TANGAZO


Thursday, April 11, 2013

Rais Dk. Shein aonana na uongozi wa Wizara ya Ardhi, Maji, Makazi na Nishati Ikulu mjini Zanzibar leo

Baadhi ya Watendaji na Maofisa wa Idara mbalimbali za Wizara ya Ardhi, Maji, Makaazi na Nishati, wakiwa katika ukumbi wa mikutano, Ikulu mjini Zanzibar leo, katika kikao cha uongozi wa wizara hiyo, kilichoongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, ikiwa ni katika mpangilio wa Rais, kuzungumzia utekelezaji wa kazi za kila wizara. (Picha na Ramadhan Othman, Ikulu)


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza Mapinduzi,  Dk. Ali Mohamed Shein, akiingia katika ukumbi wa Mikutano wa Ikulu mjini Zanzibar leo, katika kikao na uongozi wa Wizara  ya Ardhi, Maji, Makazi na Nishati, ikiwa ni katika mpangilio wa Rais, kuzungumzia utekelezaji wa kazi za kila wizara.



Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na uongozi wa Wizara  ya Ardhi, Maji, Makaazi na Nishati, katika utekelezaji wa kazi za wizara hiyo, ukumbi wa mikutano wa Ikulu, mjini Zanzibar leo. Kushoto ni Makamo wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad.


Na Rajab Mkasaba, Said Ameir, Ikulu Zanzibar.  

WIZARA ya Kazi, Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika, imeeleza malengo yake ya kuimarisha mazingira yatakayosaidia kupunguza kiwango cha umasikini miongoni mwa wananchi, kwa kusimamia ipasavyo utekelezaji wa sheria za kazi na kushajiisha upatikanaji wa ajira hasa kwa vijana.

Uongozi wa Wizara hiyo, ulieleza hayo katika mkutano wa kuangalia utekelezaji wa mpango kazi kwa kipindi cha Julai 2012 hadi Machi 2013, Ikulu mjini Zanzibar.

Mkutano huo uliofanyika Ikulu mjini Zanzibar chini ya Mwenyekiti wake Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein pia, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd alishiriki pamoja na na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee.

Uongozi huo, chini ya Waziri wake Mhe. Haroun Ali Suleiman akitoa muktasari wa mpango kazi wa Wizara hiyo alisema kuwa mbali ya juhudi hizo za kupanua soko la ajira pia, Wizara inaimarisha program za kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia mikakati mbali mbali iliyoandaliwa, ikiwemo kutoa mafunzo kwa wajasiriamali.

Pamoja na  kutoa mikopo kwa ajili ya kuanzisha au kuendeleza shughuli za kiuchumi na kuimarisha vyama vya ushirika.

Aidha, uongozi huo ulieleza mafanikio yaliyoanza kupatikana kutokana na kuwepo soko la uhakika kwa wakulima wa mboga mboga kwa upande wa Unguja na Pemba.

Nae Dk. Shein kwa upande wake alitoa pongezi kwa Wizara hiyo kutokana na juhudi inazozichukua katika kuhakikisha kuhakikisha suala la ajira linapewa kipaumbele na kufanyiwa kazi hasa kwa vijana huku akisisitiza vijana kutochagua kazi.

Pamoja na hayo, alitoa shukurani kwa juhudi kubwa zinazochukuliwa na wajasiriamali huku akiwasisitiza kuendelea na shughuli zao za kutengeneza vifaa mbali mbali kwa lengo la matumizi ya wananchi hapa nchini.


Wakati huo huo, Dk. Shein amekutana na uongozi wa Wizara ya Ardhi, Mkaazi, Maji na Nishati na kuitaka Wizara hiyo kujipanga vyema katika kutekeleza zoezi la kuzitambua na kuzisajili mali za Serikali.

“ni jukumu kubwa kwa sababu mali hizo ni nyingi na ziko maeneo mbalimbali mijini na mashamba ambazo ni nyumba za kuishi, majengo ya ofisi na taasisi kama skuli pamoja na mashamba” alieleza
Alisisitiza kuwa zoezi hili lifanyike kwa makini na kwa kupanga vipaumbele kutokana ukweli kuwa kila likichelewa baadhi ya maeneo hasa ya skuli yanazidi kuvamiwa.

Kuhusu huduma ya maji nchini Dk. Shein ameiagiza Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) kuongeza kasi ya kuelimisha wananchi kuhusu hali halisi ya tatizo la maji ili kupunguza manung’uniko ambayo hayaendani na juhudi zinazochukuliwa na Serikali hivi sasa kuondakana na tatizo hilo.

“wananchi wazidi kuelimishwa kuhusu tatizo la huduma ya maji lilivyo hivi sasa na juhudi zinazochukuliwa na Serikali kukabiliana nalo tukifanya hivyo bila ya shaka wataelewa”alisema Dk. Shein.

Naye Waziri wa Wizara hiyo, Mheshimiwa Ramadhan Abdalla Shaaban amesema katika mwaka wa fedha ujao Wizara yake imejipngia kuhakikisha kuwa asilimia kubwa ya ardhi inapimwa na kusajiliwa ili kupunguza migogoro ya ardhi.

Alifafanua kuwa katika kutekeleza malengo ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini Zanzibar II (MKUZA II) Wizara inajiwekea lengo la kusajili asilimia 50 ya ardhi ya Zanzibar ifikapo mwaka 2015.”alisema.
Kuhusu nishati ya umeme Waziri alieleza kuwa baada ya kukamilika uwekaji wa laini ya pili iliyozinduliwa jana Wizara yake sasa inaelekeza nguvu katika usambazaji wa huduma hiyo vijijini ili wananchi wengi waweze kufaidika na huduma hiyo.

Hata hivyo alieleza Wizara inaendelea na utafiti wa upatikanaji wa nishati mbadala ambapo maeneo kadhaa yameshaainishwa ambapo hatua ziko mbioni kuyapima na kuyapatia hati miliki.

No comments:

Post a Comment