Rais Jakaya Mrisho Kikwete akioneshwa na Mchungaji Alkwin Mbawi, uharibifu mkubwa uliofanywa kwenye kanisa la Pentekoste la Mbagala jijini Dar es Salaam wakati wa vurugu za Waislamu, Ijumaa iliyopita kufuatia habari za mtoto mmoja wa sehemu hiyo, kuukojolea Msahafu wa Kuraan Tukufu.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akioneshwa na Mchungaji Alkwin Mbawi uharibifu mkubwa uliofanywa kwenye magari yaliyokuwa yameegeshwa ndani ya kanisa la Pentekoste la Mbagala jijini Dar es Salaam wakati wa vurugu za Waislamu, Ijumaa iliyopita kufuatia habari za mtoto mmoja wa sehemu hiyo, kuukojolea Msahafu wa Kuraan Tukufu.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akioneshwa na Katibu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam Bw. M Mkosimonga uharibifu mkubwa uliofanywa kwenye kanisa hilo, huko Mbagala jijini Dar es Salaam wakati wa vurugu za Waislamu, Ijumaa iliyopita kufuatia habari za mtoto mmoja wa sehemu hiyo, kuukojolea Msahafu wa Kuraan Tukufu.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akitoa pole kwa baadhi ya waumini wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es salaam kufuatia uharibifu mkubwa uliofanywa kwenye kanisa hilo, huko Mbagala jijini Dar es Salaam wakati wa vurugu za Waislamu, Ijumaa iliyopita kufuatia habari za mtoto mmoja wa sehemu hiyo, kuukojolea Msahafu wa Kuraan Tukufu.
Na mwandishi wetu
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, ametoa pole kwa waumini wa makanisa yaliyochomwa moto na kuharibiwa katika eneo la Mbagala, Dar es Salaam, akisisitiza kuwa wote waliohusika katika vurumai hizo na uharibifu huo na wale waliowatuma watashughulikiwa ipasavyo na Serikali.
Aidha, Rais Kikwete ameyaelezea matukio ya jana, Ijumaa, Oktoba 12, 2012 kuwa ni ya aibu na fedheha ambayo halikustahili kutokea katika nchi yenye historia ya miaka mingi na ya kutukuka ya waumini wa dini mbali mbali kuvumiliana na kuishi kwa amani.
Rais Kikwete pia ametoa wito kwa viongozi wa dini zote mbili kuwa watulivu katika hali ya sasa na kutokuhamanika na kuviachia vyombo vya Serikali kufanya kazi, akiwaasa viongozi wa makanisa yaliyoharibiwa kuwa watulivu na kutokufikiria hatua za kulipiza kisasi kwa sababu kamwe hatakuwepo mshindi katika vurumai hasa ya kidini.
Rais Kikwete ameyasema hayo leo, Jumamosi,Oktoba 13, 2012, wakati alipofanya ziara ya ghafla kutembelea makanisa yaliyochomwa moto katika eneo la Mbagala kufuatia vurumai za jana ambako chanzo chake ni mtoto kukojolea Kitabu Kitukufu cha Qoran katika eneo hilo hilo la Mbagala.
Rais Kikwete ametembelea makanisa matatu ambako alishuhudia yalivyoharibiwa kwa vioo vya madirisha kuvunjwa, madhabau kuharibiwa na biblia kuchomwa moto, vyombo vya muziki kuibwa ama kuvunjwa, magari ya viongozi wa dini na waumini kuchomwa moto, vioo vya magari hayo kuvunjwa na mali za ndani ya magari, zikiwamo redio kuibiwa, nguo za wachungaji na hata divai kuibiwa.
Rais Kikwete ameanzia ziara yake kwenye Kanisa la Mbagala kwa Yesu la Tanzania Assemblies of God (TAG) ambako amepokelewa na Askofu Dkt. Magnus Muhiche na kuonyeshwa uharibifu mkubwa uliofanyika kwenye kabisa hilo ambalo limeonekana kufanyiwa uharibifu mkubwa zaidi kuliko makanisa mengine ikiwa ni pamoja na jenereta ya umeme ya kanisa kuibiwa.
Katika ziara hiyo ambako Rais Kikwete ameandamana na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa William Nchimbi aliambiwa na Kamanda wa Mkoa Maalum wa Dar es Salaam, Kamanda Suleiman Kova kuwa mpaka sasa watu 122 wametiwa mbaroni kufuatia vurumai na fujo za jana.
Kati ya hao, watu 36 wamekamatwa kwa kufanya uharibifu kwenye makanisa hayo na wengine 86 wamekamtwa kwa kufanya fujo za kawaida na za jumla katika hali ya mazingira ya jana.
Rais amesema kuwa ni kweli kuwa kitendo cha mtoto kukojolea Qoran ni kitendo cha makosa lakini vile vile kuvunja makanisa nalo ni kosa hasa kwa kutilia maanani kuwa uharibifu wa kukojolea Qoran ulikuwa tayari unashughulikiwa na vyombo vya ulinzi na usalama wakati makanisa yanaanza kuchomwa.
“Katika hali hiyo basi nawaomba viongozi wa pande zote mbili wawe wavumilivu na wasihamanike kwa sababu mazingira ya sasa ndiyo kipimo cha uongozi na kiongozi akihamanika basi wafuasi wake watahamanika mara 10 zaidi. Waiachie Serikali na vyombo vyake kulishughulikia jambo hili,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Kwenye vurumai za kidini hakuna mshindi. Ni shughuli haina tija. Nawaombeni viongozi kuhakikisha kuwa jambo hili haliigawi jamii yetu ambayo kwa miaka mingi imeishi pamoja bila kujali tofauti zao za kidini. Linalofaa kwa sasa ni viongozi wa pande zote kukaa pamoja na kuzungumza namna ya kurejea utulivu, amani na mshikamano.”
Rais Kikwete pia ametembelea Kanisa la Utatu Mtakatifu la Madhehebu ya Anglikana ambako amepokewa na Katibu wa Kanisa hilo, Bwana Albert Mukasimongwa ambaye vile vile amemwonyesha uharibu uliofanywa kwenye Kanisa hilo wakati wa fujo hizo ikiwa pamoja na kuharibu kabisa madhabau.
Rais amemalizia ziara yake kwenye Kanisa la KKKT ambako ameshuhudia kundi kubwa la waumini wakiendelea kusali, kuimba na kulia. Kwenye Kanisa hilo amepokelewa na Mchungaji George Fupe ambaye pia ni Msaidizi wa Askofu wa Jimbo la Dar es Salaam la KKKT aliyewaomba waumini “kutulia na kusikiliza Sauti ya Faraja ya Mheshimiwa Rais.”
Rais amewaambia waumini hao: ‘Jamani poleni sana. Nimekuja kuwapeni poleni kuhusu jambo hilo la kusikitisha, jambo la fedheha, jambo la aibu kabisa, jambo ambalo hatukutegemea litokee katika nchi yenye historia nzuri sana ya uvumilivu wa kidini.
Ameongeza Rais Kikwete: “Ombi langu kwa pande zote ni tulivu tukiongozwa na viongozi wetu. Tusilipize kisasi kwa sababu hilo halitasaidia. Tuviachie vyombo vya sheria vifanye kazi yake. Nawahakikishi eni kuwa yoyote aliyehusika atashughulikiwa ipasavyo na pamoja wale waliowatuma. Nao hawataachiwa.”
No comments:
Post a Comment