Rais Dk. Shein azitaka Mamlaka za Mikoa na Mitaa kushirikiana na vyombo vya ulinzi kukomesha wizi wa mazao na mifugo Zanzibar, akutana na Uongozi wa Wizara ya Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein (katikati), akizungumza na Uongozi wa Wizara ya Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto katika utekelezaji wa kazi za Wizara hiyo, ukumbi wa mikutano wa Ikulu, mjini Zanzibar leo asubuhi. (Picha zote na Ramadhan Othman, Ikulu)

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na Uongozi wa Wizara ya Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto (hawapo pichani), katika utekelezaji wa kazi za wizara hiyo, ukumbi wa mikutano wa Ikulu, mjini Zanzibar leo asubuhi.

Baadhi ya Watendaji na Maofisa wa Wizara ya Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto, wakiwa kwenye mkutano na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein (hayupo pichani), katika utekelezaji wa kazi za wizara hiyo, ukumbi wa mikutano wa Ikulu, mjini Zanzibar leo asubuhi.


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed
 Shein amezitaka Mamlaka za Mikoa na Serikali za Mitaa kushirikiana na vyombo vya Ulinzi na Usalama kudhibiti wimbi la wizi wa mazao na mifugo lililoshika kasi Zanzibar hivi sasa.


Dk. Shein amesema suala hilo lazima lishughuklikiwe vizuri na kwa
 umakini mkubwa kwa sababu hatua iliyofikiwa sasa na vitendo vya baadhi ya wezi kukata sehemu za viungo vya mifugo kama ng’ombe na kuwaacha wazima sio tu kuwa ni ukatili lakini ni  vitendo ambavyo haviwezi kufikiriwa kufanywa Zanzibar.


Rais ametoa wito huo wakati akihitimisha majadiliano ya Mkutano wa
 Tathmini ya Taarifa ya Utekelezaji Mpangokazi wa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Idara ya Uratibu Mamlaka za Mikoa na Serikali za Mitaa uliofanyika jana Ikulu.


“Ni vitendo vibaya na vya kikatili kukata baadhi ya viungo vya mnyama
 bila kuchinjwa huku ukimwacha akihangaika kwa maumivu. Lazima tuwe makini na hatua za kuchukua kwa kuwa wanaofanya vitendo hivi  si watu wa kawaida” alisema Rais na kueleza hofu yake kuwa nyama hiyo huishia
kuuzwa kwa matumizi mbalimbali ya wananchi kitendo ambacho kinaingilia
 hata imani ya dini.


Sambamba na agizo hilo Dk. Shein amewakumbusha viongozi na watendaji
 wa mamlaka hizo kuelewa kuwa mamlaka hizo ndizo zilizo karibu na jamii na ndizo zinazoshughulikia masuala ya wananchi hivyo kila wakati wawe tayari kupokea na kutafuta njia za kukabiliana na changamoto mbalimbali kutoka kwa wananchi hao.


“Huko mliko ndiko kwenye wananchi… sisi wote humu (kikaoni) tunaishi
 katika maeneo ya mamlaka zenu hivyo hoja zitakuja, malalamiko yatakuja na hata pongezi wakati mwingine wananchi watakujanazo zote tuzipokee,” Dk. Shein alisisitiza.


Aliwasisitizia washiriki wa mkutano huo wakiwemo wakuu wa Mikoa na
 Wilaya, Makatibu Tawala wa Mikoa na Wilaya pamoja na Watendaji wa Manispaa, Mabaraza ya Miji na Halmashauri kuwa ni wajibu wao kujibu hoja za wananchi kwa kadri wanavyozielewa na kwa kufuata Sheria na
taratibu zinazowaongoza.

Rais alieleza kuridhishwa kwake na mwelekeo mzuri wa ukusanyaji mapato katika Mamlaka za Mikoa na Serikali za Mitaa na kuzitaka ziongeze jitihada zaidi ili zifikie hatua nzuri ya kupunguza utegemezi wa ruzuku na hatimae ziweze kujitegemea.

“Tuongeze kasi ya utekelezaji majukumu yetu kwa kuongeza  kasi ya
 ushirikiano, kasi ya mashauriano na kupunguza kasi ya kulaumiana na tukubali tujisahihisha pale tunapokosolewa”aliwasisitizia viongozi na watendaji mamlaka hizo.

Wakati huo huo Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharriff Hamad ametoa wito kwa watendaji wa Mamlaka za Mikoa na Serikali za Mitaa kuhakikisha wanakuwa makini katika matumizi ya fedha za makusanyo katika mamlaka zao.
Akichangia katika mjadala huo Maalim Seif amesema mwelekeo mzuri wa makusanyo ya fedha katika mamlaka hizo ni ishara ya mwitikio mzuri wa wananchi kulipa kodi mbalimbali hivyo matokeo mazuri ya matumizi ya fedha hizo katika utoaji huduma yatakuwa kichocheo zaidi kwao
kuendelea kulipa kodi kama itakiwavyo.


“Nimetiwa moyo na hatua ya ukusanyaji mapato katika Manispaa, Mabaraza
 ya Miji na Halmashauri hivyo lazima watendaji wawe makini katika matumizi ya fedha hizo kwani mapato yanapokuwa mazuri wananchi wanatarajia huduma nzuri kutokana ma matumizi ya fedha zao” alieleza
Maalim Seif.


Makamu wa Kwanza wa Rais alizungumzia pia kuhusu vitendo vya wizi wa
 mazao vinavyoendelea hivi sasa Unguja na Pemba na kueleza kuwa vitendo hivyo vikiendelea vinavyoweza kuwavunja moyo wakulima hivyo alizitaka
Mamlaka za Mikoa na Serikali za Mitaa ziongeze jitihada za kukabiliana
 nazo.

No comments:

Post a Comment