Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, akifungua pazia kama ishara ya uzinduzi wa Barabara ya Mfenesini-Bumbwini, Wilaya ya Kaskazini B, Unguja jana. Barabara hiyo imejenga na Kampuni ya Mecco kwa ufadhili wa Benki ya Dunia na Serikali ya Mapinduzi, ikiwa ni shamrashamra ya kuadhimisha miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Shein, akizungumza na wananchi na wafanyakazi wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano katika sherehe za ufunguzi wa Barabara ya Mfenesini-Bumbwini, Wilaya ya Kaskazini Unguja.
Baadhi ya Wananchi na wafanyakazi wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano, wakimsikiliza, Rais wa Zanzibar, Dk. Shein, alipokuwa akizungumza nao katika sherehe za ufunguzi wa Barabara ya Mfenesini-Bumbwini Wilaya ya Kaskazini Unguja.
Na Rajab Mkasaba, Zanzibar
WAKATI wananchi wa Zanzibar wakiadhimisha miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar , Serikali ya Zanzibar imesema imefanikiwa kutandaza mtandao wa barabara safi za lami kilomita 560 na kubakiwa na kilomita 83 katika maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba .
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohammed Shein, Dk. Shein, aliyasema hayo jana wakati akifungua rasmi barabara ya Misufini hadi Bumbwini, wakati akiwahutubia wananchi huko katika uwanja wa mpira Makoba Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja.
Dk. Shein, alisema kuwa wananchi wa Zanzibar wana kila sababu ya kufurahia uhuru huo, kwani serikali yao imefanikiwa kuwatandazia mtandao mkubwa wa barabara nchini kote kwa kilomita 560 jambo ambalao ni tofauti na nchi nyengine.
Dk. Shein, alisema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imesaidia kwa kiasi kikubwa kuinua maisha ya wananchi wa Zanzibar , katika shughuli zao mbali mbali za maendeleo ya kila siku.
Alisema kukuwa kwa mtandao huo wa barabara hivi sasa serikali inajiandaa kuona inaendelea kukamilisha kazi ya ujenzi wa barabara za Unguja na Pemba ambazo ni kilomita 83 ambazo zitajengwa kwa kiwango cha lami.
Alisema mkazo mkubwa wa serikali hivi sasa ni kuona inakamilisha barabara hizo zikiwemo za ndani katika mitaa mbali mbali pamoja na zile zilizoingia mashambani ambazo tayari hivi sasa zimo katika utaratibu wa kujengwa.
Alisema kuwapo kwa mtandao mkubwa wa barabara umeiwezesha serikali kupiga hatua ya kuweka mazingira bora ya mabadiliko ya uchumi katika sekta mbali mbali ikiwemo ya utalii, uvuvi, afya na biashara na sekta nyengine za kiuchumi kutokana na maeneo hayo ni yenye ukanda wa kiuchumi.
Alisema jambo la msingi kwa wananchi baada ya kupata barabara hiyo kuona wanakuwa ni matumizi mazuri kwa kuzingatia faida za kiuchumi huku wakizingatia kuitumia kwa usalama wa maisha ya watu wote.
Dk.Shein, alizitaka mamlaka husika kuona wanatimiza wajibu wao kwa kuhakikisha wanasimamia vyema sheria zaa ruhusa ya ujenzi kwa kuona hawaruhusu ujenzi wa nyumba za kukaa ama maduka ya biashara karibu na barabara kwa vile ni jambo la hatari.
Alisema inasikitisha hivi sasa kuona baadhi ya watu kuamua kujenga karibu ya barabara jambo ambalo ni hatari na linahitaji kuacha tabia hiyo.
Alisema ni lazima jamii ione haja ya kutofanya hivyo kwani suala hilo limekuwa likiitia hasara serikali kwa kulazimika kulipa fidia pale inapotaka kuongeza njia.
Ili kuepuka hilo Dk. Shein, amezitaka taasisi husika kuona inalifanyia kazi suala hilo kwa kuweka alama maalum ambazo zitakuwa ni miliki ya serikali pale inapotaka kutanua njia, kwani inasikitisha kuona Mamlaka hizo zimekuwa zikishuhudia vitendo hivyo vikifanyika katika ngazi ya awali hadi pale zinapofika juu lakini hakuna hatua inayochukuliwa.
Hata hivyo, Dk. Shein aliwataka wananchi hao kuona umuhimu wa kuzitunza barabara hizo, kwa kutambua kuwa ujenzi huo serikali imeufanya kwa gharama kubwa.
Hata hivyo, Dk. Shein, aliawapongeza wananchi wa Jimbo la Bumbwini kwa jitihada zao walizozionesha kwa kuwa wastahamilivu katika kipindi chote walichikiwa hawana barabara safi ya lami.
Aidha, Dk. Shein, alilipongeza Benki ya Maendeleo ya Afrika ADB kwa jitihada inzozifanya za kusaidia maendeleo ya Zanzibar kwani imefanya kuwapo kwa mabadiliko makubwa katikamsekta muhimu za utoaji wa huduma za kijamii.
Mwakilishi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, Tonia Kandieroakitoa maelezo yake aliipongeza serikali ya Zanzibar kwa jitihada ilizozifanya kuinua sekta ya huduma za kijamii kwani serikali imeweza kubadili hali ya kiuchumi na maisha bora.
Alisema hivi sasa Benki hiyo inajiandaa kuyaangalia maeneo mapya ya kiuchumi ambayo wataweza kuisaidia Zanzibar likiwemo suala la kuimarisha miundo mbinu ya huduma ya maji safi na salama.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano, alisema barabara ya Mfenesini hadi Bumbwini, ina kilomita 13.2 na kuchelewa kwake kukamilika kulitokana na serikali kuchelewa kulipa fidia za nyumba kuondosha mabomba ya amaji, nguzo za umeme, waya za redio mvuo kubwa na kuharibika akwa vifaa vya ujenzi.
Alisema katika mradi huo, unaojumuisha na madaraja na ulipaji wa fidia, serikali, imetumia jumla ya shilingi bilioni 10,678,168,594, ambapo barabara hiyo ilitumia shilingi 8,278,543,296 na shilingi 2,078,168,594 kwa madaraja ya Mwanakombo, Mto Kipange, Mto wa Maji na Kavert ya Mkokotoni na shilingi 87,789,156 ambazo zikiwa ni za fidia.
Alisema kukamilika kwa barabara hiyo kwa kiasi kikubwa utaweza kusaidia kuwafanya wananchi wa maneo hayo kukuza kiwango chao cha maisha na kuahidi kuwa Wizara hiyo hivi sasa inajipanga kuona deni la kampuni iliyojenga bara bara hiyo ya MECCO inalilipa.
Mwakilishi wa kampuni ya MECCO alitoa maelezo yake alisema licha ya kukamilisha mradi huo lakini bado amekuwa akikabiliwa na changamoto kubwa ya deni inalolidai serikali la shilingi bilioni 5 jambo ambalo limekuwa linahatarisha utendaji wa shughuli za kampuni hiyo kwa vile wanakabiliwa na ruiba kubwa kutoka katika mabenki na kuiomba serikali kuliona atatizo hilo na kulipatia ufumbuzi.
Waziri wa Wizara hiyo Rashid Hemed, akitoa maelezo yake aliishukuru Benki ya ADB, kwa michango yake inayoendelea kuipatia serikali ya Zanzibar na wananachi wake.
Nae Mkuu wa Mkoa huo, Pembe Juma Khamis, aliwapongeza wananchi wa vijiji iliyopita abarabara hiyo kwa kuwa wastahamilivu katika kipindi chote walichokuwa hawana barabara safi
Bara bara ya Mfenesini hadi Bumbwini, kwa mara ya mwisho ilijengwa 1927.


No comments:
Post a Comment