TANGAZO


Friday, October 12, 2012

Khamis Mgeja aibuka kidedea nafasi yake ya Uenyekiti

Mbunge wa Jimbo la Kahama, James Daud Lembeli (kulia), akimpongeza Mwenyekiti wa CCM, Hamis Mgeja kwa kuteuliwa kwake na Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa kutetea nafasi yake hiyo. Mgeja ameshinda nafasi hiyo katika uchanguzi uliofanyika mwanzoni wiki hii.




Na Mwandishi wetu,
Shinyanga
HATIMAYE Khamis Mgeja amefanikiwa kutetea kiti chake cha uenyekiti wa mkoa baada ya kuibuka na ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Shinyanga uliofanyika juzi mjini Shinyanga akiwabwaga wapinzani wake watatu.
Huku jina lake likiwa limerejeshwa na Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa (NEC) katika dakika za majeruhi, Mgeja aliweza kupata kura 435 kati ya kura 754 zilizopigwa ambapo mshindani wake wa karibu Hassan Mwendapole alipata kura 277 huku kura tatu zikiharibika.
Katika kinyang’anyiro hicho cha uenyekiti wagombea wengine Alex Seseja alipata kua 27 huku Dkt. Gerald Mwanziya akiambulia kura 10 wakiwa wameachwa mbali na Mgeja ambaye awali uvumi ulikuwa umeenea mjini hapa kwamba huenda asingechaguliwa kutokana na mizengwe iliyokuwa imemwandama ikiwemo vikao vya mkoa kufyeka jina lake.
Wajumbe wanane wa Halmashauri Kuu ya mkoa waliochaguliwa wawili kutoka kila wilaya ambapo kutoka wilaya ya Kishapu walioibuka na ushindi walikuwa Paul Makolo na Christina Gule, Shinyanga vijijini, Amos Mshandete na Richard Masele.
Katika wilaya ya  Shinyanga mjini wajumbe walioibuka na ushindi walikuwa ni Deogratias Sulla na Eisha Stima, ambapo  kwa upande wa wilaya ya Kahama waliochaguliwa walikuwa ni Patricia Nangale na Khalfan Mandwa.
Nafasi ya Katibu wa Siasa na Uenezi mkoani Shinyanga imekwenda kwa Emmanuel Mlimandago aliyeibuka na ushindi na kuwashinda wapinzani wake wawili huku Mwendapole aliyekuwa akitetea nafasi hiyo akiamua kujitoa kabla ya kufanyika kwa zoezi la upigaji kura.
Wajumbe wa halmashauri ya CCM mkoa pia walimchagua Gasper Kileo kuwa Katibu wa Uchumi na Fedha wa mkoa huku Paulo Makolo, Amos Mshandete, Erasto Kwilasa, Alhaj Salum Simba na Boniface Butondo wakichaguliwa kuwa wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa.
Akifungua mkutano huo, msimamizi wa uchaguzi huo mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) kutoka Zanzibar Asha Abdalah aliwatahadharisha wajumbe kuhakikisha wanachagua viongozi wenye uwezo wa kufanya kazi  watakaoweza kukivusha chama hicho katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Msimamizi huyo alisema viongozi wanaotakiwa kuchaguliwa katika kipindi hiki ni wale wenye moyo wa kukitumikia chama wasio wabinafsi, wenye uwezo, waadilifu na hodari watakaokuwa wabunifu wenye moyo wa kujitolea katika shughuli za chama.
Akiwashukuru wajumbe baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi huo Mgeja aliishukuru Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) kwa uamuzi wake wa kuamua kulirejesha jina lake pamoja na kwamba vikao vya mkoa na kamati kuu vilikuwa vimemuengua kwa kile kilichodaiwa kuwepo kwa shinikizo la baadhi ya vigogo ambao hawaungi mkono.
Alisema baadhi ya vigogo ndani ya CCM walifanya chini juu kuhakikisha jina lake linakatwa na vikao vya awali hali ambayo ingesababisha ashindwe kutetea nafasi yake hiyo kwa chuki binafsi zisizo na maslahi ndani ya chama.
“Wana CCM wenzangu kwa siku ya leo sina budi kukushukuruni sana kwa maamuzi yenu ya busara, sina cha kuwalipa zaidi ya kuwashukuru, mmeonesha imani kubwa kwangu, na napenda niwathibitishie kwamba Mgeja mliyemchagua leo siyo Mgeja wa yule wa jana, huyu ni Mgeja mpya anayekuja na mambo mapya,” alisema.
Mgeja alisema mbali ya kuwashukuru wajumbe wa mkutano mkuu huo, lakini pia aliwaomba kurejesha umoja na mshikamano miongoni mwao kwa lengo moja la kukiwezesha chama kiweze kuendelea kuaminiwa na watanzania na kifanikiwe kuongoza serikali.
Alisema pamoja na baadhi ya watu kuendesha kampeni za majitaka katika kipindi cha kampeni kwa lengo la kumchafua na wakisambaza fedha kwa wapiga kura ili kuhakikisha hachaguliwi lakini mbinu zote hizo hazikufua dafu bado wana CCM wameonesha kuwa na imani naye wameendelea kumpa ridhaa ya kukiongoza chama hicho katika mkoa wa Shinyanga.



No comments:

Post a Comment