TANGAZO


Tuesday, August 14, 2012

Waziri Mkuu Pinda awataka wanafunzi kuwa na nidhamu

Waziri Mkuu Mizengo Pinda

Na Magreth Kinabo, Maelezo Dodoma
14/8/2012
WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda  amewataka  wanafunzi wote nchini kuwa na nidhamu, kujituma na kufuata maelekezo vizuri ya walimu wao na kuepuka makundi mabaya ili kuweza kupata mafanikio katika masomo yao.
Aidha Waziri Mkuu Pinda  amewaasa  wanafunzi waliofanya vizuri katika mtihani  wa kuhitimu  kidato cha sita  wa  mwaka huu  kutumia uhuru vizuri  watakaoupata   kwenye maisha ya vyuo vya elimu ya juu bila kurudi nyuma katika maendeleo ya  masomo yao.
Kauli hiyo ilitolewa leo na Waziri Mkuu, Pinda Bungeni mjini Dodoma kabla ya kuwatunuku  vyeti vya kuwapongeza wanafunzi  hao  19 kati 20  waliofanya vizuri katika mtihani huo,kutoka shule mbalimbali nchini, ambapo mmoja wao, Jamal Juma  yuko nje ya nchi.
Wanafunzi hao ambao wote walipata  ufaulu wa daraja la kwanza katika mtihani huo, saba kati yao  wanatoka katika shule  ya wasichana ya Marian, watatu Mzumbe, wawili Fedha na wengine wawili Kibaha. Waliobakia mmoja mmoja anatoka Kilakala, Ufundi Ifunda, Tabora girls, Tabora boys, Minaki na Mpwapwa.
“Mmefanya vizuri. Mnastahili ! Hongereni Sana.   Tunataka ufaulu wenu uwe mzuri zaidi kwa vile sasa ninyi mnakweda kujenga weledi. Mnakuwa wataalamu wa fani Fulani. Tumieni muda wenu kujifunza zaidi kutafuta maarifa zaidi na kuvumbua mambo makubwa zaidi yatakayowasaidia ninyi wenywe na jamii kwa ujumla  kujiletea maendeleo,” alisema Waziri Mkuu Pinda.
 Aliongeza  kuwa   ni vizuri utaratibu  huo wa kuwatambua wanafunzi bora uwe endelevu na  ikiwezekana wapatiwe fursa ya kuendelezwa katika vyuo vikuu vya kipekee nje ya nchi hususan kwenye fani zitakazojenga uwezo kwa taifa.
 Waziri Mkuu  alisema kati ya shule 10 ,ambazo wanafunzi hao wanatoka, wawili  ni kutoka  shule za kata, ambao ni Ester Marcel toka shule ya sekondari ya wasichana ya Olele Kilimanjaro na Brighton Lema  toka shule ya sekondari ya Kitangiri, Mwanza.
“Napenda niwape pongezi za pekee wanafunzi hawa kwa jihudi  kubwa walizozionesha. Kufaulu kwao kunadhihirisha kwamba shule hizi za kata tukiweka bidii   kwa kuziwezesha zaidi  zitafanya vizuri zaidi kama ilivyo katika shule nyingine,” alisisitiza .
 Waziri Mkuu pia aliwataka walimu wote nchini kushirikiana na wazazi na serikali kwa pamoja kufundisha watoto kwa bidii ili waweze kufanya vizuri  katika masomo yao kama wanafunzi hao waliotunukiwa vyeti hivyo.
Kwa upande wake Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa alisema wanafunzi hao watazawadiwa  pakato (laptop) na sh. 200,000, pia   kila  shule iliyotoa mwanafunzi bora itazawadiwa  sh. milioni moja katika hafla  maalum  itakayofanyika jioni.
Wanafunzi hao wanatoka katika mchepuo wa PCM ambao ni 16 na mmojammoja toka mchepuo wa PGM, CBA, ECA na HKL.
Naye Spika wa Bunge la Jamhuri, Anna   Makinda  aliwataka wanafunzi hao kuwa makini na makundi kwa kuyasilikiza huku wakitumia akili zao  huku akitoa changamoto shule nyingine kujitahidi kufanya vizuri.

No comments:

Post a Comment