Maelfu ya raia wa Tunisia wameandamana katika mji mkuu wa nchi hiyo, Tunis, kupinga mienendo ya serikali ya nchi hiyo inayoongozwa na wanasiasa wa Kiislamu wenye siasa kali, ambayo wanashuku inaweza kukandamiza haki za kina mama.
Serikali ya Tunisia, imezindua katiba mpya ambayo inataja kina mama kama wasaidizi wa wanaume.
Kina mama wengi walioandamana walibeba mabango ambayo yaliandikwa ''Amkeni kina mama na mtetee haki zenu''
Tunisia ilikuwa miongoni mwa mataifa yasiyozingatia utawala wa kidini katika mataifa ya Kiarabu kabla ya chama cha Kiislamu cha Ennahda kushinda uchaguzi mkuu mwaka uliopita.
Chama hicho kilitwaa madaraka ya nchi kufuatia machafuko yaliyopelekea kuondolewa madarakani kwa rais Zine el-Abidine Ben Ali Januari mwaka wa 2011.
Kwa mujibu wa katika ya nchi hiyo iliyoundwa mwaka wa 1956, wanawake walikuwa na haki sawa na wanaume lakini ilipiga marufuku wanaume kuwa na zaidi ya mke mmoja na wakati huo huo kutoa fursa ya talaka na ndoa kupitia mahakama.
Mbunge atetea katiba mpya
Mbunge mmoja wa chama hicho cha Ennahda, Farida al-Obeidi, ambaye ni mwanachama wa kamati ya bunge ya haki za kibinadam, amesema kipengee hicho cha katiba hakihujumu haki za kina mama kwa njia yoyote.
'' kipengee hicho kinatoa fursa kwa wanaume na wanawake kugawana majukumu na sio sawa kusema wanaume ni viumbe bora au wana haki zaidi kuliko kina mama'' alisema mbunge huyo.
Lakini mwenyekiti wa chama cha Demokrasia cha kina mama DWA, Ahlam Belhadj, ameikashifu serikali ya nchi hiyo na kusema kipengee hicho kinaidhinisha ubaguzi dhidi ya kina mama.
''Ikiwa tutanyamaza leo, basi hiyo itatoa fursa kwa mambo mengi makubwa kujitokeza'' alisema Bi Belhadj.
Maandamano hayo yalianza jana jioni baada ya kukamilika mwa mwezi mtukutu wa Ramadan.
No comments:
Post a Comment