TANGAZO


Thursday, October 4, 2012

Kocha mpya wa Yanga akiri Simba ni zaidi ya Yanga


 Kocha Msaidizi wa Yanga, Fredy Felix Minziro (katikati) akimuelekeza jambo Kocha Mkuu wa klabu hiyo Ernstus Wilhelmus Johannes Brandts (kulia), wakati wa pambano kati ya Yanga na Simba kwenye Uwanja wa Taifa.
 Mshambuliaji Haruna Moshi 'Boban' wa Simba kulia, akichuana na beki wa kulia wa Yanga, Mbuyu Twite wakati wa pambano baina ya klabu hizo juzi kwenye Uwanja wa Taifa.
Mlinda mlango wa Yanga Yaw Berko kushoto, akipeana mkono kwa furaha na mshambuliaji wa Simba Daniel Akuffo. Berko na Akuffo wote ni nyota wa kimataifa Ghana na baada ya kumalizika kwa mechi walionekana kukumbatiana na kufurahi pamoja huku wakiongea machache.

DAR ES SALAAM, Tanzania 

BRANDTS aliyejaza pengo la Mbelgiji Tom Saintfiet, alikiri kwamba, kupoteana kwa kikosi chake katika kipindi cha kwanza, hakukutokana na wachezaji kutofuata mafundisho, bali kuzidiwa kimbinu, ufundi na umakini na mahasimu wao Simba

KOCHA mpya wa timu ya Yanga, Ernstus Wilhelmus Johannes Brandts, amekiri uimara wa kikosi cha Simba, huku akisema soka lililochezwa na Wekundu hao wa Msimbazi kipindi cha kwanza cha pambano dhidi yao juzi linastahili kupongezwa.

Akizungumza baada ya pambano hilo la Ligi Kuu ya Vodacom lililoisha kwa sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Brandts alisema Simba ni timu nzuri iliyompa wakati mgumu katika dakika zake 30 za kwanza kama Kocha Mkuu wa Yanga.

Mholanzi huyo aliyejaza pengo la Mbelgiji Tom Saintfiet, alikiri kwamba, kupoteana kwa kikosi chake katika dakika zote hizo hakukutokana na wachezaji kutofuata mafundisho, bali kuzidiwa kimbinu, ufundi na umakini miongoni mwa nyota wake.

“Simba ilionekana kulianza vema pambano na hali kuwa ngumu kwetu kwa dakika 30. Viungo wakaonekana kupoteza umakini, na kuruhusu mashambulizi kuja kwetu, lakini shukrani ni kwamba licha ya kutawala mchezo, lakini walishindwa kutumia makosa yetu,” alisema Brandts.

Aliongeza kuwa, ubora wa kikosi chochote ni pamoja na matumizi ya makosa ya wapinzani, na kama Simba ingekuwa makini katika hilo hali ingekuwa ngumu zaidi kwao ndani ya kipindi hicho, kitu alichoahidi kukifanyia kazi kuelekea mechi zijazo.

"Ilikuwa mechi ngumu mno dhidi ya mabingwa watetezi Simba, lakini kwa upande mwingine nimeridhishwa na aina ya upiganaji wa vijana wangu na kuambulia pointi muhimu."

"Ikumbukwe hii ni mechi yangu ya kwanza na nilikuwa na timu hii kwa siku mbili tu kuelekea mechi hii, lakini nimeyaona mapungufu hasa ya kinidhamu na naahidi kuyafanyia kazi," alisema Brandts.

Hata hivyo, alipongeza mabadiliko yake ya mapema ya kumtoa mshambuliaji Hamisi Kiiza na kumuingiza kiungo Frank Domayo, yaliyoirejeshea Yanga uhai sehemu ya kati na kumudu kuibadili sura ya mchezo, hasa baada ya kuwaingiza pia Didier Kavumbagu na Juma Abdul.

Brandts aliamua kumtoa Kiiza na kumuingiza Domayo dakika ya 35 ya mchezo, mabadiliko yaliyoipa Yanga uhai kwa dakika 10 za mwsho za kipindi hicho, kisha kipindi cha pili ilikomudu kushambulia na kuipa wakati mgumu safu ya ulinzi ya Simba.

Mholanzi huyo alikataa kuyazungumzia maamuzi ya refa Mathew Akrama aliyemuonya kwa kadi ya njano mshambuliaji Haruna Moshi ‘Boban’, huku akimlima nyekundu Simon Msuva katika matukio mawili yaliyozua maswali miongoni mwa mashabiki.

Boban ‘alimpanda’ katika nyama za paja beki Kelvin Yondani na kuambulia kadi ya njano, huku Msuva akilimwa nyekundu kwa kwa madai ya kumfanyia rafu beki Juma Nyoso  baada ya kuwa filimbi ilishapigwa na yoso huyo wa Yanga kuonywa kwa kadi ya njano.

“Nisingependa kuzungumzia maamuzi ya refa. Alichoamua ni sehemu ya majukumu yake na kukosoa si kati ya tabia njema za kiuanamichezo. Nafikiri itakuwa vema kama nitaulizwa kuhusu kilichofanywa na nyota wa pande mbili, hasa wa kikosi changu,” alisema Brandts.

Licha ya awali kudaiwa angekuwa jukwaani kutokana na kukosa kibali cha kufanya kazi nchini, Brandts akachomoza katika karatasi za vikosi ‘line up’, kabla ya kuingia na timu hiyo wakati wa mazoezi mepesi na kuamsha shangwe kwa mashabiki wa timu yake, kisha kukaa kwenye benchi wakati wa mchezo.

No comments:

Post a Comment