Bango likionesha idadi ya
Watanzania wakati wa uzinduzi wa matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi,
uliofanywa na Rais Jakaya Kikwete leo kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es
Salaam.
Rais Jakaya Kikwete
akibofya kwenye kompyuta kuzindua rasmi matokeo ya awali ya Sensa ya Watu na
Makazi kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam. Idadi ya Watanzania kwa
sasa ni 44,929,002.
Kikundi cha uhamasishaji
kutoka wilayani Temeke, kikishangilia kwa furaha wakati wa uzinduzi huo.
Rais Jakaya Kikwete
akihutubia wakati wa hafla hiyo.
Rais Jakaya Kikwete
(kulia), Waziri Mkuu, Mizengo Pinda (katikati) na Mwenyekiti wa Kampuni za IPP,
Reginald Mengi wakifurahi baada ya uzinduzi huo.
Kamishna wa Sensa,
Hajat Amina Mrisho, akipongezwa na viongozi wa Serikali kwa kufanikisha sensa hiyo.
Baadhi ya viongozi wa
Vyama na Serikali wakiwa katika hafla hiyo
Baadhi ya wananchi wakiwa katika uzinduzi huo.
Mwakilishi wa Umoja wa
Mataifa wa Shirika la Idadi ya Watu Duniani akihutubia wakati wa hafla hiyo
Sasa ni wakati wa kuimba
utenzi wa kusifu sensa hiyo
Wanahabari wakijadiliana
jambo wakati wa uzinduzi huo. Kutoka kushoto ni Traiphone Mweji, Adamu Gire,
Chris Mfinanga na Antony Siame.
Baadhi ya wakazi wa Dar
es Salaam wakishangilia huku wakiwa na mabango ya kumpongeza Rais Jakaya
Kikwete.
Rais Jakaya Kikwete
(katikati waliokaa), akiwa na viongozi wengine wa Serikali pamoja na watumishi wa
Ofisi za Taifa za Takwimu za Tanzania Bara na visiwani wakati wa uzinduzi wa
matokeo ya awali ya Sensa ya Watu na Makazi kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar
es Salaam
Rais Kikwete, akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali na Idara ya Takwimu ya Taifa.
![]() |
Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, akimpongeza Rais Kikwete kwa kufanikisha sensa
hiyo.
|
Rais Jakaya Kikwete
akiteta na Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim
Lipumba wakati wa hafla hiyo.
HOTUBA
YA MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE,
RAIS
WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,
KWENYE
UZINDUZI WA MATOKEO YA AWALI YA
SENSA
YA WATU NA MAKAZI YA MWAKA 2012,
VIWANJA
VYA MNAZI MMOJA, DAR ES SALAAM
TAREHE
31 DESEMBA, 2012
Mheshimiwa
Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania;
Mheshimiwa
Balozi Seif Idd, Makamu wa Pili wa
Rais wa Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar;
Waheshimiwa
Mawaziri;
Waheshimiwa
Mabalozi;
Wawakilishi
wa Mashirika ya Kimataifa;
Viongozi
na watendaji wakuu wa Serikali;
Viongozi
wa Vyama vya Siasa, Viongozi wa Dini, Viongozi wa Jamii; Wanahabari;
Wageni
Waalikwa;
Mabibi
na Mabwana;
Nashukuru
kwa kunialika kuja kushiriki kwenye tukio hili muhimu na la kihistoria la
kutangaza matokeo ya awali ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012. Haya ni
matokeo ya kazi ya kuhesabu watu iliyofanyika kwa siku 14 kuanzia tarehe 26
Agosti, 2012 hadi 4 Septemba, 2012.
Ndugu
wananchi;
Napenda kutumia nafasi hii kutoa
pongezi za dhati kwa wale wote waliofanikisha zoezi la kuhesabu watu na wale
waliokamilisha uchambuzi unaotuwezesha leo kutangaza idadi ya Watanzania ilivyo
sasa. Kwanza kabisa napenda kutambua
Kamati ya Taifa ya Sensa iliyoongozwa na Mheshimiwa Mizengo Peter Kayanza Pinda,
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwa na Mheshimiwa Balozi Seif Ali Idi,
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akiwa Mwenyekiti upande wa Zanzibar. Nawashukuru kwa uongozi wao mzuri ambao
matunda yake ndiyo haya yanayotukusanya leo.
Pia nawashukuru wajumbe wa Kamati za Sensa za Mikoa na Wilaya
nchini.
Pili, napenda kuwatambua viongozi na
wafanyakazi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu ya Jamhuri ya Muungano chini ya uongozi
wa Mama Albina Chuwa na wenzao wa Afisi ya Mtakwimu Mkuu wa Zanzibar chini ya
uongozi wa Ndugu Mohammed Hafidh Rajab.
Nawapongeza kwa umahiri wao katika kuongoza, kuratibu na kisimamia
utekelezaji wa jukumu lenyewe la kuhesabu watu.
Ni wao kuliko mtu mwingine ye yote ndiyo waliokabidhiwa kazi ngumu ya
kutengeneza mipango na taratibu za kufanya zoezi lenyewe. Walitayarisha madodoso, kuyachapisha,
kuyasambaza, kuteua watu wa kuhesabu watu na wasimamizi wao. Waliwafundisha wajibu wao na kuwasimamia
katika utekelezaji wao. Ni wao pia
waliohakikisha kuwa madodoso yote yanakusanywa na uchambuzi unafanywa mpaka sasa
tuko tayari kutangaza matokeo.
Nawatambua na kuwashukuru makarani wa
sensa waliopita nyumba kwa nyumba kuhesabu watu na kukusanya taarifa mbalimbali
kwa mujibu wa madodoso waliyokuwa nayo.
Tunatoa shukrani na pongezi maalum kwao kwa sababu ni wao hasa
waliowezesha kupatikana taarifa itakayotangazwa leo na nyingine zitakazofuatia
siku za usoni. Kama si wao
tusingekusanyika hapa leo. Nawapongeza kwa umakini wao na moyo wao wa
uvumilivu na uzalendo. Haikuwa kazi
rahisi kwa ukubwa wa kazi yenyewe. Pia,
walikumbana na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na baadhi ya maeneo kuwa na
mazingira magumu ya kufanyia kazi kama vile ya usafiri. Lakini pia kulikuwa na
ugumu wa kupata taarifa kutoka kwa wanaoulizwa. Baadhi hawakutoa ushirikiano
unaotakiwa. Yalikuwepo pia matatizo ya
kupata huduma stahiki za kufanyia kazi na hasa posho. Nafahamu kuwa wapo bado wanaodai stahili
zao. Hazina wamekiri hilo na kuahidi
watalimaliza haraka.
Ndugu
wananchi;
Kufanya
sensa ni kazi kubwa na ghali sana. Hata
hivyo nchi zote duniani hufanya sensa kwa sababu ya umuhimu wake. Kupitia Sensa, hupatikana taarifa muhimu za
kutumiwa na Serikali kupanga mipango ya maendeleo ya nchi na jinsi ya kuhudumia
wananchi. Taarifa hizo hutumika na wadau
mbalimbali katika shughuli zao za kuwahudumia wanadamu. Ndiyo maana madodoso yalikuwa na mambo mengi
na ndiyo maana tumeambiwa kuwa taarifa ya leo ni ya mwanzo tu. Zipo taarifa zitakazofuatia zenye uchambuzi
wa mambo mbalimbali. Naomba tuwe na
subira kwa taarifa mbalimbali
tunazozitaka, kwani tutazipata wakati wake utakapofika. Kwa niaba yenu niwaombe wahusika wafanye kila
wawezalo kuhakikisha kuwa taarifa hizo zinapatikana kwa wakati
uliopangwa.
Ndugu
Wananchi;
Nitakuwa
mwizi wa fadhila kama sitawatambua watu wengine wafuatao: Wa
kwanza ni Hajat Amina Mrisho, Kamishna wa Sensa ambaye tulimkabidhi jukumu
la kutoa uongozi wa kisiasa katika kazi ya kuhesabu watu na kuwa kiungo kati ya
wataalamu na uongozi wa Serikali. Vile
vile, tulimpa kazi ya kusaidia kufikisha ujumbe pande zote ili kuona kuwa mambo
yanakwenda vizuri. Bahati nzuri
mwenyewe ni mjuzi wa masuala ya takwimu.
Alitokea huko kabla ya kumchukua na kumleta katika shughuli za uongozi wa
kisiasa. Hivyo, kazi ilikuwa mikononi
kwa mwenyewe. Namshukuru kwa kuifanya
kazi hiyo kwa ufanisi mkubwa. Anao
mchango mkubwa katika mafanikio haya. Wa pili ni wananchi wa Tanzania. Nawashukuru kwa ushirikiano wao. Kabla na wakati wa Sensa, kulikuwa na
purukushani na maneno mengi ya upotoshaji na kutishia kuvuruga zoezi
lenyewe. Wapo wenzetu walioamua
kuendesha kampeni ya kutaka watu wasusie.
Wapo walioamua kufanya maandamano na mikutano ya siasa wakati huo na
jitihada zote za kuwasihi wasubiri siku 14 zipite walizipuuza. Wakati mwingine unashindwa kuelewa baadhi
yetu tuna dhamira gani katika kujihusisha na shughuli za siasa? Hivi inakuwaje
washindwe kutambua umuhimu wa kuhakikisha jambo kubwa kama hili linafanikiwa?
Hivi zoezi la sensa lisipofanikiwa kiongozi wa siasa au wa dini unanufaika
nini? Ndiyo maana nawashukuru sana
wananchi kwa ushirikiano wao uliofanya njama za kuvuruga zoezi
kushindwa.
Ndugu
wananchi;
Wa
tatu ni
Wajumbe wa Kamati za Sensa za Mikoa na Wilaya kwa kufanikisha zoezi la Sensa
katika Mikoa na Wilaya zao. Nawashukuru Wakuu wa Mikoa na Wilaya wote nchini kwa
uongozi wao mzuri. Wa nne ni viongozi wa kijamii wakiwemo wa vyama vya
siasa, madhehebu ya dini na wa kimila waliosimama kidete kuhamasisha wafuasi wao
kushiriki katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi. Tunawashukuru kwa mchango wao
muhimu. Wa tano ni wamiliki wa vyombo vya
habari na wana habari. Nawashukuru kwa
kufanya kazi kubwa na nzuri ya kuhamasisha na kuelimisha jamii katika kipindi
chote cha utekelezaji wa zoezi la Sensa. Wito wangu kwenu ni kwamba, endeleeni
kuelimisha na kuhamasisha matumizi ya
taarifa za Sensa kwa maendeleo ya taifa letu.
Wa
mwisho,
lakini siyo kwa umuhimu, nawashukuru sana washirika wetu wa maendeleo wakiwemo
UNFPA, DFID, JICA, CIDA na Benki ya Dunia kwa mchango na msaada wao mkubwa.
Nawashukuru Wenzetu hawa wametupa ushirikiano mkubwa uliotuwezesha kufanikisha
zoezi la Sensa hadi kufikia hatua hii ya sasa ya kutoa matokeo ya awali. Naomba washirika wetu wa maendeleo waendelee
kushirikiana nasi kukamilisha kazi hii na pia katika kuimarisha sekta ya takwimu
nchini.
Ndugu
wananchi;
Baada
ya kusema maneno hayo sasa nipo tayari kuzindua rasmi matokeo ya awali ya Sensa
ya Watu na Makazi ya mwaka 2012. Kwa
heshima na unyeyekevu mkubwa natangaza kuwa kwa mujibu wa Sensa ya Watu na
Makazi iliyofanyika kwa siku 14 kuanzia Agosti 26, 2012, Tanzania ina watu 44,929,002 ambapo Tanzania Bara kuna watu 43,625,434 na Zanzibar kuna watu 1,303,568.
Katika Sensa ya tatu ya mwaka 2002 tulikuwa milioni 34.4 hivyo tumeongezeka kwa
watu milioni 10.5 ongezeko ambalo ni
sawa na asilimia 2.6 kwa mwaka. Naomba taarifa hizi zitumike kwa madhumuni
yaliyokusudiwa ambayo ni kuboresha maisha ya kila Mtanzania.
Ndugu
Zangu;
Hii
ni Sensa ya nne kufanyika nchini tangu kuasisiwa kwa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania mwaka 1964. Sensa ya kwanza
ilifanyika mwaka 1967 ambapo nchi yetu ilikuwa na watu 12,313,054. Tanzania Bara ilikuwa na watu 11,958,654 na Zanzibar watu 354,400. Kwa maana hiyo, katika miaka 45 tangu Sensa ya kwanza na hii,
Watanzania wameongezeka kwa watu milioni
33.
Ndugu
Wananchi;
Kama
kasi ya ongezeko la watu la asilimia
2.6 halitapungua ifikapo mwaka 2016 nchi yetu itakuwa na watu milioni 51.6. Inawezekana idadi hiyo ikaonekana
kuwa siyo tatizo la kuumiza kichwa kwa nchi kubwa kama yetu, lakini ni mzigo
mkubwa kwa taifa, jamii na uchumi kuwahudumia.
Inabidi pawepo na mikakati madhubuti na ionekane katika mipango ya
maendeleo kuanzia sasa jinsi ya kuhudumia watu hao 51.6 na zaidi ya hao miaka
inayofuata. Kwa familia, lazima tutambue
umuhimu wa kupanga uzazi, vinginevyo hali ya maisha itashuka sana. Kwa ujumla hatuna budi kufanya kazi kwa bidii
zaidi na nguvu zaidi.
Asanteni
sana kwa kunisikiliza.



No comments:
Post a Comment