Umewahi kupuuza ujumbe wa mpenzi au mchumba wake? Tahadhari: huenda hilo likatumiwa dhidi yako kortini.
Mwanamke mmoja nchini Taiwan ameruhusiwa kumpa talaka mume wake, kwa kutumia ishara kwamba ujumbe wake aliomtumia mumewe ulisomwa kama ushahidi kwamba mumewe alikuwa akimpuuza.
Mtandao wa kijamii wa Line unaonesha mumewe alikuwa akifungua ujumbe huo, lakini hakujibu.
Jaji amemkubalia ombi la kumtaliki mumewe.
Mwanamke huyo alitumia alama za rangi ya buluu ambazo hutumiwa na mitandao kama vile Line na WhatsApp mtu anaposoma ujumbe kudai kwamba mumewe alikuwa ameupokea ujumbe.
Jaji katika mahakama ya masuala ya kifamilia Hsinchu amesema hali kwamba mwanamume huyo alipuuza ujumbe huyo ni ushahidi kwamba ndoa kati ya wawili hao haiwezi 'kuokolewa' na vyombo akawaruhusu kupatiana talaka.
Katika kipindi cha miezi sita hivi, mwanamke huyo ambaye jina lake la ukoo ni Lin, alimtumia mumewe ujumbe mara kadha, wakati mmoja ikiwa ni baada yake kulazwa hospitalini baada ya kuhusika katika ajali barabarani, kwa mujibu wa Jaji Kao.
Katika ujumbe mmoja, alimwambia mumewe kwamba alikuwa katika chumba cha dharura hospitalini na akamwuliza ni kwa nini anasoma ujumbe wake lakini hamjibu.
Ingawa mumewe alimtembelea hospitalini mara moja, mahakama ilisema kwamba hali kwamba alikuwa akipuuza ujumbe wake ni msingi tosha wa kumpa talaka.
"Mshtakiwa hakumjulia hali mlalamishi, na habari aliyotumiwa na mlalamishi aliisoma lakini hakujibu," mahakama ilisema kwenye uamuzi wake.
Ilikuwa ni baada ya mwezi mmoja au miwili hivi baada ya ajali hiyo ambapo mumewe alimtumia ujumbe mfupi.
"Ujumbe wake ulikuwa kumhusu mbwa wao na alimfahamisha pia kwamba kulikuwa na barua iliyotumwa kwake, lakini hakuonesha ishara za kutaka kujua hali yake," Jaji Kao alisema.
Wawili hao walifunga ndoa 2012.
Mwanamke huyo ambaye amewahi kuolewa awali ana miaka 50 hivi na mumewe ana miaka 40 hivi.
No comments:
Post a Comment