TANGAZO


Wednesday, January 9, 2013

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Zanzibar, Maalim Seif afungua Shule ya Mbuyu Tende kisiwani Zanzibar


 
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, akisalimiana na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Ali Juma Shamhuna mara baada ya kuwasili katika Kijiji cha Mbuyu Tende, Wilaya ya Kaskazini  “A” kwa ajili ya kufungua Shule ya Msingi yenye madarasa manne, ikiwa ni shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, akikata Utepe kuashiria kufungua Shule yenye madarasa manne katika Kijiji cha Mbuyu Tende, Wilaya ya Kaskazini  “A”, ikiwa ni  katika shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif  Sharif Hamad, akipanda mche wa mnazi kwenye uwanja wa  Shule ya Mbuyu Tende, Wilaya ya Kaskazini “A”, Baada ya Kuifungua, ikiwa ni shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Wanafunzi wa Shule ya Mbuyu Tende, Wilaya ya Kaskazini  “A”, wakifurahia baada ya kufunguliwa  shule yao hiyo, ikiwa ni katika shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar. (Picha zote na Yussuf Simai - Maelezo Zanzibar)

Na Khadija Khamis –Maelezo Zanzibar                        09/01/2013.

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Maalim Seif Shariff Hamad, amewataka Wazazi na Walezi wa Wanafunzi wa Shule ya Mbuyu Tende kujenga Mashirikiano na Walimu ili  kuweza kuwapatia  haki na fursa sawa wanafunzi wa kike na wakiume Shuleni hapo.    

Hayo ameyasema leo huko Shule ya Msingi Mbuyu Tende Wilaya Kaskazini “A” Unguja wakati wa ufunguzi wa skuli hiyo ikiwa ni mwendelezo wa shamra shamra za kutimiza miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Maalim Seif  amewataka Wazazi wasikubali kuwaozesha watoto wa kike waume mapema kwani hali hiyo ndiyo inayochangia ukosefu wa Walimu wa kike wazawa katika Vijiji  vingi.

Aidha alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaendelea kuwapatia wananchi wake haki ya elimu bila ya malipo ili kuondosha adui ujinga na kuwaletea maendeleo.

“Elimu ni msingi wa maisha kwa vijana na ndio inayoleta maendeleo na mwangaza hasa wakati wa sasa na ujinga ni kiza katika maisha ya leo,”alisisitiza Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar.

Alisema kuwa wanafunzi wakipata msingi mzuri wa elimu wataweza kupambana na mazingira ya sasa ya sayansi na teknolojia kwa kwa ufanisi mkubwa.

“Tusitazamie vijana kupata maisha mazuri bila ya elimu hasa katika zama hizo za Sayansi na tecnología kwani elimu ndio kila kitu’’alisema Makamo wa Kwanza .

Maalim Seif aliitaka Idara ya Mitaala kuandaa mbinu bora  za ufundishaji wa mafunzo ya amali ili wanafunzi wakimaliza masomo yao waweze kujiajiri wenyewe na kuweza kuondosha mzigo kwa Serikali.

Kwa upande wake Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Ali Juma Shamhuna alisisitiza wananchi wa kijiji hicho kuchukua juhudi ya kuwasimamia  watoto wao hasa wa kike kupata elimu kwani wanauwezo wa  kufanya vizuri zaidi katika masomo.

Aidha katika uzinduzi huo zaidi ya shilingi milioni 11 zilichangwa kwa ajili ya maendeleo ya skuli hiyo ambapo Makamu wa Kwanza wa Rais alichangia milioni tano na Waziri Shamhuna milioni tatu.

Ujenzi wa Skuli ya Mbuyu Tende umegharimu jumla ya shiling Milioni 44 kwa ajili ya kujengea jengo lenye madarasa manne pamoja na kununua madawati kwa Shule hiyo.                          

No comments:

Post a Comment