![]() |
| Profesa Issa Shivji wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere |
NIMESHITUSHWA na gazeti moja la kila siku (Tanzania Daima 2012) lilonipandikizia maneno katika kichwa chake cha hab alar it akrweahme b7a A ‘Sghoisvtjii , Lwaitama wataka Muungano uvunjwe’. Siwezi nikamsemea Dr. Lwaitama lakini kwa
upande wangu sijasema wala kumaanisha kwamba ‘Muungano uvunjwe’. Nikitoa mchango wangu baada ya mada mbili kuwasilishwa na Prof. Abdul Sheriff na Dr. Azaveli Lwaitama, nilisisitiza mambo haya matatu ya msingi. Mosi, kwamba wasomi, wakiwemo wanahabari, wana jukumu zito la kutokupinda
ukweli wa kihistoria kwa lengo la kuhalalisha mtazamo na msimamo wao kuhusu
Muungano. Nikatoa mfano wa jinsi Merehemu Sheikh Karume anavyodekezwa
katika msimamo wake juu ya Muungano. Wasemaji hapa bara wanamsifu kwa kuwa
muasisi mwaminifu na mshabiki mkubwa wa Muungano tangu mwanzo. Huko
Zanzibar, wasemaji hawachoki kumnukuu Mzee Karume kuwa tangu mwanzo yeye
hakutaka Muungano isipokuwa alikuwa anafikiria Shirikisho.
Wanaendelea kusema kwamba aliposaini Mkataba wa Muungano, Mzee Karume
alifikiri kwamba anasaini Shirikisho la Serikali tatu, lakini kutokana na kiwango cha
elimu yake hakuelewa vizuri mantiki na maana ya alichokuwa anasaini.
Nikaendelea kueleza kwamba maelezo haya yote mawili hayaungwi mkono na
ushahidi wa kihistoria. Ukweli ni kwamba, Mzee Karume aliingia katika Muungano
kutokana na hesabu zake mwenyewe za kisiasa. Muungano kwake ulikuwa njia ya
kuondoa upinzani, au upinzani tarajiwa, wa utawala wake. Yaani ilikuwa ni tendo la
mwanasiasa yeyote yule kudumisha utawala wake (political survival).
Na kwa watawala wote wa Zanzibar waliomfuata, wakiwemo wa upinzani, ndivyo
ilivyokuwa. Wamekuwa wakitumia mwavuli wa muungano wakati utawala wao uko
hatarini na kushawishi wananchi wao dhidi ya muungano wakitafuta umaarufu wa
kisiasa.
Nikitoa mfano nikasema kwamba kuna taarifa kwamba chama kimoja huko Zanzibar
kinapandikiza pendekezo la ‘muungano wa mkataba, sio wa katiba’ bila ya kueleza
waziwazi maana yake. Ukweli ni kwamba huwezi ukawa na muungano wa mkataba
bila kwanza kuuvunja muungano. Kwa hivyo, wanachoshawishi moja kwa moja ni
kuuvunja muungano. Basi waseme hivyo badala ya kujificha nyuma ya pazia la
‘muungano wa mkataba’.
Jambo la pili nililorudia ni kwamba tuliangalie suala zima la muungano kwa mtazamo
na maslahi na matakwa ya Umma wa Zanizbar na Umma wa Tanzania bara, hususan
matabaka ya hali ya chini. Katika hali yao kimaisha – kiuchumi na kisiasa – hakuna
tofauti kati ya wananchi wa Zanzibar na wananchi wa Tanzania bara. Uduni wa hali
yao ni uleule; ukosefu wa ajira ni uleule; kutokuwa na mfumo wa dhati wa
demokrasia unaojali walalahoi ni kulekule.
Kwa hivyo, umuhimu kwao ni mshikamano wao kuboresha mifumo ya uchumi na
siasa. Wasiburuzwe na wanasiasa na vyama vyao kwa maslahi yao binafsi ya muda
mfupi ya kudumisha, au kuingia kwenye, utawala.
2
Jambo la mwisho nililogusia ni kwamba kiini cha suala la muungano si idadi ya
serikali (mbili au tatu) bali ni mgawanyo wa madaraka (distribution of power) kati ya
dola la Zanzibar na dola la Muungano. Na katika hili kila muungano duniani ni wa
kipekee kutokana na hali halisi yao ya kihistoria na uwiano wa kisiasa. Sisi pia
tukiwashirikisha wananchi kikamilifu na tukaelewa vizuri matakwa yao tunaweza
kubuni muundo wetu wa muungao ambao ni wa kipekee bila kujali idadi ya serikali.
Nimeona niweke wazi mtazamo wangu kwa sababu ya baadhi ya vyombo vya habari
kuwa na hulka ya kupotosha mambo kutokana na ushabiki wao bila kujali madhara
yanayoweza kutokea.
Mwishoni ningependa kusema kwa dhati kwamba uvunjaji wa muungano hauwezi
kuwa kwa manufaa ya walio wengi. Ukweli ni kwamba unaweza ukasambaratisha
nchi na jamii zetu pande zote mbili za muungano. Tukianza kubaguana kati ya
Watanganyika na Wazanzibari, tutaendelea kubaguana kwa msingi wa Uislamu na
Ukristo, na Usukuma na Uchaga, Uarabu na Uafrika, weusi na weupe bila kikomo.
Kama alivyosema Mwalimu, ukishaonja nyama ya mtu basi utaendelea kumtafuna.
Issa Shivji
Profesa wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere,
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Agosti 8, 2012


No comments:
Post a Comment