Na Mery Kitosio, Arusha
MAANDALIZI ya zoezi la sensa ya kuhesabu watu na makazi kwa mkoa wa Arusha yamekamilika vya kutosha ambapo jumla ya makarani elfu 5037 wamechaguliwa kuendeleza shughuli hiyo sanjari na kukamilika kwa vifaa mbali mbali vitakavyotumika katika zoezi hilo.
Hayo yalisemwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Magesa Mulongo, alipokuwa akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake jijini humo leo, kuhusiana na kukamilika kwa zoezi hilo ambalo linatarajiwa kuanza agosti 26.
Aidha, alisema kuwa tayari maandalizi yote ya sensa kwa mkoa huo yameshakamilika ikiwa ni pamoja na kukamilika kwa makarani hao ambao walipatiwa mafunzo yaliyofungwa rasmi jana pamoja na kukamilika kwa vifaa vyote vinavyotarajiwa kutumika katika zoezi hilo.
“maandalizi ya sensa ni mazuri na tumejipanga vema katika kuhakikisha kuwa zoezi hili linaenda vizuri kwa kuwa tayari makarani wa zoezi hili wameandaliwa vizuri kwa kuwa wamepatiwa mafunzo ya kutosha hivyo wananchi watawatambua vya kutosha kwa kuwapa ushirikiano”alisema Mulongo.
Aliongeza kuwa jumla ya maeneo 3290 tayari yameshatengwa kwa ajili ya kuendeshea zoezi hilo ambapo alisema kuwa makarani hao wameshaanza kupita ili kuonana na viongozi mbali mbali ili wabaini ukomo wa maeneo yao watakayokuwa wanayafanyia kazi.
Mulongo alisema kuwa pia kukamilika kwa maandalizi ya zoezi hilo kumetokana na mafunzo waliyoyatoa kwa madiwani ,viongozi wa dini pamoja na viongozi wa vyama vya siasa ambapo makundi haya yamesaidia kwa kiwango kikubwa katika kuhamasisha watu ili washiriki katika zoezi hilo.
Aidha aliwataka wale watu wote wenye nia mbaya ya kuwatisha makarani hao wawapo kwenye zoezi hilo kutambua kuwa ulinzi utakuwepo kwa kila eneo husika na yeyote atakayebainika atachukuliwa hatua za kisheria kwa kuwa zoezi hilo sio la mtu binafsi bali ni la kitaifa.
Akizungumzia swala zima la baadhi ya watu waliodai kugoma kushireiki zoezi hilo kwa ajili ya imani alisema kuwa tayari wameshaongea na viongozi wa dini ambapo wameshaelwa umuhimu wa kushiriki kwani swala hilo halihusiani na mambo ya dini yeyeote.
Hata hivyo aliwasihi wananchi wote kutoa ushirikiano wa kutosha katika zoezi hilo huku akiwataka wale wenye migogoro isiwe chanzo cha kuwanyima kushiriki kuhesabiwa kwa kuwa takwimu ni kwa faida yao na watakuwa wanjinyima haki zao za msingi
No comments:
Post a Comment