TANGAZO


Sunday, January 13, 2013

TPA yasisitiza ushirikiano zaidi toka kwa wadau

Kaimu Meneja wa Kitengo cha Makasha wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Brigita Madolomani (katikati), akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani), jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, kuhusu ujio wa mashine mpya na za kisasa aina ya 'Gott Wald Crane' kwa ajili ya upakuaji na upakiaji wa mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam na Tanga. Kulia ni Kaimu Ofisa Mawasiliano Mkuu, Peter Milanzi. Mashine hizo za kisasa kila moja imenunuliwa kwa Ero milioni 2.6.


Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imeomba wasafirishaji mizigo kwenda nje kutoa ushirikiano mkubwa kwa mamlaka ili kwenda na kasi ya maboresho yanayofanywa katika bandari zake hasa ile ya Dar es Salaam.
Kaimu Meneja Mawasiliano wa Mamlaka hiyo Bi. Janeth Ruzangi alisema hayo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ushirikiano unaotakiwa kuwepo kati ya bandari na wasafirishaji hao hasa katika kipindi hiki cha maboresho makubwa ya bandari za mamlaka hiyo, hasa ya Dar es Salaam.
“Tunawaomba wasafirishaji kutoa ushirikiano mkubwa wa kuwahisha mizigo bandarini hapo ili kuzuia usumbufu wa mizigo kukosa meli kusafirishwa nje ya nchi,”alisema Bi.Ruzangi.
Bi. Ruzangi alisema alisema watumiaji wa kitengo cha mizigo ya kawaida (General Cargo Terminal) ya kwenda nje ya nchi wahakikishe wanatumia muda uliowekwa vizuri  kufikisha mizigo yao kwa wakati.
Kawaida wasafirishaji wanahitajika kufikisha mizigo yao siku tano kabla ya meli kufunga gatini na mwisho wa kupokea mzigo ni saa sita kabla ya meli kufunga gatini.
Alifafanua kuwa usumbufu unaojitokeza ni pamoja meli kufunga gatini bila kuwepo mizigo yote na kulazimika kuondoka.
Bi. Ruzangi alieleza kuwa kitendo hicho kinasababisha malalamiko kwa wasafirishaji na msongamano wa mizigo bandarini hapo na kukosa sehemu ya kuihifadhi.
Alisema utaratibu wa kuwahisha mizigo unasaidia kutoa nafasi ya kutosha kufanya maandalizi ya awali ya upakiaji wa mizigo (Pre- loading plan) kwa ajili ya kuongeza ufanisi wa kupakia mizigo melini.
Naye  Kaimu Meneja Kitengo cha Makashi (AG Container Terminal) wa Mamlaka hiyo, Bi.Brigita Madolomani alisema mamlaka imefanya maboresho ya vifaa vya kupakia na kupakua mizigo na wasafirishaji wanatakiwa kwenda na kasi hiyo.
“Meli ikiwa imetangazwa, wasafirishaji wanahitajika kuwahi kufanya malipo ya kupata nafasi ya kusafirisha mzigo,”alisema Bi.Madolomani.
Alisisitiza kuwa mizigo ikichelewa kufikishwa bandarini husababisha usumbufu kwa wenye meli na mamlaka.
Hivi karibuni TPA ilinunua vifaa vinne vya kisasa aina ya Gotwald kwa ajili ya kuboresha huduma za upakiaji na upakuani mizigo katika bandari za Dar es Salaam na Tanga.
Vifaa hivyo vyenye thamani ya jumla ya Euro 10.4 milioni vilinunuliwa kwa thamani ya Euro 2.6 Milioni kila kimoja na vina uwezo mkubwa wa kupakua na kupakia mizigo kwenye meli tofauti na ilivyo kuwa hapo nyuma.
Kununuliwa kwa vifaa hivyo kunafanya uwezo katika bandari hiyo kuongezeka kwa kiasi kikubwa na hatua hiyo ni moja ya mikakati ya kuhimili ushindani katika utoaji wa huduma hiyo katika ukanda huu.
Vifaa hivyo  pia vina uwezo wa kuendeshwa kwa rimoti na kufanya kazi kwa ufanisi na kwa umakini katika utoaji wa huduma hiyo kwa jamii.
Bandari ya Dar es Salaam ni moja ya bandari ambayo hutegemewa na nchi jirani zikiwemo Zambia, Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC), Rwanda na Burundi.



No comments:

Post a Comment