TANGAZO


Friday, October 5, 2012

Mgeja aibuka kidedea uchaguzi wa CCM Shinyanga

Hamis Mgeja, mdogo wa Msabaha, aliyeshinda Wilaya ya Shinyanga Vijijini leo.


Na mwandishi wetu,
Shinyanga
KINYANG’ANYIRO cha uchaguzi wa viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika Wilaya ya Shinyanga vijijini leo, kimekamilika huku Mwenyekiti aliyekuwa akitetea nafasi yake, Msabaha Mgeja akiibuka na ushindi wa kishindo kwa kumgaragaza aliyekuwa Katibu wa Wilaya wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) wilayani humo, Richard Pambe.

Mgeja ambaye ni kaka mkubwa wa Mwenyekiti wa CCM, mkoani Shinyanga katika uchaguzi huo, alipata kura 1,056 na kumshinda mpinzani wake aliyeambulia kura 59, matokeo ambayo yamemuacha njia panda Pambe aliyeamua kujiuzulu ukatibu wa UVCCM wilayani humo akiwa na matumaini makubwa ya kuibuka na ushindi katika kinyang’anyiro hicho.

Wagombea wengine katika nafasi hiyo ya Uenyekiti wa Wilaya, walikuwa ni Charles Miti aliyepata kura 45 na Mary Butondo Nchambi akiambulia kura 39.  Nafasi ya mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) ilikwenda kwa mbunge wa viti maalumu Azza Hillal baada ya kuwabwaga wapinzani wake wawili Christina Mzava na Patrick Chokala.

Nafasi ya Katibu wa Itikadi na Uenezi ilichukuliwa na Emmanuel Lukanda aliyepata kura 82 aliyemshinda Mohamed Gimbuyi aliyekuwa akitetea nafasi hiyo aliyeambulia kura 31 akifuatiwa na Robert Njille aliyepata kura 17 huku Emmanuel Masunga akipata kura 11.

Wajumbe wa mkutano huo walimchagua Filipo Msabila kuwa Katibu wa Uchumi na Fedha kwa kura 83 na kumshinda mpinzani wake Juma Warioba aliyepata kura 50 ambapo wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM Taifa walioibuka na ushindi ni pamoja na Amos Mshandete, Christina Mzava, Abeid Aljabry, Charles Kabogo na Isaack Sengerema.

Wilayani Kishapu mwenyekiti aliyekuwa akitetea nafasi yake Shija Ntelezu alifanikiwa kuendelea na wadhifa huo baada ya kupata kura 594 na kuwashinda wapinzani wake John Ndama aliyepata kura 440 na Ally Shiganga aliyepata kura 146.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa (NEC) ilikwenda kwa Boniface Butondo aliyeibuka mshindi baada ya kupata kura 665 na kumshinda mpinzani wake wa karibu aliyewahi kuwa mbunge wa Jimbo la Kishapu Bw. Paulo Makolo aliyepata kura 427 huku Bw. Anthony Sollo akipata kura 36.

Wilaya ya Shinyanga mjini Kanali mstaafu wa jeshi la wananchi (JWTZ) Tajiri Maulidi alifanikiwa kuibuka mshindi katika nafasi ya mwenyekiti wa wilaya hiyo baada ya kumwangusha Salum Abdalah (Zamzam) kwa kura 340 dhidi ya kura 318 alizopata mpinzani wake huku Alhaji Salum Simba aliyekuwa akitetea nafasi yake ambaye alipata kura 90.

Katika uchaguzi huo Charles Shigino alichaguliwa kuwa Katibu wa Itikadi na uenezi wa wilaya baada ya kumshinda Said Bwanga aliyekuwa akitetea nafasi hiyo huku Ahmed Dotto Mapalala alichaguliwa kuwa Katibu wa Uchumi na fedha wa wilaya huku Gaspar Kileo (Gaki) akichaguliwa kuwa mjumbe wa NEC akimbwaga kwa mbali mpinzani wake  Erasto Kwilasa.

Huko wilayani Kahama Mabala Mlolwa alichaguliwa kuwa mwenyekiti mpya wa wilaya hiyo kwa kupata kura 992 na kumshinda mpinzani wake baada ya uchaguzi kulazimika kurudiwa mara ya pili baada ya ule wa kwanza wagombea wote kushindwa kupata kura zaidi ya nusu Patricia Nangale alipata kura 789.

Nafasi ya mjumbe wa NEC katika wilaya hiyo ilikwenda kwa Catherine Dalali ambaye ni nduguye na Waziri Mary Nagu aliyewashinda wapinzani wake wawili waliokuwa wakiwania kwa pamoja nafasi hiyo muhimu ndani ya Chama cha Mapinduzi.

Macho na masikio ya wakazi wa mkoa wa Shinyanga hivi sasa yanasubiri kwa tashwishi kubwa uchaguzi wa ngazi ya mkoa unaotarajiwa kufanyika mjini hapa Oktoba 9, mwaka huu ambapo ushindani mkubwa unatarajiwa kuwa kati ya Khamis Mgeja na aliyekuwa katibu mwenezi wake wa mkoa Hassan Mwendapole.


No comments:

Post a Comment