Mamia ya waogeleaji waliokuwa utupu walijumuika kwa pamoja kuogelea katika mto wenye maji baridi katika jaribio la kuvunja rekodi nchini Finland.
Washiriki walikuwa wanataka kuvunja rekodi ya dunia ya watu wengi zaidi kuwahi kuogelea kwa pamoja wakiwa utupu.
Watu 789 waliokuwa pia wanahudhuria tamasha ya muziki mashariki mwa Finland walijitosa kwenye maji kuogelea wakiwa utupu, waandalizi wanasema.
Walifanikiwa kuvunja rekodi ya awali iliyokuwa imewekwa na waogeleaji nchini Australia, kwa kuzidi watu hao kwa watu watatu, taarifa zinasema.
Waandalizi wamesema sasa wanasubiri rekodi yao ithibitishwe na maafisa wa Guinness World Records.
Hii ni mara ya tatu kwa jaribio la kuvunja rekodi hiyo kuandaliwa nchini Finland, mtandao wa habari wa Yle umesema.
Majaribio ya awali mjini Helsinki mwaka 2015 na mwaka 2016 yalivutia watu takriban 300.
Waandalizi wa tamasha hiyo ya muziki ya Ilosaari Rock mjini Joensuu walikuwa wamekusubia kuwapata watu 1,000.
Sawa na ilivyokuwa katika majaribio ya awali, ni watu mia kadha waliokuwa wamejitolea kushiriki.
Lakini muda mfupi kabla ya jaribio kufanywa, jua lilichomoza na hilo liliwafanya watu wengi zaidi kujitokeza, Yle wanasema.
Rekodi waliokuwa wakijaribu kuivunja iliwekwa mwaka 2015 mjini Perth na watu 786 waliokuwa wanajaribu kuhamasisha watu kuipenda miili yao.
Kuogelea nje kwenye mito na bahari ni utamaduni wa miaka mingi nchini Finland, ambapo "avantouinti" - kuogelea katika shimo la barafu - hutangazwa na bodi ya utalii nchini humo kama shughuli inayosaidia kusisimua mwili.
No comments:
Post a Comment