TANGAZO


Tuesday, August 14, 2012

Waziri Mkuchika atoa ufafanuzi kuhusu Taasisi za WAMA na EOTF, Bungeni mjini Dodoma

Waziri Mkuchika

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Utawala Bora, Kapteni George Mkuchika amesema kuwa  Taasisi ya Wanawake na Maendeleo(WAMA)  na Taasisi ya  Mfuko  wa Fursa Sawa kwa Wote (EOTF),  zilianzishwa na  kuandikishwa kwa mujibu wa sheria inayotawala taasisi hizo na wala hazitumii rasilimali za serikali.
Kauli hiyo ilitolewa  na Waziri Mkuchika leo, wakati akijibu swali Bungeni  la Mbunge wa  Viti Maalum(CHADEMA) , Naomi Kaihula ililoulizwa na Leticia Nyerere Viti Maalum (CHADEMA), kuwa  kumekuwepo na tabia ya wake wa marais hapa nchini kuunda NGO’S na kuzisajili kama taasisi zao binafsi wakati zinatumia rasilimali za serikali.
 Je Serikai itaweka lini utaratibu wa kufanya taasisi hizo ziwe za kisheria ili hata wake wa marais wanapomaliza muda wao wapokezane vijiti kama urais unavyofanywa.
Waziri Muchika akifafanua  kuhusu swali hilo, alisema  ni kweli zipo  taasisi zinazoendeshwa  wake  za  marais. Hivyo taasisi hizo hufanya shughuli zake kama zilivyo taasisi nyingine zisizo za kiserikali. Ipo taasisi ya WAMA  iliyoanzishwa na  Mke wa Rais  wa Awamu ya Nne Mama Salma  Kikwete na  EOTF  iliyoanzishwa na Mke wa Rais wa Awamu ya Tatu, Mama Anna Mkapa.
Aliongeza kuwa kama zilivyo taasisi zingine za hiari na zisizo za kiserikali (NGO,S). Taasisi hizo ziliundwa kutegemea na jinsi mke wa Rais anavyopenda kujishughulisha na shughuli za kijamii.
Mke wa Rais Kikwete, Mama Salma na Rais mstaafu Benjamin Mkapa, Anna Mkapa,  viongozi wa taasisi za WAMA na EOTF

Alisema inawezekana kabisa akatokea mke au mme wa Rais  ambaye hana utashi au mapenzi ya kujishughulisha na shughuli za kijamii. Hivyo kutokana na mazingira hayo serikali haioni sababu za kuweka utaratibu wa kufanya  taasisi hizo ziwe za kisheria ili wake / waume  za marais wanapomaliza muda wao wapokezane vijiti.
Aliongeza kuwa kwa kufanya hivyo tutakuwa tunawalazimisha  kufanya shughuli wasizo na utashi  nazo.
Akijibu swali la nyongeza la Leticia liliouliza kuwa  Watanzania wananufaikaje na taasisi hizo bila tofauti za kiitikadi. Waziri Mkuchika alisema hakuna anayefanya kazi kwa kubagua na alizipongeza taasisi hizo kwa kufanya kazi mijini na vijijini huku akiwataka Watanzania kuanzisha taasisi  mijini na vijijini .
 Alisema jumla  ya wanafunzi  939 wamenufaika  kielimu kupitia WAMA. Pia WAMA imetoa msaada wa vitanda na magodoro katika wodi za akina mama na imetoa  kiasi cha fedha sh. milioni 2 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya wanawake ya MEWATA, ambazo ni msaada kutoka Taasisi ya Nakayama, Japan.
Aidha, alisema ina mpango wa kutoa vifaa vya hospitali vyenye thamani ya dola za Marekani milioni tatu kupitia msaada wa Project Care, vinavyotarajia kuingia nchini.
 Alisema taasisi ya EOTF imetoa mafunzo kwa wajasiliamali mbalimbali.

No comments:

Post a Comment