Mkimbiza Mwenge Kitaifa, Fredrick Joseph
Na Tiganya Vincent-Nzega
16 Julai 2017
VIONGOZI mkoani Tabora wametakiwa kuandaa mazingira ambayo yatawavutia wawekezaji kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vya kuchakata na kuzalisha sigara mkoani hapa ili mkulima wa zao hilo, aweze kunufaika zaidi kuliko ilivyo sasa.
Kauli hiyo ilitolewa jana katika Kijiji cha Sigiri wilayani Nzega na Mkimbiza Mwenge Kitaifa Bw. Fredrick Joseph wakati akitoa ujumbe wa mjumbe kwa mwaka 2017.
Alisema kuwa wa Tabora ni Mkoa unaozalisha Tumbaku kwa wingi hapa nchini kwa hiyo ipo haja ya kujenga Viwanda mkoani hapa ili viweze kusaidia kuongeza thamani ya zao hilo kwa ajili ya kumsaidia mkulima badala ya kusafirisha tumbaku ikiwa bado haijasindikwa.
Bw. Joseph alisema kuwa tumbaku ni moja wapo wa zao linaloliingizia Taifa fedha nyingi za Kigeni ni vema wakulima wake wakanufaika na fursa hiyo walau kwa kuwa na kiwanda kinachosaidia kuongeza thamani yake.
Aliongeza kuwa hatua ya kusafirisha tumbaku ambayo haijachakatwa nje ya Mkoa wa Tabora haimsaidii sana mkulima kumpa mapato mengi kama zao hilo lingesindikwa hapa na kuzalisha bidha kama sigara.
Aidha alitoa wito kwa wakulima wa tumbaku kulima kwa wingi zao hilo na kutumia fedha zake kwa ajili ya kujiletea maendeleo badala ya kuendeleza starehe na hasana.
Bw. Joseph aliongeza kuwa ni vema wanapopata fedha za tumbaku wakazitumia katika kuboresha maisha yao ikiwemo kujenga nyumba bora na uendelezaji watoto wao kielimu.
Katika hatua nyingine Mkimbiza Mwenge huyo wa Kitaifa alitoa wito kwa wakazi wa Tabora kufuga nyuki kwa ajili ya kujipatia kipato na kujiendeleza kiuchumi.
Aliongeza kuwa ni vema wakaachana na ukataji miti ovyo kwa ajili ya uchomaji mkaa badala yake wajiunge na shughuli hiyo ambao ni rafiki kwa mazingira na inatija kubwa.
Akipokea Mwenge wa Uhuru Mkuu wa Mkoa wa Tabora Bw. Aggrey Mwanri alisema kuwa Mwenge huo unatarajiwa kukimbizwa katika Halmashauri zote nane za Mkoa huo.
Alisema jumla ya miradi 51 yenye thamani ya shilingi bilioni 21 itawekewa wawe za Msingi na kuzinduliwa mkoani hapo.
Bw. Mwanri alisema kuwa kati ya miradi yote jumla ya shilingi bilioni 9 ni miradi iliyotokana na nguvu za wananchi.
Mwenge wa Uhuru umewasili leo(jana-16 Julai 2017) ukitokea Mkoani Shinyanga ambapo ulikimbizwa katika Halmashauri 6 za Mkoa huo na Tabora inatarajia kukabidhiwa Mkoani Kigoma tarehe 24 Mwezi huu.
Kauli mbiu ya Mwenge mwaka huu shiriki kukuza uchumi wa viwanda kwa maendeleo ya nchi.
No comments:
Post a Comment