Na Hillary Shoo, SINGIDA.
WAHITIMU wa kozi mbalimbali katika chuo cha uhasibu tawi la Singida (TIA),  wametakiwa kuweka uadilifu mbele popote watakapokuwa kwa kuwa ndiyo dira sahihi ya maisha yao.

Hayo yamebainishwa jana mjini hapa na Naibu Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum, wakati wa sherehe za mahafali ya kwanza ya Tawi hilo zilizofanyika Chuoni hapo eneo la Ginnery mjini Singida.Naibu Waziri huyo alisema kuwa taaluma ya uhasibu ni taaluma iliyotukuka hivyo ni jambo zuri iwapo watu walioisomea watazingatia miiko na kanuni zake kwa kiwango cha hali ya juu.Alieleza kuwa kashfa mbalimbali zinazosikika nchini na kwingineko duniani ni matokeo ya watu kukosa uadilifu na hivyo kujiingiza katika vitendo viovu.“Naomba kuwakumbusha kwamba mtakapotoka hapa baada ya kuhitimu masomo yenu, mtakutana na changamoto mbalimbali, ila mkumbuke tu kwamba ni uadilifu pekee ndio utakaowaongoza katika maisha yenu yote” alifafanua.

Aliwataka wahitimu hao kutumia vema elimu waliyoipata katika kubuni, kuanzisha na kusimamia shughuli mbali mbali ya kibiashara zitakazowasaidia wao na jamii yote ya Watanzania kwa kuleta maendeleo.
“Enzi ya kutaraji kuajiriwa na serikali imepitwa na wakati. Wekeni mawazo yenu sasa katika kujiajiri wenyewe kwani elimu mliyopata inatosha kuwawezesha kupambana vizuri na changamoto zozote mtakazokumbana nazo. “ Alisema.

Aidha, Salum alitoa mwito kwa wahitimu hao kutotosheka na elimu waliyopata bali wajiendeleze zaidi na kuhakikisha wanafikia malengo wanayojiwekea.Awali, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa TIA, Shah Hanzuruni alimweleza Naibu Waziri huyo kuwa Tawi la TIA Singida linakabiliwa na uhaba mkubwa wa madarasa, nyumba za wahadhiri, kumbi za mihadhara, samani, maktaba ya kisasa na wahadhiri.Jumla ya wahitimu 1,331, wakiwemo wanawake 662 na wanaume 669, walitunukiwa vyeti na stashahada za fani mbalimbali ikiwemo uhasibu, uboharia, raslimali watu na biashara.