TANGAZO


Saturday, November 3, 2012

Rais Kikwete akemea unafiki wa wanasiasa, Ikibidi kuzifunga baadhi ya NGO's

Rais Jakaya Kikwete
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amekemea unafiki wa baadhi ya wanasiasa nchini ambao wao wanaishi maisha mazuri lakini wanawahubiria wananchi kubakia katika maisha ya uduni.

Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa kama itakuwa ni lazima, Serikali itazifunga baadhi ya taasisi zisizokuwa za kiserikali – NGO’s – ambazo kazi zao imekuwa ni kuendesha kampeni za kuvuruga jitihada za maendeleo za wananchi kwa kuwapotosha.

Rais pia amesema kuwa ni kupoteza muda na wakati kwa baadhi ya wanasiasa kuendesha kampeni ya kupinga ujenzi wa Barabara ya Loliondo kwa sababu wapende, wasipende barabara hiyo itajengwa ingawa haitajengwa kwa lami ndani ya Mbunga ya Taifa ya Serengeti.
Rais Kikwete ameyasema hayo leo, Jumamosi, Novemba 3, 2012, wakati alipozungumza na wananchi katika kijiji cha Masaika, nje ya mji mkuu wa Mkoa wa Manyara wa Babati, kabla ya kuzindua barabara mpya ya Singida-Babati-Minjingu yenye urefu wa kilomita 98.
Rais Kikwete amelazimika kuonya kuhusu unafiki wa baadhi ya wanasiasa kutokana na jitihada ambazo zimekuwa zinafanywa na wanasiasa hao wakiwarubuni na kuwapotosha wananchi wa jamii ya Kimasai kuhusu jitihada za Serikali kuwaletea maendeleo wananchi wa jamii hiyo.
“Kuna baadhi ya wanasiasa na NGO’s ambao wamekuwa wanaendesha upotoshaji wakidai kuwa jitihada za Serikali kuwahimiza wananchi wa Jamii ya Kimasai kujenga nyumba nzuri, kuishi maisha mazuri na kwenda shule ni kuwanyima haki Wamasai hao. Wanadai kuwa wanatetea haki za Wamasai. Huu ni uptoshaji tu,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Hawa wanasiasa na wanaharakati ni watu wa ajabu sana. Wao wanavaa vizuri, wanakwenda wamevaa suti na sketi nzuri na za kuvutia kwenda kuwapotosha wanajamii ya Kimasai wakiwaambia waendelee kuvaa ngozi, kuvaa lubega, kuishi kwa kura mizizi. Unafiki tu, mbona wao hawaishi maisha ya Kimasai na wao wanatoka kabila hilo hilo. Wanafanya kazi ya kuwapiga picha ili wakauze na kupata picha lakini Wamasai wabakie vile vile.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Sisi viongozi tuna dhamana ya kuwasaidia wananchi kujiletea maendeleo, siyo kuwadanganya watu.”

Amesema kuwa kama ni lazima Serikali itazifungua NGO’s ambazo zinacheza mchezo huu wa kuwapotosha wananchi. “Tutazifunga kama zitaendelea kupinga maendeleo ya wananchi.”

Kuhusu Barabara ya Loliondo, Rais Kikwete amewaambia baadhi ya wabunge wa eneo hilo, “Barabara ile ya Loliondo anayeamua ni mimi. Hamtafanikiwa katika kampeni yenu kwa sababu kama mnataka kupata barabara ya kupita Kusini mwa Serengeti mimi nitawasaidieni kuipata. Lakini barabara ya Kaskazini mwa Serengeti itajengwa na msije kujidanyanga kuwa mkiipigia debe ile ya Kusini na kuipinga ile ya Kaskazini kutazuia kujengwa kwa barabara ile.”

No comments:

Post a Comment