TANGAZO


Sunday, January 6, 2013

Rais Dk. Shein azindua Bohari Kuu ya Dawa Maruhubi mjini Zanzibar

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, akifungua pazia kama ishara ya uzinduzi wa Jengo la Bohari Kuu ya Dawa, Maruhubi, nje ya Mji wa Zanzibar leo, ikiwa ni shamrashamra za kilele  cha maadhimisho ya miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar. Kulia ni Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Alfonso Lenhardt. (Picha zote na Ramadhan Othman, Ikulu)
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, akikata utepe kama ishara ya uzinduzi wa Jengo la Bohari Kuu ya Dawa, huko Maruhubi nje ya Mji wa Zanzibar leo, ikiwa ni shamrashamra za kilele  cha maadhimisho ya miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar. Kulia ni Naibu Waziri wa Afya, Sira Ubwa Mamboya na  Balozi wa Marekani nchini, Alfonso Lenhardt.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, akipata maelezo kutoka kwa Meneja wa Bohari Kuu ya Dawa, Said Mohamed (kulia), alipotembela sehemu ya kuhifadhia dawa, baada ya kuzindua Jengo la Bohari Kuu ya Dawa huko Maruhubi, nje ya Mji wa Zanzibar, ikiwa ni shamrashamra za kilele  cha maadhimisho ya miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar. Wa tatu kushoto ni Balozi wa Marekani nchini, Alfonso Lenhardt.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein (wa tatu kulia) pamoja na viongozi
wengine, akiwemo Balozi wa Marekani nchini, Alfonso Lenhardt, wakiangalia namna ya uchukuaji dawa kwa kutumia mashine maalum na kutoa nje ya Bohari Kuu ya Dawa, baada ya kuifungua rasmi leo, huko Maruhubi, nje ya Mji wa Zanzibar, ikiwa ni shamrashamra za Maadhimisho ya miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar.


Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzíbar     06/01/2013
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema uzinduzi wa Bohari Kuu ya Dawa utaiwezesha Serikali ya Mapinduzi Zanzíbar kupanga bajeti yake vyema ya dawa na kusaidia utoaji wa huduma za afya kwa ubora wa hali ya juu.

Rais shein ameyasema hayo katika hafla ya uzinduzi wa Bohari Kuu ya Dawa iliyopo Maruhubi mjini Zanzibar leo, ikiwa ni mwendelezo wa shamrashamra za kutimiza miaka 49 ya Mapinduzi Zanzibar.

Amesema Bohari hiyo ya kisasa ni matunda ya kujivunia ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo kwa hakika italeta tija katika upatikanaji wa dawa na uimarisha wa afya za wananchi.

Dkt. Shein ameelezea matumaini yake kwa sekta ya afya kupitia Bohari hiyo na kwamba anaamini baada ya miaka mitatu Zanzibar itakuwa haipeleki tena Wagonjwa nje ya nchi kwa matibabu.

Aidha Dkt. Shein amewataka watumishi wa Serikali kubadilika kiutendaji kulingana na kasi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na wafanyakazi wa Bohari hiyo kuitunza vyema ili iendelee kutoa huduma kama inavyotakiwa.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya Sira Ubwa amesema Bohari hiyo itaboresha utoaji wa huduma kwa uhakika kutokana na ubora wa vifaa na mitambo ya kisasa ambapo wataalamu wataweza kubaini mahitaji ya Dawa zinazohitajika katika kila Hospitali za Unguja na Pemba.

Kwa upende wao Mabalozi wa Marekani na Denmark wameelezea kufurahishwa kwao na juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha afya ya Wananchi hasa katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Malaria na Ukimwi.

Aidha wameahidi kuendelea kutoa mashirikiano kwa Serikali hasa katika huduma za Afya kwa Mama na Watoto, Elimu, Mapambano dhidi ya magonjwa ya maambukizi pamoja na uzazi wa mpango.

Bohari hiyo iliyojengwa na Serikali ya Mapinduzi kwa msaada wa Shirika la USAID na NIDA inaelezewa kuwa ya tatu duniani katika viwango vya ubora ambapo jumla ya Dolla za Kimarekani Milion 1.2 zimetumika kukamilisha ujenzi wake.

No comments:

Post a Comment